Sherehe ya Tokeo la Bwana, Epifania ni Ufunuo wa Kristo Yesu, Mwanga wa Mataifa. Sherehe ya Tokeo la Bwana, Epifania ni Ufunuo wa Kristo Yesu, Mwanga wa Mataifa. 

Sherehe ya Tokeo la Bwana: Mamajusi na Wachungaji Safi! Herode Katili!

Tokeo la Bwana ni sherehe ya ufunuo wa Kristo Yesu, Mwanga wa Mataifa, na Yeye mwenyewe anasema “Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye mimi hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima wa milele” (Yoh.8:12). Huu ni wito kwa waamini kulitafakari na kulimwilisha Fumbo la Mwanga katika ushuhuda wa maisha ya Kikristo yenye mvuto na mashiko!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Sherehe ya Tokeo la Bwana, au Epifania kama inavyojulikana kwa lugha ya Kigiriki ἐπιφάνεια, epifaneia, ni sherehe ya ufunuo wa Kristo Yesu, Mwanga wa Mataifa, na Yeye mwenyewe anasema “Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye mimi hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima wa milele” (Yoh.8:12). Huu ni wito kwa waamini kulitafakari na kulimwilisha Fumbo la Mwanga katika ushuhuda wa maisha ya Kikristo yenye mvuto na mashiko. Sherehe ya Tokeo la Bwana ni Siku pia ya Utoto Mtakatifu. Maadhimisho ya Mwaka 2021 yanaongozwa na kauli mbiu “Tunogeshe udugu wa kibinadamu”. Mwaka 2021 umetawaliwa sana na athari za janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari zake kuhusu Sherehe ya Tokeo la Bwana, mara nyingi anapenda kuwaangalisha waamini kuwatazama na kuwatafakari Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali waliojifunga kibwebwe, wakathubutu kufunga safari kwenda kumtafuta Mtoto Yesu, Mfalme wa Wayahudi aliyekuwa amezaliwa mjini Bethlehemu, nyumba ya mikate, huku wakiongozwa na nyota angavu!

Hawa ni watu waliokuwa na hekima, busara na utajiri wa mali na utu wema. Ni watu waliokuwa na furaha kubwa walipomwona Mtoto Yesu, Maria na Yosefu. Wakaanguka na kumsujudia. “Nao walipokwisha kufungua hazina zao, wakamtolea tunu: dhahabu na uvumba na manemane.” Mt. 2: 11-12. Baba Mtakatifu Francisko anasema zawadi hizi zinafumbata maana na utume wa Kristo Yesu hapa duniani. Dhahabu ni kielelezo cha heshima ya hali ya juu kwa Kristo Yesu kama Mfalme. Huu ni ufalme wa kweli na uzima; ufalme wa utakatifu na wa neema; ufalme wa haki, mapendo na amani. Uvumba unadokeza Umungu wa Kristo Yesu. Hii ni alama ya upendo na sadaka itakayofikia kilele chake Mlimani Kalvari. Manemane inaashiria ubinadamu wake ambao umefunuliwa katika Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu. Mamajusi ni mfano bora wa kuigwa katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayofumbatwa katika furaha yenye upendo. Hii ni changamoto ya kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu na kwa jirani. Mamajusi hawakwazwi na umaskini, mazingira na hali ya Mtoto Yesu.

Wanamtambua kuwa ni Mfalme, wanampigia magoti na kumsujudu. Wanamtambua Mwenyezi Mungu anayeratibu kazi ya uumbaji na kuongoza mkondo wa historia. Huyu ni Mungu anayewakweza wanyonge na kuwaangusha wakuu kutoka katika viti vyao vya enzi. Rejea kwenye Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: “Admirabile signum” yaani “Ishara ya Kushangaza”: Maana na Umuhimu wa Pango la Noeli” namba 5-7. Baba Mtakatifu anawataja pia Makuhani na waandishi wa watu, mabingwa katika kuchambua na kuyatafakari Maandiko Matakatifu, kiasi hata cha kuonesha ni mahali gani ambako Mtoto Yesu alizaliwa. Lakini hili ni kundi la watu wasiojali wala kuguswa na tukio kubwa la kuzaliwa kwa Mtoto Yesu, kama ilivyokuwa hata kwa Mfalme Herode. Huyu alifadhaika, na Yerusalemu pia pamoja naye. Hili ni kundi ambalo lilimezwa mno na malimwengu kiasi cha kumwona Kristo Yesu kuwa ni tishio katika maisha yao. Matokeo yake ni kutaka kuufifisha Mwanga wa Mataifa.Ni kundi ambalo limejibovusha kwa kupenda mno anasa za dunia, mali, utajiri na faida kubwa hata kwa gharama ya maisha ya watu wengine.

Watu wajibidiishe kumtafuta Kristo Bwana, Njia, Ukweli na Uzima, ili kukuza na kuimarisha imani, mapendo na matumaini ya watu wa Mungu. Kristo Yesu ni Mwanga wa Mataifa. Waamini wanaweza kukutana na Kristo Yesu kwa njia ya: Neno lake, Sakramenti za Kanisa, Matendo ya huruma kwa maskini pamoja na katika historia ya maisha yao! Kundi la tatu ni wachungaji “Ikawa, malaika hao walipoondoka kwenda zao mbinguni, wale wachungaji waliambiana, Haya, na twendeni mpaka Bethlehemu, tukalione hilo lililofanyika, alilotujulisha Bwana. Wakaenda kwa haraka wakamkuta Mariamu na Yusufu, na yule mtoto mchanga amelala horini. Walipomwona wakatoa habari waliyoambiwa juu ya huyo mtoto. Wote waliosikia wakastaajabu kwa hayo waliyoambiwa na wachungaji. Lakini Mariamu akayaweka maneno hayo yote, akiyafikiri moyoni mwake. Wale wachungaji wakarudi, huku wanamtukuza Mungu na kumsifu kwa mambo yote waliyosikia na kuyaona, kama walivyoambiwa.” Lk. 2:15-20.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, wachungaji wamekuwa mashuhuda wa kwanza kupokea zawadi ya wokovu inayofumbatwa katika Fumbo la Umwilisho. Wachungaji wakabahatika kukutana na upendo wa Mungu, wakashikwa na mshangao wenye shukrani. Maskini na wanyenyekevu wa moyo ni walengwa wakuu wa Habari Njema ya Wokovu na kwa hakika ndio wale wanaoweza kutambua kirahisi uwepo wa Mungu kati ya waja wake. Katika umaskini wao, waamini wanahimizwa kutafuta na kuambata kile kilicho cha maana na kuishi kwa ajili yake. Ni kielelezo cha mapinduzi na matumaini mapya, ili kusimamia utu, heshima na haki msingi za binadamu. Haya ni mapinduzi ya utamu wa upendo, njia muafaka kuelekea katika mchakato wa ujenzi wa ulimwengu bora zaidi, unaoheshimu na kuthamini utu, heshima na udugu wa kibinadamu, ambamo hakuna mtu anayetengwa wala kusukumizwa pembezoni mwa jamii. Rejea kwenye Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: “Admirabile signum” yaani “Ishara ya Kushangaza”: Maana na Umuhimu wa Pango la Noeli”. Nambari, 6.

Papa: Tokeo la Bwana
05 January 2021, 16:12