Baba Mtakatifu Francisko asema: Umoja wa Wakristo ni matunda ya sala na ushuhuda unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili ili watu wa Mataifa waweze kuona na kusadiki! Baba Mtakatifu Francisko asema: Umoja wa Wakristo ni matunda ya sala na ushuhuda unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili ili watu wa Mataifa waweze kuona na kusadiki! 

Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo: Umoja Ni Matunda ya Sala

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu: “Majadiliano ya Kiekumene” wanakazia kuhusu: Ushirikiano katika sala: wongofu wa moyo, utakatifu wa maisha na sala za kibinafsi na kijumuiya kwa ajili ya umoja wa Wakristo kwani hii ni sehemu muhimu sana ya uekumene wa sala. Lengo ni kumsaidia Kristo Yesu aweze kutekeleza ndoto yake “ili wote wawe na umoja”. SALA.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kuanzia tarehe 18 hadi 25 Januari 2021 Sikukuu ya kuongoka kwa Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa, Wakristo wanaadhimisha Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo. Kauli mbiu ya maadhimisho haya ni “Kaeni katika pendo langu, ili mzae matunda”. Rej. Jn 15-5-9. Kristo Yesu ndiye Mzabibu wa kweli ni ufafanuzi unaotolewa katika Injili ya Yohane 15:1-17. Jumuiya ya Wamonaki 50 kutoka katika Makanisa na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo wa Grandchamp iliyoko nchini Uswisi ndiyo iliyopewa dhamana ya kuandaa masomo, sala na tafakari kwa mwaka 2021. Tema hii ni kielelezo cha wito wao unaojielekeza kwa namna ya pekee katika: Sala, upatanisho na umoja wa Makanisa sanjari na familia kubwa ya binadamu katika ujumla wake. Wamonaki hawa wanarutubisha maisha na utume wao kwa njia ya: Sala ukimya na tafakari ya kina ya Neno la Mungu. Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko Jumatano tarehe 20 Januari 2021 aliyoiendesha kutoka kwenye Maktaba yake binafsi, imeongozwa na Sala ya Yesu kwa ajili ya Mitume wake: Yesu akainua macho yake kuelekea mbinguni, akasema… Mimi nawaombea hao … ulionipa, kwa kuwa hao ni wako; na wote walio wangu ni wako, na walio wako ni wangu; nami nimetukuzwa ndani yao. Wala si hao tu ninaowaombea; lakini na wale watakaoniamini kwa sababu ya neno lao. Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma. Rej. Yn. 17:1.9. 20-21.

Hii ni Sala ambayo Kristo Yesu aliisali mara tu baada ya Karamu ya Mwisho, akiwaombea wanafunzi wake ili waweze kuwa wamoja. Huu ni wosia wa maisha ya kiroho kutoka kwa Kristo Yesu kwa ajili ya wanafunzi wake, muda mfupi kabla ya kuteswa, kufa na hatimaye, siku ya tatu kufufuka kwa wafu! Hii ni Sala kwa ajili ya kuombea Umoja wa Wakristo. Kumbe, mchakato wa kuombea umoja wa Wakristo duniani ni zawadi na neema kutoka kwa Kristo Yesu wanayopaswa kuiomba kwa njia ya sala na wala si nguvu wala jitihada zao binafsi. Hii ni sehemu ya muhtasari wa katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko ambaye amekazia kwamba, kila mwamini anapaswa kujizatiti katika sala kwa ajili ya kuombea umoja wa Wakristo. Hii inatokana na ukweli kwamba, si rahisi sana kwa wao kuweza kulinda na kudumisha umoja, hata ndani mwao kama ilivyokuwa hata kwa Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa anayezungumzia kuhusu uhuru wa Mungu aliye mtawala na mashindano ya makusudi ya mtu. Rej. Rum. 7:19.

Kuna utashi wa kutaka kutenda mema, lakini daima mwanadamu anajikuta akitenda mabaya. Hiki ndicho kiini cha kinzani, migawanyiko na mipasuko inayoendelea kuzunguka kati ya watu, ndani ya familia, katika jumuiya na hata kati ya waamini wenyewe bila kusahau kwamba, mgawanyo huu unawameng’enya hata kutoka katika undani wa maisha yao. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wameliona hili wanapogusia kuhusu maswali mazito zaidi yanayomkabili mwanadamu. Kinzani na mipasuko inayoutesa ulimwengu mamboleo yanahusiana na lile la ndani zaidi lenye mizizi yake katika moyo wa binadamu. Kwa hiyo huteswa na mgawanyiko huo uliopo ndani yake mwenyewe ambao kutokana nao huzuka pia fitina nyingi na kubwa katika jamii. Rej. GS. No. 10. Ni katika muktadha huu, anasema Baba Mtakatifu Francisko suluhu ya mapambano dhidi ya mgawanyiko na mipasuko hiyo si “mzigo anaoweza kutwishwa” mtu mwingine, kwa sababu kinzani moja huzaa kinzani nyingine.

Jambo la msingi ni kuanza kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu kwa kusali na kuomba amani, upatanisho na umoja. Hii ni dhamana ambayo kwanza kabisa inapaswa kutekelezwa na Wakristo. Umoja wa Wakristo unaweza kufikiwa tu kwa kutambua kwamba, haya ni matunda ya sala. Jitihada za kidiplomasia, majadiliano ya kiekumene sanjari na tafiti mbalimbali za kitaalimungu, ni muhimu lakini peke yake, hazitaweza “kufua dafu”, ndiyo maana Kristo Yesu anawataka wafuasi wake kusali ili kuombea umoja. Sala ya waamini kwa ajili ya kuombea umoja wa Wakristo inasimikwa katika fadhila ya unyenyekevu inayowawezesha kushiriki katika ile Sala ya Kristo Yesu ambaye anawaambia kwamba, ikiwa kama watakaa ndani yake na maneno yake yakikaa ndani yao, wakiomba lolote watakalo watatendewa! Rej. Jn. 15:7. Baba Mtakatifu anawaswalisha wakristo, ikiwa kama kweli wanasali kwa ajili ya kuombea umoja wa Wakristo? Huu ni utashi wa Kristo Yesu mwenyewe, lakini inawezekana kana kwamba, Wakristo hawajasali vya kutosha kwa ajili ya kuombea umoja wao.

Umoja wa Wakristo ni muhimu ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba Kristo Yesu ametumwa na Baba yake wa mbinguni. Malumbano ya hoja za Kitaalimungu hazitaweza kuusadikisha ulimwengu isipokuwa ushuhuda wa upendo, unaowaunganisha Wakristo na kuwafanya kuwa majirani wema kwa watu wote na kwa njia hii, watu wataweza kuamini. Nyakati za majanga, umoja na mshikamano wa kidugu ni muhimu sana, kwani umoja ni nguvu na unapaswa kushinda mambo yote yanayowagawa na kuwasambaratisha Wakristo. Huu ni wakati wa kusimama kidete na kujielekeza zaidi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni wakati wa kuambata hija ya pamoja itakayowawezesha Wakristo kuwa na umoja kamili na unaoonekana. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa wema na ukarimu wake wa ajabu na kwamba, katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene, Wakristo wamepiga hatua kubwa, lakini jambo la msingi upendo, moyo wa sala na imani vinapaswa kushuhudiwa zaidi. Haya ni matunda na kazi ya Roho Mtakatifu, Wakristo kamwe hawawezi tena kurejea nyuma!

Kusali maana yake ni kupambana katika ujenzi wa umoja wa Wakristo, kwa kutegemea nguvu na msaada wa Roho Mtakatifu. Shetani, Ibilisi, anawapepeta si katika masuala ya taalimungu ya hali ya juu, bali ni katika udhaifu wao. Shetani, Ibilisi anakuza makosa na kuonesha mapungufu ya waamini wengine. Anapandikiza mbegu ya chuki na uhasama, anachochea malumbano na kukuza kinzani na migawanyiko. Anafurahia watu wanaposigana na kusambaratika! Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mwenyezi Mungu anazo njia zake kwani anawawachukua na kuwapokea watoto wake jinsi walivyo; anatambua kwamba, kimsingi wanazo tofauti zao; ni wadhambi, lakini hata hivyo bado anawahimiza kujikita katika mchakato wa ujenzi wa umoja wa Wakristo. Waamini wanaweza kufanya tathmini binafsi ili kuangalia ikiwa kama katika makazi yao, wamekuwa ni watu wanaopandikiza “ndago” za chuki na kinzani, au wamekuwa ni watu wanaojielekeza zaidi katika kuhamasisha na kukuza umoja kwa kutumia nyenzo ambazo wamekirimiwa na Mwenyezi Mungu yaani: Sala na Upendo! Watu wanapenda kukoleza chuki na uhasama kwa umbea na shutuma dhidi ya wengine. Umbea ni silaha kali mikononi mwa Shetani, Ibilisi, kwani kwa njia hii, anapandikiza mbegu ya utengano inayoigawa jumuiya ya Wakristo, familia na marafiki. Lakini, Roho Mtakatifu anawahamasisha katika mchakato wa umoja!

Baba Mtakatifu anasema kauli mbiu ya maadhimisho haya ni “Kaeni katika pendo langu, ili mzae matunda”. Rej. Jn 15-5-9. Upendo ndiyo fadhila inayopewa kipaumbele cha pekee kwa mwaka 2021. Mizizi ya umoja wa Wakristo ni upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, anayewawezesha kuvuka mipaka ya maamuzi mbele, ili kuweza kuangaliana kama ndugu wanaopaswa kuheshimiana na kupendana daima. Kwa njia hii, waamini wataweza kugundua kwamba, Wakristo wa Makanisa na Madhehebu mengine, pamoja na Mapokeo na historia yao, wao ni zawadi ya Mungu inayoonekana katika maeneo na jumuiya zao: kijimbo na kiparokia. Huu ni mwaliko wa kuanza kusali kwa ajili ya kuwaombea na pale inapowezekana kushiriki na kushikamana nao katika sala kwa kusali pamoja. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha katekesi yake kuhusu Sala ya Kuombea Umoja wa Wakristo kwa kusema, Wakristo wataweza kujifunza kuwapenda na kuwathamini. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika Tamko lao “Unitatis redintegratio” yaani kuhusu “Majadiliano ya Kiekumene” wanakazia kuhusu: Ushirikiano katika sala: wongofu wa moyo, utakatifu wa maisha na sala za kibinafsi na kijumuiya kwa ajili ya umoja wa Wakristo kwani hii ni sehemu muhimu sana ya uekumene wa sala. Huu ndio mwanzo wa mchakato wa sala ya kiekumene ili kumsaidia Kristo Yesu aweze kutekeleza ndoto yake “ili wote wawe na umoja”. Rej. UR. 8.

Papa: Ushuhuda

 

20 January 2021, 15:30