Domenika ya Neno la Mungu: Zawadi ya Neno la Mungu kwa watu wote kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano. Domenika ya Neno la Mungu: Zawadi ya Neno la Mungu kwa watu wote kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano. 

Dominika ya Neno la Mungu: Zawadi ya Neno la Mungu Kwa Watu Wote!

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika ya Neno la Mungu amewaambia waamini kwamba, Neno la Mungu ni zawadi kubwa ambayo Mwenyezi Mungu amewakirimia waja wake katika Karne ya 21. Kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, leo hii kuna uwezekano mkubwa wa Kusoma, Kusikiliza na Kuona Maandiko Matakatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika Barua yake Binafsi, Motu Proprio “Aperuit illis” yaani: “Aliwafunulia akili zao” iliyochapishwa kunako tarehe 30 Septemba 2019 ameanzisha Dominika ya Neno la Mungu ambayo imeadhimishwa tarehe 24 Januari 2021: “Aliwafunulia akili zao wapate kuelewa na Maandiko” (Lk 24:45). Kitendo hicho ni kati ya vitendo vya mwisho alivyovitenda Bwana mfufuka, kabla ya kupaa kwake mbinguni. Alionekana kwa wanafunzi wake walipokuwa wamekusanyika pamoja, akamega mkate pamoja nao, akawafunulia akili zao wapate kuelewa na Maandiko Matakatifu. Kwa watu wale waliokuwa wameshikwa na hofu na kukata tamaa, alifunua maana ya fumbo la Pasaka: yaani kwamba, kadiri ya mpango wa milele wa Mungu Baba, Yesu alipaswa kuteswa na kufufuka kutoka kwa wafu ili awajalie watu wote wongofu na msamaha wa dhambi (taz. Lk. 24:26.46-47); pia aliahidi kumpeleka Roho Mtakatifu atakayewapa nguvu ya kuwa mashahidi wa Fumbo hili la wokovu (taz. Lk 24:49).

Maadhimisho ya Dominika ya Neno la Mungu tarehe 24 Januari 2021 yamenogeshwa na kauli mbiu “Mkishika neno la uzima”. Flp. 2:16. Askofu mkuu Salvatore Rino Fischella, Rais wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji Mpya ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na kutangazwa mubashara na vyombo mbalimbali vya mawasiliano na mitandao ya kijamii. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika ya Neno la Mungu amewaambia waamini kwamba, Neno la Mungu ni zawadi kubwa ambayo Mwenyezi Mungu amewakirimia waja wake katika Karne ya 21. Kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, leo hii kuna uwezekano mkubwa wa Kusoma, Kusikiliza na Kuona Maandiko Matakatifu.

Mtakatifu Jerome (Jina kamili ni Eusebius Sophronius Hieronymus) kwa agizo la Papa Damasi wa kwanza, kwa muda wa miaka 23 alifanya kazi ya kutafsiri na kupanga vitabu vya Biblia kwa lugha ya Kilatini, maarufu kama “Vulgata” iliyopitishwa na Mababa wa Mtaguso wa Trento (1545-1563) kwamba inafaa kufundishia imani. Alifariki dunia tarehe 30 Septemba 420 akiwa ameliachia Kanisa utajiri mkubwa wa Maandiko Matakatifu. Mama Kanisa tarehe 30 Septemba 2020 ameadhimisha kumbukumbu ya miaka 1600 tangu Mtakatifu Jerome alipofariki dunia. Wakati huo huo, Tarehe 30 Septemba 2020, Sikukuu ya Mtakatifu Jerome, Padre na Mwalimu wa Kanisa, Baba Mtakatifu Francisko alitia “mkwaju” kwenye Waraka wa Kitume Unaojulikana kama: "Scripturae Sacrae Affectus" Yaani “Waraka wa Kitume Juu ya Upendo Kwa Maandiko Matakatifu, Miaka 1600 Tangu Alipofariki Dunia Mtakatifu Jerome”.

Mtakatifu Jerome, Padre na Mwalimu wa Kanisa aliyeweka Maandiko Matakatifu kuwa kiini cha maisha yake, awasaidie waamini kupyaisha ndani mwao ari, moyo na upendo wa kusoma, kutafakari na kumwilisha Maandiko Matakatifu katika uhalisia wa maisha yao. Waamini wajenge utamaduni wa kujadiliana na Mwenyezi Mungu kwa njia ya Maandiko Matakatifu. Utambulisho wa Wakristo unafumbatwa kwa namna ya pekee, katika mahusiano ya dhati kati ya: Kristo Mfufuka, Maandiko Matakatifu na Jumuiya ya waamini. Ndiyo maana Mtakatifu Jerome anasema “Kutojua Maandiko Matakatifu ni kutomfahamu Kristo”. Liturujia ya Kanisa na Sala ni fursa ya kuzungumza na Mwenyezi Mungu.

Katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu Dominika ya Neno la Mungu, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Wakati wa Liturujia ya Neno la Mungu, Somo la kwanza limetangazwa na Bwana Pierfrancesco Favino, mwandishi wa habari kutoka Kituo cha Televisheni cha Taifa, RAI. Mlemavu wa macho amesoma Somo la Pili kwa kutumia maandishi ya nukta nundu yaliyogunduliwa na Braille. Liturujia ya Neno la Mungu imepewa uzito na heshima ya juu kabisa katika maadhimisho ya Dominika ya Neno la Mungu. Mimbari ni ile iliyotumika wakati wa maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Mwishoni mwa Ibada ya Misa, baadhi ya waamini kutoka katika medani mbali mbali za maisha wamepewa Biblia Takatifu, kuonesha umuhimu wa amana na utajiri wa Maandiko Matakatifu katika maisha na utume wa Kanisa. Kwa namna ya pekee kabisa, mlemavu wa macho amepewa nakala ya Injili ya Marko ambayo imeandikwa kwa kutumia maandishi ya nukta nundu.

Hii ni sehemu ya mbinu mkakati wa Mama Kanisa kuendelea kujikita katika mchakato wa uinjilishji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Maadhimisho ya Dominika ya Neno la Mungu yanaratibiwa na Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji Mpya. Lengo ni kuwahamasisha waamini kujenga na kudumisha utamaduni wa kupenda kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao mintarafu maisha na utume wa Kanisa.

Maandiko Matakatifu
24 January 2021, 15:29