2020.12.06 Sala ya Malaika wa Bwana 2020.12.06 Sala ya Malaika wa Bwana 

Papa Francisko:Uongofu ni kufungulia moyo katika huruma ya Mungu

Ni lazima kujifungulia mchakato wa safari ya uongofu wa moyo,ili kuondokana na maisha ya malimwengu,dhambi,utajiri ili kukutana na Mungu.Ndiyo njia aliyoshauri Papa Francisko wakati wa tafakari yake,kabla ya sala ya Malaika wa Bwana siku ya Dominika ya Pili ya kipindi cha Majilio aliyoongozwa na sura ya Mtakatifu Yohane Mbatizaji katika Injili ya Siku.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

Hali mbaya ya hewa haikuzuia waamini jariri kuwepo katika  Uwanja wa Mtakatifu Petro. Ndiyo maneno ya Papa Francisko ameisistiza wakati wa sala ya Malaika wa Bwana tarehe 6 Desemba 2020  akiwapongeza waamini na mahujaji waliofika kusali naye katika Dominika ya II ya Majlio. Tafakari ya Papa Francisko katika Dominika hii, umezungukia juu ya neno  Uongofu  hasa  wa kukataa dhambi na malimwengu pamoja na kuwa na uwezekano wa kweli wa kubadili maisha na kujifungulia uzuri, wema na upole wa Mungu. Uongofu ndiyo unasisitizwa sana katika kipindi cha Majilio, ikiwa ni mwaliko ambao unao onekana katika matukio ya Yohane Mbatizaji, mwanaume makini sana ambaye alikataa mambo yasiyofaa na kutafuta yale msingi, kama kiini cha Injili ya siku.

Papa Francisko amesema kwamba kwa kawaida uongofu unapelekea uchungu kwa sababu ya dhambi zilizotendeka hasa inapotokea kuwa na shauku ya kutaka kukombolewa nazo, kuwa na mapendekezo ya kutotenda dhambi tena na kubadilisha maisha binafsi. Ili kuweka pembeni dhambi hizo ni lazima kuzikataa  kwanza hata kila aina ya ashirio litokanalo na dhambi hizo. Viashiria hiviyo Papa Francisko amevitaja kuwa ni hisia za kiulimwengu, kupendelea raha na kupendelea utajiri.  Hiyo ni mantiki ya kwanza. Akiendelea Papa amebainisha wazi kwamba kuna mantiki ya  pili ambayo ni utafutaji wa Mungu na Ufalme wake.

Uongofu wa kweli kwa hakika unahitaji kuachana kabisa na matendo ya kutaka raha na hisia za ulimwengu huu, ili kuweza kufikia muungano kamili na Mungu na kuwa na urafiki naye. Safari hii  lakini pia siyo rahisi, Papa amebainisha kwa sababu yapo mahusiano mengi yanayotushikilia karibu na dhambi. Akifafanua mahusiano hayo amesema ni: “kutofautiana, kukata tamaa, uovu, mazingira mabaya na mifano mibaya”. Mara nyingi kuna msukumo dhaifu ambao unakufanya kuhisi kuelekea kwa Bwana lakini wakati huo utafikiria kama vile Mungu ananyamaza; utafikiri yuko mbali na kama vile ahadi zake za faraja,sio  za kweli,  kama vile picha ya mchungaji mwema ambayo inasisitizwa katika somo la Isaya.

Kwa kutoa mfano Papa ameuliza maswali. Ni mara ngapi tumesikia hisia ya kukata tamaa? “siwezi kabisa! Mimi ninaanza kidogo alafu ninarudi nyuma”, Papa ameongeza kusema, "hiyo ni mbaya! Kwa maana upo uwezekano. Kwa kushauri amesema “Unapohijiwa na hisia za kukata tamaa, usibaki katika hisia hizo, kwa sababu ni mchanga mwepesi, Papa amesisitiza. Ni mchanga mwepesi ambao upo na ugumu wake. Na ndiyo hiyo ugumu. Kama ilivyo katika vita kutafuta kimbilio na ndivyo katika maisha ya kila mmoja katika uongofu ni lazima kutafuta kimbilio katika sala kwa Mungu.

Uongofu ni neema  ya kuomba kwa nguvu”,Papa Francisko amesisitiza. “Tutaongoka kwa hakika kadiri ambavyo tutajifungulia uzuri, wema na huruma ya Mungu. Fikirieni huruma ya Mungu. Mungu sio baba mbaya: hapana. Yeye ni mpole, anatupenda sana, kama Mchungaji Mwema, ambaye hutafuta aliye wa mwisho wa kundi lake. Ni upendo, na uongofu ndiyo huu yaani  neema kutoka kwa Mungu. Wewe anza kutembea, kwa sababu ndiye anayekusogeza utembee, na utaona jinsi atakavyofika. Omba, tembea na kila wakati utapiga hatua mbele”. Kwa kuhitimisha Papa Francisko ameomba maombezi ya Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya Asili ili atusaidie kuondokana daima na dhambi,na malimwengu ili tujifungue kwa Mungu, katika Neno lake, katika upendo wake anaotupatia na kutukomboa.”

06 December 2020, 14:23