Maadhimisho ya Siku ya Mshikamano Kimataifa yasaidie kujenga umoja na upendo unaosimamiwa na kanuni ya auni katika medani mbalimbali za maisha. Maadhimisho ya Siku ya Mshikamano Kimataifa yasaidie kujenga umoja na upendo unaosimamiwa na kanuni ya auni katika medani mbalimbali za maisha. 

Papa Francisko: Siku ya Mshikamano wa Kimataifa: Huduma Makini!

Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mshikamano wa Kimataifa kwa Mwaka 2020 anasema, mshikamano ni fadhila inayomwilishwa kwa umakini mkubwa katika huduma zinazoweza kuwa katika mifumo mbalimbali, kama sehemu ya mchakato wa kuwatunza wengine. Huduma maana yake ni kitendo kinachoonesha kuwajali wengine hasa wanyonge.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mafundisho Jamii ya Kanisa yanabainisha kwamba, mshikamano unatoa mwanga kwa njia fulani iliyoungana kabisa na maumbile ya jamii ya binadamu, usawa wa wote katika kuheshimiana na haki na njia ya watu binafsi na binadamu wote kuelekea katika hali ya kujitoa katika umoja. Mshikamano unapaswa kumwilishwa katika sekta mbalimbali za maisha ya mwanadamu. Ikumbukwe kwamba, binadamu wote wanategemeana na kukamilishana katika hija ya maisha yao hapa duniani. Mshikamano ni kama kanuni ya jamii na fadhila ya maadili inayosaidia ukuaji wa kawaida wa binadamu. Mshikamano kadiri ya Mafundisho Jamii ya Kanisa unapaswa kuongozwa na kanuni auni.

Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mshikamano wa Kimataifa kwa Mwaka 2020 anasema, mshikamano ni fadhila inayomwilishwa kwa umakini mkubwa katika huduma zinazoweza kuwa katika mifumo mbalimbali, kama sehemu ya mchakato wa kuwatunza wengine. Huduma maana yake ni kitendo kinachoonesha kuwajali wengine hasa wanyonge katika familia, jamii na watu wa Mungu katika ujumla wake. Itakumbukwa kwamba, Siku ya Mshikamano wa Kimataifa ilianzishwa na Umoja wa Mataifa kunako mwaka 2005 na tangu wakati huo, inaadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 20 Desemba. Mshikamano unapaswa kuwa ni msingi wa mahusiano na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa. Huu ni mwaliko na changamoto kwa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kushikamana ili kupambana na matatizo pamoja na changamoto mbalimbali zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo.

Mshikamano unapaswa kuonesha katika mapambano dhidi ya ukosefu wa haki msingi za binadamu, utu na heshima yake; uharibifu wa mazingira nyumba ya wote pamoja na mapambano dhidi ya umaskini, baa la njaa na magonjwa duniani. Mshikamano ni nyenzo muhimu katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu kufikia mwaka 2030. Mshikamano wa kidugu ni nyenzo muhimu ya kupambana na pengo kubwa la maskini na matajiri duniani. Siku hii inaadhimishwa wakati ambapo kuna changamoto kubwa ya maambukizi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Bila mshikamano wa Kimataifa, watu wengi wataendelea kupoteza maisha kutokana na ukosefu wa rasilimali fedha, dawa na vifaa tiba. Bila mshikamano, chanjo dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19 itakuwa ni ndoto kwa nchi nyingi duniani!

Siku ya Mshikamano Kimataifa
20 December 2020, 15:16