Baba Mtakatifu Francisko tarehe 21 Desemba 2020 amekutana na kuzungumza na Makardinali pamoja na wafanyakazi wa Sekretarieti kuu ya Vatican ili kutakiana heri na baraka za Noeli kwa Mwaka 2020. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 21 Desemba 2020 amekutana na kuzungumza na Makardinali pamoja na wafanyakazi wa Sekretarieti kuu ya Vatican ili kutakiana heri na baraka za Noeli kwa Mwaka 2020. 

Hotuba ya Papa Francisko Kwa Makardinali na Curia Romana 2020

Baba Mtakatifu amegusia kuhusu: Fumbo la Umwilisho na Pasaka; Waraka wa Kitume "Fratelli tutti": Ametafakarisha kuhusu athari za ugonjwa wa COVID-19. Anabainisha na kutofautisha kati ya mgogoro na kinzani na hatimaye umuhimu wa kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha kwa njia ya wongofu wa ndani, sala na kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kuliongoza Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Jumatatu tarehe 21 Desemba 2020 amekutana na kuzungumza na Makardinali pamoja na Familia ya Sekretarieti kuu ya Vatican, kama sehemu ya mapokeo ya kutakiana heri na baraka za Sherehe za Noeli kwa mwaka 2020. Baba Mtakatifu katika hotuba yake pamoja na mambo mengine amegusia zaidi kuhusu: Fumbo la Umwilisho na Pasaka; kielelezo cha unyenyekevu wa Mungu kwa ajili ya huduma kwa binadamu. Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” ni Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayokita mizizi yake katika udugu na urafiki. Baba Mtakatifu ametafakarisha kuhusu athari za ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Anabainisha na kutofautisha kati ya mgogoro na kinzani na hivyo kuwa tayari kupokea changamoto zake ili kufahamu na hatimaye, kuweza kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha kwa njia ya wongofu wa ndani, sala na kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kuliongoza Kanisa. Kanisa liendelee kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu kwa kuendelea kulinda na kudumisha amani na utulivu wa ndani.

Baba Mtakatifu pamoja na waandamizi wake wote ni wahudumu wa Injili na zawadi ya Noeli, changamoto kubwa kwa wao ni kuomba zawadi ya unyenyekevu ili waweze kutekeleza huduma yao kwa watu wa Mungu. Lakini zaidi ya yote, wawe ni vyombo na mashuhuda wa furaha kwa watu wa Mataifa. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Fumbo la Umwilisho linawakumbusha wanadamu kwamba,  hata kama watakufa, lakini wanapaswa kuanza upya. Noeli ni Sherehe ya matumaini kwani hili ni tukio la Habari Njema ya Kuzaliwa kwa Mwana wa Mungu kati ya waja wake. Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu ni mahali muafaka pa majiundo ikiwa kama waamini wataweza kuishi bila kujihami kupita kiasi, kwa kujikita katika fadhila ya unyenyekevu na kuzingatia mambo msingi katika maisha. Programu ya maisha inayoshauriwa na Mtakatifu Paulo ni ile ambayo inajitahidi kufumbata uzima mpya katika Kristo Yesu kwa kuondokana na: uchungu, ghadhabu, hasira, kelele, matukano na kila ubaya.

Tena wajitahidi kufadhiliana wao kwa wao, huku wakiwa na huruma, watu wa kusamehe kama na Mungu katika Kristo Yesu alivyowasamehe. Wawe ni wapole na wanyenyekevu wa moyo kama alivyo Kristo Yesu, tayari kuwa wahudumu wa wote, kwa kujitahidi kuishi ufukara, kwa kujipatia mahitaji msingi. Sherehe za Noeli kwa Mwaka 2020 zimegubikwa na janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 ambalo limesababisha mgogoro mkubwa katika sekta ya afya, uchumi, jamii na hata kugusa na kutikisa, maisha ya Kanisa na ulimwengu katika ujumla wake. Mgogoro huu umekuwa ni jukwaa la majadiliano katika medani mbalimbali za maisha. Hiki ni kipindi cha majaribio, ili kuisaidia Jumuiya ya Kimataifa kushikamana zaidi. Hii inatokana na ukweli kwamba, janga hili limeanika udhaifu wa binadamu na kufichua mapungufu katika usalama ambao watu walijijengea kwa kujipangia ajenda, miradi, mazoea na vipaumbele vyao. Huu ni wakati wa kugundua tena: mizizi, asili na kumbukumbu ili kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu.

Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” unaopembua kuhusu udugu na urafiki wa kijamii unapata chimbuko lake kutoka katika Maandiko Matakatifu, Simulizi la Kuzaliwa kwa Mtoto Yesu na hivyo kujenga umoja na mafungamano ya kijamii kati ya Bikira Maria, Mtakatifu Yosefu, Wachungaji pamoja na Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali, ambao usiku wa manane walipokea Habari Njema ya Neno wa Mungu aliyefanyika Mwili! Hii ni fursa na mwaliko wa kutambua utu na heshima ya binadamu, ili kujenga mshikamano ili kusonga mbele kwa pamoja kama binadamu lakini kila mmoja kadiri ya imani na sauti yake! Wote watambue kwamba ni ndugu wamoja!

Baba Mtakatifu anasema, janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, ni fursa muafaka ya kuweza kutafakari maana ya changamoto hii mintarafu Maandiko Matakatifu kwa kuwatumia Mababa wa imani na Manabii, waliojipambanua katika kuandika Historia ya Wokovu. Hawa ni Abramu, Musa, Nabii Eliya, Yohane Mbatizaji na Paulo wa Tarso aliyelidhulumu Kanisa. Abramo alilazimika kuihama nchi yake, akaamriwa na Mungu kumtoa sadaka mwanaye wa pekee Isaka. Na kutoka kwake, wakazaliwa watu wapya. Changamoto hii ilimsaidia Abramu kukuza na kuimarisha imani yake. Musa alikuwa ni mtu asiyejiamini hata kidogo, daima alipenda kuweka matatizo yake mbele ya Mungu, lakini hatimaye, Mwenyezi Mungu akamteuwa kuwa ni mtumishi wake aliyeliongoza Taifa teule kutoka utumwani Misri.

Nabii Eliya alikuwa na nguvu kiasi cha kufananishwa na moto! Akapitia majaribu makubwa akitaka kuona mkono wa Mungu ukitenda maajabu, lakini hatimaye yake, akakutana na Mwenyezi Mungu katika sauti ndogo na yenye utulivu. Yohane Mbatizaji alipata changamoto kubwa kutambua Umasiha wa Kristo Yesu hapo awali. Lakini baada ya kufungwa na Kristo Yesu kuanza kutangaza Habari Njema ya Wokovu, hapo ndipo alipomgundua. Paulo wa Tarso aliyelidhulumu Kanisa, alikutana na Kristo Mfufuka akiwa njiani kwenda Dameski, akajiachilia mikononi mwa Mungu, na neema na hatimaye akawa ni Mtume na Mwalimu wa Mataifa. Hapa kila mwamini anaweza kujipatia mfano wake katika maisha.

Katika maisha na utume wa Yesu hadharani, Injili pacha zinamweka mbele ya waamini Roho Mtakatifu anayemwongoza Yesu katika maisha na utume wake kwa kufunga siku arobaini jangwani na huko anajaribiwa na Ibilisi, Shetani. Akiwa Bustanini Getsemani aliona huzuni nyingi kiasi cha kufa, akaogopa na kuhuzunika sana. Akiwa ametundikwa Msalabani, akajisikia kana kwamba, ameachwa na Baba yake wa mbinguni, lakini akaendelea kumwamini na hatimaye,  akajiaminisha kwa Baba yake wa mbinguni kwa kusema, “Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu” Lk. 23:46. Na huo ukawa ni mwanzo wa mchakato wa Fumbo la Ufufuko. Mama Kanisa naye katika maisha na utume wake, amepia historia iliyoandikwa kwa kashfa ya watoto wake, kiasi hata cha kujisikia kukosa matumaini, lakini Ufalme wa Mungu unaendelea kukua na kuchanua kwa njia ya ushuhuda wa maisha ya Kikristo. Alama za matumaini ndani ya Kanisa si habari inayopewa kipaumbele cha kwanza na vyombo vya mawasiliano ya jamii. Janga hili ni wakati muafaka wa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Injili, ili kuwajengea watu imani, matumaini na mapendo.

Baba Mtakatifu anachambua na kutofautisha kati mgogoro na kinzani. Mgogoro hauwezi kudharauliwa au kufichwa. Ni lazima kukabiliana nao. Katikati ya mgogoro, watu wanapoteza uwezo wao wa kutambua umoja wa kimsingi wa mambo yote yaliyo kweli. Kanisa likitumbukia katika mgogoro linapoteza dira na mwelekeo wake na matokeo yake hofu na mashaka vinatawala; Kanisa linakuwa na “shingo ngumu”, dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa inapungua; umoja na utofauti wa Kanisa, zawadi ya Roho Mtakatifu inapungua. Kwa neema ya Mungu, Kanisa linaweza kuondokana na kashfa hizi kwa kuiachia neema ya Mungu itende kazi ndani mwao; kwa njia ya ushuhuda, toba na wongofu wa ndani pamoja na kufisha utu wa kale. Waamini wanahimizwa kulipamba Kanisa kwa mavazi mapya. Udhaifu na mapungufu ya watoto wa Kanisa kisiwe ni kikwazo cha kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa kutambua kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya Wokovu, mahali pa kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu.

Hazina kubwa ya mageuzi ndani ya Kanisa ni Mapokeo ya Kanisa Katoliki. Ni fursa ya kumwachia Roho Mtakatifu ili aweze kutenda kazi ndani ya Kanisa, kwa kukazia dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa ili kujenga na kudumisha umoja. Huu ni muda wa kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kuendelea kujadiliana na Mwenyezi Mungu kwa njia ya sala inayosheheni matumaini. Wawe ni wahudumu wa Injili wenye amani na utulivu wa ndani na kamwe wasiruhusu huzuni kuwatala. Wafanyakazi wa Sekretarieti kuu ya Vatican wawe wafuasi wanyenyekevu wa Kristo Yesu kama walivyokuwa wale Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali. Familia ya Sekretarieti kuu ya Vatican ikiwa imeungana na Baba Mtakatifu ni wahudumu wa Injili na zawadi kubwa ya Noeli. Hii ni changamoto ya kuutambua uso wa Mwana wa Mungu kati ya maskini wanaokutana nao. Kamwe wasiwe ni vikwazo vya kazi ya Mungu, bali walijitahidi kumwomba Mungu ili awakirimie zawadi ya unyenyekevu katika huduma, ili Kristo Yesu azidi na wao kupungua!

Papa: Curia Romana
21 December 2020, 14:41