Papa Francisko asema, vazi la arusi ni alama ya upendo, huruma na neema ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake, mwaliko ni kutubu na kumwongokea Mungu! Papa Francisko asema, vazi la arusi ni alama ya upendo, huruma na neema ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake, mwaliko ni kutubu na kumwongokea Mungu! 

Papa Francisko: Vazi La Arusi ni Alama ya Upendo Na Neema!

Vazi la arusi ni alama ya upendo na huruma ya Mungu; yaani neema inayotolewa bure kwa watu wote!. Bila neema ya Mungu si rahisi sana kwa mwamini kupiga hatua mbele katika maisha yake ya kiroho. Kumbe, kuna haja ya kutubu na kumwongokea Mungu, ili kupokea huruma na upendo wa Mungu, yaani neema yake, inayopaswa kupokelewa kwa mshangao, furaha na shukrani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mwinjili Mathayo katika sura ya 22:1-14 anaweka mbele ya macho ya waamini karamu ya arusi ambayo Kristo Yesu anaifafanua  na kuielezea kwamba, ni sehemu ya mpango wa Mungu kwa ajili ya mwanadamu. Huyu ni Mfalme aliyemfanyia mwanawe arusi, kielelezo cha upendo na umoja kwa binadamu wote, kumzunguka Mwanae wa pekee. Mara mbili alijitahidi kuwatuma watumwa wake ili kwenda kuwaalika watu kuhudhuria arusini. Lakini kwa bahati mbaya sana, hawakupenda kushiriki katika arusi, kwa sababu walikuwa ni mipango mingine vichwani mwao, kiasi hata cha kutojali kabisa. Baadhi yao walikwenda shambani mwao na wengine walikuwa wanajishughulisha na biashara zao. Hivi ndivyo inavyotokea hata kwa waamini katika nyakati hizi, kwa kuweka mafao binafsi na mambo ya kidunia mbele ya mwaliko unaotolewa na Mwenyezi Mungu anayewaalika kushiriki katika sherehe ya arusi. Lakini, Mfalme hakukata tamaa na watu kutohudhuria Sherehe ya arusi ya Mwanae mpendwa. Kwani alitamani kuwapatia waalikwa amana, tunu na utajiri kutoka katika Ufalme wake. Ni katika muktadha huu, Mfalme akawaambia watumwa wake, kwenda njia panda za barabara, yaani mwisho wa mipaka ya mji, kuanza kuelekea mashambani, ili kuwaita wale wote wanaowaona njiani, bila ya kumbagua mtu awaye yote! Kwa sababu nyumbani mwa Mwenyezi Mungu hakuna anaye baguliwa!

Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 11 Oktoba 2020, Jumapili ya 28 ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa. Mfalme alitamani kuona kwamba, ukumbi wa karamu ya arusi ya Mwanawe mpendwa unajaa na kufurika watu, wale watu waliotengwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii; watu ambao walionekana kutostahili hata kidogo kushiriki kwenye karamu ya arusi ya Mwana wa Mfalme. Njiani wakawakusanya wote waliowaona, waovu kwa wema, arusi ikajaa wageni. Hivi ndivyo ilivyokuwa hata kwa Kristo Yesu aliyekuwa anakubali mwaliko wa chakula kutoka kwa watoza ushuru na wadhambi wa nyakati zake; watu waliokuwa wanabezwa kwa sababu hawakuwa wanastahili kushiriki katika karamu ya arusi ya Mwana mpendwa wa Mfalme. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Mwenyezi Mungu haogopi kugusa nyoyo za waja wake waliojeruhiwa kutokana na dhambi, kwa sababu anawapenda upeo na bado anawaalika kushiriki katika karamu ya arusi ya Mwanae mpendwa. Kanisa linaitwa na kutumwa kuwaendea wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele na mambo msingi ya kijamii; watu waliopondeka na kuvunjika moyo; watu ambao hawana tena matumaini.

Hii ni changamoto ya uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko; ushuhuda unaofumbwatwa katika Injili ya upendo usiokuwa na mipaka. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwafungulia maskini na wahitaji malango ya nyoyo na jumuiya zao, ili watu wote waweze kushiriki furaha, huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka kwa watu wote. Hawa ni wale watakatifu, wadhambi, wenye akili na wajinga. Lakini kwa wote wote hawa kuna sharti moja tu! Kila mtu anapaswa kuvaa vazi la arusi ambalo kila mshiriki alikuwa anapewa mara tu anapongia langoni. Arusi ilikuwa imejaa wageni. Lakini alipoingia Mfalme, ili kuwatazama wageni wake walioalikwa dakika za mwisho mwisho, akaona mle mtu mmoja asiyevaa vazi la arusi, naye akatekewa sana kwa sababu hakukubali kupokea lile vazi la arusi, akafungwa mikono na miguu akatupwa nje, huko ambako kuna kulia na kusaga meno.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, huyu ni mtu aliyejiamini kupita kiasi; akaona kwamba, anajitegemea kwa mambo yote na wala hakuwa na chembe hata kidogo ya kutaka kutubu na kumwongokea Mungu. Vazi la arusi ni alama ya upendo na huruma ya Mungu; yaani neema inayotolewa bure kwa watu wote bila ya ubaguzi! Bila neema ya Mungu si rahisi sana kwa mwamini kupiga hatua mbele katika maisha yake ya kiroho. Kumbe, kuna haja ya kutubu na kumwongokea Mungu, ili kupokea huruma na upendo wa Mungu, yaani neema yake, inayopaswa kupokelewa kwa mshangao, furaha na shukrani. Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kumwomba Bikira Maria ili awasaidie, kuiga mfano wa watumwa wa Mfalme mwenye arusi, ili waweze kutoka katika ubinafsi wao; waweze kuona vyema, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, ili watu wengi zaidi, waweze kushiriki katika karamu ya arusi, inayowapatia zawadi ya neema ya Mungu inayookoa!

Papa: Arusi
11 October 2020, 15:16