2020.10.28 Katekesi ya Papa 2020.10.28 Katekesi ya Papa 

Masikitiko ya Papa kufuatia na mauaji ya watoto wa shule nchini

Mara baada ya tafakari ya Katekesi ya Papa Francisko Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020,ameonesha masikitiko yake makubwa kufuatia na mauaji ya kinyama yaliyotokea Jumamosi tarehe 24 Oktoba 2020 huko Kumba nchini Kameruni.Jitihada zifanywe ili kuhakikisha usalama wa wote na haki ya kila kijana kwenda shule.Ametoa salam za rambi rambi kwa familia zao na kwa taifa zima.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Papa Francisko mara baada ya Katekesi yake Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020 kwa waamini na mahujaji waliofika katika ukumbi wa Papa Paolo VI mjini Vatican amesema "Ninaungana na familia katika uchungu kwa ajili ya vijana wanafunzi waliouwawa kinyama siku ya Jumamosi  iliyopita huko Kumba nchini Kamerun. Ninapata uchungu mkubwa kwa ajili ya tendo hilo la kikatili sana na la kinyama, ambalo limeondoa maisha ya wadogo wasio na hatia wakati wanajifunza shuleni".  Papa Francisko kwa uchungu huo akiendelea kutoa salamu zake za rambirambi kwa familia amesema kuwa, Bwana aweze kuwaangazia mioyo kwa sababu ishara ya namna hiyo isirudiwe tena na kwa sababu vita hivyo nchini Kamerun ziweze hatimaye kusitishwa na kupata amani. Ni matarajio ya Papa Francisko kuwa silaha ziweze kusitishwa ili kuhakikisha hatimaye usalama kwa wote na haki ya kila kijana kujifunza na kwa wakati ujao. Aidha ameonesha upendo wake kwa familia katika mji wa Kumba na Kamerun yote na kuwatakia faraja ambayo ni Mungu peke yake anaweza kuitoa.

Shukrani kwa Bwana kwa zawadi ya ubatizo

Papa Francisko aliendelea na salam katika lugha ya Kijerumani amesema ni kumshukuru Bwana kwa zawadi ya Ubatizo kwa njia ya yake sisi sote tumekuwa Wana wa Mungu na wajumbe wa mwili mmoja wa Kristo ambao ni Kanisa. Tunaishi na kushirikishana neema hii kwa furaha ya kiroho, na kubaki daima kwa kina katika mizizi ya upendo wa Ubaba wa Mungu. Aidha hata kwa upande wa wanaozungumza lugha ya Kipoland amekumbusha juu ya maadhimisho yaliyofanywa tarehe 22 Oktoba 2020 katika Liturujia ya Kumbu kumbu ya Mtakatifu Yohane Paulo II, katika mwaka huu ambao ni jubilei ya miaka yake 100 tangu kuzaliwa. Yeye daima alishauri kuwa na upendeleo kwa walio wa mwisho na wasio na mtetelezi na kulinda kila maisha ya binadamu, kuanzia kutungwa kwake hadi kifo chake cha kawaida, amesema Papa. Kwa njia ya maombezi ya Mama Maria Mtakatifu na Baba Mtakatifu wa Kipoland, “ Ninaomba Mungu aweze kutoa katika mioyo ya wote heshima kwa ajili ya maisha ya ndugu zetu hasa walio wadhaifu zaidi na kutoa nguvu kwa wale ambao wanawakaribisha na kuwatunza ,hata kama inawataka upendo wa kishujaa na Bwana na awabariki”.

Hakuna linalozuia kukua ndani ya upendo wa baba wa mbingu

Papa Francisko akiwalekea wa lugha  ya kireno, amesema hakuna lolote linaweza kuzuia kuishi na kukua katika upendo wa Baba wa Mbingu na kutoa ushuhuda  kwa wote juu ya wema wake na huruma yake. Juu yao na familia yao amewabariki! Hatimaye katika lugha ya kitaaliano amesema “ Kanisa linaadhimisha Sikukuu ya Mtakatifu  Simoni na Yuda Taddei. Amewashauri kufuata mifano yao na kuweka daima katikati Kristo katika maisha yao na kuwa mashuhuda wa kweli wa Injili katika jamii yetu. Mawazo yake pia kama kawaida ni kwa ajili ya wazee, vijana, wagonjwa na wanandoa wapya. Amewatakia kila mmoja kukua kila siku katika kutafakari wema na huruma ambao unaangaza kutoka kwa mtu Yesu.

Sala ya Mtakatifu Yuda Taddei

“Mtakatifu Yuda Tadei,/ Mtume Mtakatifu,/ mtumishi mwaminifu na rafiki wa Yesu./ Jina la yule msaliti aliyemwuza Yesu/ limewafanya wengi wakusahau./ Walakini Kanisa zima linakuheshimu/ na kukuomba kama Msaidizi katika mashaka makubwa,/ na katika mambo yasiyo na matumaini tena./Uniombee mimi mnyonge./ Ninaomba utumie uwezo ule uliojaliwa/ wa kuleta upesi msaada kwa watu walioukosa./ Unisaidie sasa katika mahitaji yangu,/ ili nipate kitulizo na msaada wa mbinguni/ katika lazima zangu,/ masumbuko na mateso,/ hasa/ (taja shida yako)./ Pia ili niweze kumsifu Mungu nawe na wateule wote milele./ Mtakatifu Yuda Tadei,/ utuombee,/ na uwaombee watu wote wanaokuheshimu na kukuomba msaada./ Moyo Mtakatifu wa Yesu,/ Rafiki mpenzi wa Yuda Tadei,/ nakutumainia./

 

28 October 2020, 14:15