Baba Mtakatifu Francisko ametuma ujumbe kwa njia ya video kwa mahuaji kwenye madhabahu ya Bikira Maria wa Lujan kwa mwaka 2020. Baba Mtakatifu Francisko ametuma ujumbe kwa njia ya video kwa mahuaji kwenye madhabahu ya Bikira Maria wa Lujan kwa mwaka 2020. 

Ujumbe wa Papa Francisko Kwa Mahujaji wa B. Maria wa Lujan!

Papa Francisko amesema, kuna wakati ambapo hija ya maisha ya kiroho inakuwa ngumu sana. Kipindi hiki, kuna hatari ya maambukizi makubwa ya Virusi vya Corona, hali ambapo inaendelea kusababisha hofu kubwa miongoni mwa watu wa Mungu. Janga hili limeibua changamoto mbalimbali ambazo hazina budi kufanyiwa kazi kwa umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Familia ya Mungu nchini Argentina kuanzia tarehe 23-26 Septemba 2020 imefanya hija ya 40 kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Luján “Nuestra Señora de Luján" kwa njia ya mitandao ya kijamii kutokana na hofu ya maambukizi makubwa ya janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Haya ni Madhabahu ambayo Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Askofu aliyatembelea mara kwa mara na kutoa Sakramenti ya Kitubio kwa waamini waliokuwa wamejiandaa vyema. Ni madhabahu ambayo yameacha chapa ya kudumu katika akili na moyo wake. Hija hii, imehitimishwa rasmi, Jumapili tarehe 27 Septemba 2020 kwa Ibada ya Misa Takatifu, kama sehemu ya kumbukumbu ya Jubilei ya Miaka 100 ya Ukanda wa Neuqunèn. Ibada hii ya Misa Takatifu imeongozwa na Askofu Fernando Croxatto wa Jimbo Katoliki la Neuquèn.

Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa njia ya video amesema kwamba, kuna wakati ambapo hija ya maisha ya kiroho inakuwa ngumu sana. Kipindi hiki, kuna hatari ya maambukizi makubwa ya Virusi vya Corona, COVID-19, hali ambapo inaendelea kusababisha hofu na wasi wasi mkubwa miongoni mwa watu wa Mungu. Janga hili limeibua changamoto mbalimbali ambazo hazina budi kufanyiwa kazi kwa umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria ili aweze kuwakumbatia. Kauli mbiu ya hija hii ni “Mama tukumbatie, tunahitaji bado kutembea”.

Baba Mtakatifu amewashirikisha mahujaji walioshiriki katika hija hii, baadhi ya shuhuda kutoka kwa waamini wenzao, kwa kusema kwamba, dhamana na utume wa wanawake ni kuwapokea na kuwakusanya watoto wake. Kumbe, anapoumia mmoja kati ya watoto wake, anaumia hata yeye pia. Watoto wote wanatofautiana lakini wote ni sawa mbele ya mama yao. Hivi ndivyo ilivyo hata kwa waamini, ambao kimsingi wako tofauti sana lakini wote wanakumbatiwa bila ubaguzi na Bikira Maria wa Luján “Nuestra Señora de Luján.” Baba Mtakatifu amewasindikiza na kuungana pamoja nao kwa njia ya sala na kuwaomba pia kuendelea kumkumbuka kwa njia ya sala katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Papa Argentina

 

29 September 2020, 15:38