Tarehe 29 Septemba, Mama Kanisa anawakumbuka na kuwaenzi watakatifu Malaika wakuu: Mikaeli, Gabrieli na Rafaeli. Tarehe 29 Septemba, Mama Kanisa anawakumbuka na kuwaenzi watakatifu Malaika wakuu: Mikaeli, Gabrieli na Rafaeli. 

Sikukuu Ya Watakatifu Malaika Wakuu: Mikaeli, Gabrieli na Rafaeli

Papa Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, anamwomba Malaika mkuu Mikaeli awasaidie waamini katika mapambano ya kazi ya ukombozi. Malaika Mkuu Gabrieli, awaletee watu wa Mungu Habari Njema ya Wokovu, Kristo Yesu, aliyemkomboa mwanadamu, awakirimie matumaini. Malaika Mkuu Rafaeli, awasindikize katika safari yao ya uponyaji!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 29 Septemba anawakumbuka na kuwaenzi Watakatifu Malaika wakuu: Mikaeli, Gabrieli na Rafaeli ambao wametajwa kwa namna ya pekee kabisa katika Maandiko Matakatifu na kila mmoja akitajwa kwa kazi maalum anayoifanya mbele ya Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, anamwomba Malaika mkuu Mikaeli awasaidie waamini katika mapambano ya kazi ya ukombozi. Malaika Mkuu Gabrieli, awaletee watu wa Mungu Habari Njema ya Wokovu, Kristo Yesu, aliyemkomboa mwanadamu, awakirimie matumaini. Malaika Mkuu Rafaeli, awashike mkono na kuwasindikiza katika safari yao ya uponyaji! Mikaeli maana yake “Ni nani aliye sawa na Mungu? Huyu ni Malaika mkuu aliyepambana fika na Ibilisi, Shetani na kushinda, kiasi kwamba, yule nyoka mkubwa, aitwaye Shetani, Ibilisi audanganyaye ulimwengu wote, akatupwa hata katika nchi kama tunavyosoma kwenye Maandiko Matakatifu. Rej. Uf. 12:7. Malaika mkuu Rafaeli ni mlinzi wa watu wa Mungu kwa sababu yeye ni Jemedari mkuu. Rej. Dan. 12: 1.

Gabrieli maana yake ni nguvu ya Mungu. Huyu ni kati ya Malaika wakuu saba wanaokaa siku zote mbele ya Mwenyezi Mungu kama alivyosema Malaika Gabrieli alipokuwa anajibizana na Zakaria kwa kumkumbusha kwamba, yeye alikuwa ni Gabrieli anayesimama mbele ya Mungu na ametumwa kumpasha Habari Njema ya kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji. Malaika mkuu Gabrieli ndiye aliyetumwa na Mungu kwenda mpaka mji wa Galilaya, jina lake Nazareti kwa Bikira Maria, ili kumpasha Habari Njema kwamba, atakuwa ni Mama wa Mungu. Kwa maneno machache, Malaika wakuu ndio wanaowafunulia watu siri za Mwenyezi Mungu. Rej. Lk. 1-19; Lk. 1:26-28.

Rafaeli maana yake ni dawa ya Mungu inayoponya. Rafaeli ni kati ya Malaika watakatifu saba wanaopeleka sala za watakatifu, na kuingia mbele za utukufu wake aliye Mtakatifu. Mwenyezi Mungu ndiye anayepaswa kupewa heshima, utukufu na sifa. Re. Tob. 12:15 na Ufu. 8:2. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanasema katika liturujia ya hapa duniani, waamini wanashiriki, wakionja liturujia ya mbinguni, iadhimishwayo katika Mji Mtakatifu Yerusalemu, wanaouelekea kama wasafari, ambako Kristo Yesu ameketi mkono wa kuume wa Mwenyezi Mungu kama mhudumu wa patakatifu na wa ile hema ya kweli. Waamini wanaungana na wapiganaji wa jeshi la mbinguni kumwimbia Mwenyezi Mungu wimbo wa utukufu. Wakiwakumbuka kwa heshima watakatifu, wanatumaini kupata ushirika nao, wanangojea kwa shauku Mkombozi, Kristo Yesu, mpaka atakapojidhihirisha, Yeye ambaye ni uzima wao, ndipo nao watakapodhihirishwa pamoja naye katika utukufu. Rej. SC. 8.

Malaika Wakuu
29 September 2020, 16:23