Jumuiya ya Kimataifa tarehe 21 Septemba 2020 inaadhimisha Siku ya Amani Duniani, inayoongozwa na kauli mbiu "Kujenga Amani kwa Pamoja" Siku ya upendo, huruma, wema na matumaini. Jumuiya ya Kimataifa tarehe 21 Septemba 2020 inaadhimisha Siku ya Amani Duniani, inayoongozwa na kauli mbiu "Kujenga Amani kwa Pamoja" Siku ya upendo, huruma, wema na matumaini. 

Ujumbe wa Papa Francisko Kwa Siku ya Amani Duniani, Sept. 2020

Maadhimisho ya Siku ya Amani Duniani kwa mwaka 2020 yanaongozwa na kauli mbiu “Kujenga Amani Kwa Pamoja”. Ni muda wa kusambaza: huruma, upendo, wema na matumaini” kwa watu walioathirika sana na janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona. Ni wajibu wa Jumuiya ya Kimataifa kuondokana na ubaguzi, chuki na uhasama kati ya watu wa Mataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Amani ni msingi wa wema, heshima na maendeleo fungamani ya binadamu; ni paji na zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomshirikisha na kumwajibisha binadamu. Amani ni tunda la upendo linalopaswa kuboreshwa kwa njia ya malezi ya dhamiri nyofu; ukweli na uhuru; usalama wa raia na mali zao; kwa kulinda na kuheshimu utu wa binadamu, ustawi na maendeleo ya wengi. Kwa ufupi, amani ni kazi ya haki na matunda ya upendo! Amani duniani inatishiwa sana na mashindano ya silaha, utengenezaji pamoja na mchakato wa ulimbikizaji wa silaha duniani! Ni wajibu wa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha amani duniani! Vita ni chanzo kikuu cha maafa, mateso na mahangaiko ya binadamu! Kila mwaka ifikapo tarehe 21 Septemba, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Amani Duniani, iliyoanzishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kunako tarehe 30 Novemba 1981 na kunako mwaka 2001, Umoja wa Mataifa ukapanga tarehe 21 Septemba kuwa ni siku ya kusitisha pia vita, chuki na uhasama. Lengo ni kuimarisha dhana ya amani duniani na kati ya wanachama wa Jumuiya ya Kimataifa.

Huu ni muda muafaka wa kuondokana na chuki, uhasama, kinzani pamoja na mambo yote yale yanayosababisha vita duniani. Ni muda wa kusitisha vita, chuki na uhasama kwa siku nzima, ili hatimaye, huu uwe ni utamaduni wa Jumuiya ya Kimataifa. Vijana wa kizazi kipya wanapaswa kuelimishwa kuhusu umuhimu wa kulinda, kutunza na kudumisha amani duniani. Maadhimisho ya Siku ya Amani Duniani ambayo kwa mwaka 2020 yanaongozwa na kauli mbiu “Kujenga Amani Kwa Pamoja”. Hii ni siku ya kusambaza “Virusi vya huruma, upendo, wema na matumaini” kwa watu walioathirika sana na janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona. COVID-19. Ni wajibu wa Jumuiya ya Kimataifa kuondokana na kishawishi cha kutaka kutumia janga la Corona, COVID-19 kusababisha ubaguzi, chuki na uhasama kati ya watu wa Mataifa. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii kama sehemu ya maadhimisho ya siku hii anasema, safari ya upatanisho inahitaji uvumilivu na imani. Amani ya kweli haiwezi kupatikana, ikiwa kama hakuna anayeitumainia.

Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii, kuwahamasisha watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu, kwa kutambua kwamba, wote ni watoto wa Mungu, wanaotamani amani ya kweli, inayopata chimbuko lake kutoka katika undani wa moyo wa mwanadamu. Kamwe watu wa Mungu wasikate wala kukatishwa tamaa kutafuta na kudumisha amani duniani. Vita ni majanga yasiyokuwa na mashiko, kuna umuhimu wa kuzingatia kanuni maadili na sera makini za kisiasa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Huu ni wajibu wa Jumuiya ya Kimataifa kujizatiti katika ujenzi wa amani dumifu, inayofumbatwa katika ukweli, haki, upendo na uhuru kamili. Wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa hawana budi kusitisha mapigano na kuanza kujikita katika nguvu ya kimaadili; dhana ambayo inajikita katika ushuhuda wa kinabii. Badala ya kuwekeza katika utengenezaji na ulimbikizaji wa silaha duniani, rasilimali hii ingeweza kuwekezwa zaidi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi

Mtakatifu Yohane XXIII katika Waraka wake wa Kitume “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani”, aliouandika kunako mwaka 1963: akikazia kwa namna ya pekee kabisa: ukweli, haki, upendo na uhuru. Tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, Kanisa limeendelea kuandika na kushuhudia Injili ya amani inayofumbatwa kwa namna ya pekee kabisa katika tunu msingi za Kiinjili yaaani: haki, upendo, utu na heshima ya binadamu. Hii ni misingi inayopambana na vitendo vyote vya kigaidi, vita na machafuko ya aina mbali mbali ambayo kimsingi ni kashfa kubwa kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Utunzaji wa amani duniani ni dhamana inayopaswa kutekelezwa na kumwilishwa katika maisha ya kila siku. Nguvu ya amani, itawale zaidi kuliko silaha zinazosababisha maafa kwa watu na mali zao; nguvu ya majadiliano katika ukweli na uwazi, ipewe kipaumbele cha kwanza, kuliko kupimana nguvu kwani katika vita hakuna mtu anayeweza kujigamba kwamba, ameshinda! Nguvu ya kimaadili ipewe nafasi ya kwanza badala ya utawala wa mabavu! Hiki ni kipindi muafaka cha kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha amani duniani, kwa ujasiri na ushupavu; kwa kukazia umuhimu wa amani kama kikolezo kikuu cha maendeleo fungamani ya binadamu, ili kuondokana na vita inayosababisha maafa na mateso makali kwa watu wasiokuwa na hatia.

Amani Duniani 2020
21 September 2020, 16:23