Vatican News
Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza madaktari, wauguzi, wafanyakazi katika sekta ya afya pamoja na watu wa kujitolea katika mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza madaktari, wauguzi, wafanyakazi katika sekta ya afya pamoja na watu wa kujitolea katika mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19.  (©angellodeco - stock.adobe.com)

Papa Francisko: Mshikamano wa Upendo Dhidi ya COVID-19

Papa Francisko anawashukuru wadau katika sekta ya afya, vyama vya kitume na watu wanaojitolea katika kupambana na janga la Virusi vya Corona, COVID-19. Kuna mambo mengi yanayoweza kuwakamata na kuwashtua watu, lakini zaidi wakumbuke kwamba, Mungu ndiye Bwana wa maisha, anawapenda watu wake upeo na zaidi ya yote, yeye yuko ulimwenguni kati ya viumbe vyake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya katekesi yake kuhusu “Uponyaji wa Ulimwengu”, Jumatano tarehe 16 Septemba 2020, kwenye Uwanja wa Jengo la Mtakatifu Damas lililoko mjini Vatican, kwa mara nyingine tena, amewashukuru na kuwapongeza madaktari, wauguzi na wafanyakazi katika sekta ya afya. Amevishukuru vyama vya kitume na watu wanaojitolea katika kupambana na janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Kuna mambo mengi yanayoweza kuwakamata na kuwashtua watu, lakini zaidi wakumbuke kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye Bwana wa maisha, anawapenda watu wake upeo na zaidi ya yote, yeye yuko ulimwenguni kati ya viumbe vyake. Mwenyezi Mungu kamwe hawezi kuwaacha watu wake katika upweke, kwa sababu amejishikamanisha sana na waja wake na upendo wake wa daima, unawawezesha kupata njia mpya. Kumbe, Mwenyezi Mungu anapaswa kutukuzwa milele! Waamini wanakumbushwa kwamba, Roho Mtakatifu ni chemchemi ya wema wote, awasaidie waamini kutafakari kuhusu hali tete ya maisha ya mwanadamu, ili hatimaye, Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, aweze kuwalinda na kila ubaya!

Waamini wajitahidi kumwomba Mwenyezi Mungu ili awakirimie neema na baraka ya kuweza kutafakari matendo makuu ya Mungu yanayojidhihirisha katika kazi ya uumbaji, ili hatimaye, waweze kukuza na kudumisha wajibu wa mtu binafsi na ule wa kijumuiya, ili kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Mtakatifu Yohane Paulo II aliwahi kusema kwamba, alikuwa anautafakari uzuri wa dunia hii, kiasi cha kuonekana kuwa, alikuwa anazungumza kwa lugha yenye nguvu mintarafu anga angavu iliyopambwa kwa rangi ya bluu. Alikuwa anaona misitu ya kijani kibichi, mashamba yaliyokuwa yanapendeza kuangaliwa kwa macho; kazi ya mikono ya Mwenyezi Mungu iliyokuwa inategemeza maziwa na mito ya maji, wote huu ukiwa ni ushuhuda wa upendo wa Mungu, Muumbaji anayevitegemeza vyote hivi kwa nguvu ya Roho Mtakatifu na kwa kazi ya ukombozi iliyotekelezwa na Kristo Yesu kwa ajili ya binadamu na viumbe vyote. Mtindo huu wa maisha anasema Baba Mtakatifu Francisko, unaoonesha mahusiano na mafungamano kati ya binadamu na kazi ya uumbaji uwe ni msingi wa dhamana kwa ajili ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Hatimaye, Baba Mtakatifu amesema kwamba, katika nyakati hizi, anapenda kuyaelekeza mawazo yake kwa namna ya pekee kabisa kwa wazee, wagonjwa pamoja na wale wote wanaowahudumia kwa moyo wa furaha, ukarimu na majitoleo makubwa. Anawaombea wote, kila jema kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kuwataka kuwa ni wasambazaji wa ujumbe wa Injili ya upendo wa Mungu kwa watu wa Mataifa. Amewakumbuka na kuwaombea pia vijana pamoja na wanandoa wapya, ili waendelee kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya familia inayofumbatwa katika Injili ya uhai. Baba Mtakatifu Francisko amesema kwamba, tarehe 14 Septemba 2020, Mama Kanisa ameadhimisha Sikukuu ya Kutukuka kwa Msalaba. Kumbe, Msalaba ni chombo cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu! Ni kielelezo cha imani kwa Kristo Yesu. Ni ishara ya neema, sala, msamaha, upatanisho na matumaini. Ni kutokana na maana hii mpya, Mama Kanisa anaona fahari kuu kuimba sifa kuu za Msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Msalaba unaendelea kumfunza mwamini kwamba, hakuna mapendo kamili yasiyokuwa na mateso na matumaini ya maisha na uzima wa milele.

Papa: Mshikamano
16 September 2020, 15:00