Vatican News
Tanzia: Kardinali  Adrianus Johannes Simonis amefariki dunia tarehe 2 Septemba 2020 akiwa na umri wa miaka 88 ya kuzaliwa. Tanzia: Kardinali  Adrianus Johannes Simonis amefariki dunia tarehe 2 Septemba 2020 akiwa na umri wa miaka 88 ya kuzaliwa. 

Tanzia: Kardinali Adrianus J. Simonis Amefariki Dunia 2 Sept.

Kardinali Adrianus Johannes Simonis alizaliwa tarehe 26 Novemba 1931 huko Lisse. Tarehe 15 Juni 1957 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tarehe 29 Desemba 1970, Mtakatifu Paulo VI akamteuwa kuwa Askofu na kuwekwa wakfu tarehe 20 Machi 1971. Tarehe 27 Juni 1983, Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa ni Askofu mkuu mwandamizi mwenye haki ya kurithi Jimbo kuu Utrecht.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Kardinali Adrianus Johannes Simonis, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Utrecht  kilichotokea tarehe 2 Septemba 2020 huko Utrecht nchini Uholanzi, akiwa na umri wa miaka 88 ya kuzaliwa. Baba Mtakatifu amemtumia salam za rambirambi Kardinali Willem Jacobus Eijk, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la  Utrecht kufuatia kifo cha Kardinali Adrianus Johannes Simonis, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Utrecht. Katika salam zake za rambirambi, Baba Mtakatifu anaiombea roho ya Marehemu Kardinali Adrianus Johannes Simonis, ili iweze kupata huruma kutoka kwa Kristo Yesu, Mchungaji mwema na hatimaye, iweze kupumzika katika usingizi wa amani. Baba Mtakatifu anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa ushuhuda na uaminifu aliouonesha Marehemu Kardinali Adrianus Johannes Simonis katika miaka yake yote kama Askofu kwa Majimbo ya Rotterdam na Utrecht, bila kusahau mchango wake mkubwa katika mchakato wa kujenga na kudumisha umoja wa Kikanisa.

Mwishoni wa salam zake za rambirambi, Baba Mtakatifu anapenda kutoa baraka za kitume kwa wale wote walioguswa na kutikiswa na msiba huu mzito wa Kardinali Adrianus Johannes Simonis, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Utrecht. Itakumbukwa kwamba, Marehemu Kardinali Adrianus Johannes Simonis alizaliwa tarehe 26 Novemba 1931 huko Lisse, Jimbo Katoliki la  Rotterdam, nchini Uholanzi. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 15 Juni 1957 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Kati ya mwaka 1959 hadi mwaka 1966 alitumwa mjini Roma ili kujiendeleza katika Sayansi ya Maandiko Matakatifu na kufanikiwa kutunukiwa Shahada ya Uzamivu katika Maandiko Matakatifu. Tarehe 29 Desemba 1970, Mtakatifu Paulo VI akamteuwa kuwa Askofu na kuwekwa wakfu tarehe 20 Machi 1971, akiwa anaongozwa na kauli mbiu yake ya Kiaskofu “Ut dongoscant Te” yaani “Wakujue wewe” chemchemi ya maisha na uzima wa milele. Tarehe 27 Juni 1983, Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa ni Askofu mkuu mwandamizi mwenye haki ya kurithi Jimbo kuu Utrecht.

Na ilipogota tarehe 8 Desemba 1983 katika maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, akasimikwa rasmi na kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Utrecht. Tangu wakati huo, amekuwa ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uholanzi. Ni kiongozi aliyejipambanua sana katika masuala ya kufundisha, elimu na umuhimu wa dini shuleni. Kardinali Adrianus Johannes Simonis aliwahi kuteuliwa kuwa ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Nijmegen. Kwa hakika ni kiongozi shupavu, aliyesimama kidete kutangaza na kushuhudia umuhimu wa Mafundisho tanzu ya Kanisa kuhusu tunu msingi za maisha ya ndoa, familia sanjari na Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Mtakatifu Yohane Paulo II alimteuwa kuwa Kardinali tarehe 24 Mei 1985 . Na tarehe 14 Aprili 2007, akang’atuka kutoka madarakani. Kwa kifo cha Kardinali Adrianus Johannes Simonis, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Utrecht, sasa Baraza la Makardinali lina jumla ya Makardinali 220 kati yao wenye haki ya kupiga na kupigiwa kura wakati wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro ni 122 na wengine hawa 98 hawana tena haki ya kupiga wala kupigiwa kura.

Tanzia: Kard. Simonis
04 September 2020, 15:33