Kanisa Katoliki nchini Tanzania, Jumapili tarehe 2 Agosti 2020 linaadhimisha Siku ya Upashanaji Habari Ulimwenguni kwa kuongozwa na Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Siku ya 54 ya Upashanaji Habari. Kanisa Katoliki nchini Tanzania, Jumapili tarehe 2 Agosti 2020 linaadhimisha Siku ya Upashanaji Habari Ulimwenguni kwa kuongozwa na Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Siku ya 54 ya Upashanaji Habari. 

Ujumbe wa Papa Francisko Siku ya Mawasiliano Tanzania: 2020

Ujumbe wa Papa Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 54 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni iliyoadhimishwa na Mama Kanisa tarehe 24 Mei 2020 sanjari na Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni. Kauli mbiu “Nawe upate kusema masikioni mwa wanao, na masikioni mwa mjukuu wako” Sehemu ya Maandiko Matakatifu kutoka Kitabu cha Kutoka:10:2. Maisha yanakuwa ni historia. BIBLIA!

Na Shemasi Karoli Joseph AMANI, - Tabora, TANZANIA.

Jumapili ya kwanza ya Mwezi Agosti, yaani tarehe 2 Agosti 2020, Kanisa Katoliki nchini Tanzania linaadhimisha Siku ya Upashanaji Habari Ulimwenguni. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 54 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni iliyoadhimishwa na Mama Kanisa tarehe 24 Mei 2020 sanjari na Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni, ulipambwa kwa kauli mbiu “Nawe upate kusema masikioni mwa wanao, na masikioni mwa mjukuu wako” Sehemu ya Maandiko Matakatifu kutoka katika Kitabu cha Kutoka:10:2. Maisha yanakuwa ni historia. Mawasiliano ni tunu faradhi katika mchakato mzima wa utangazaji na usambazaji wa Neno la Mungu kwa watu ulimwenguni. Taifa la Mungu linapata Ujumbe wa Habari Njema ya wokovu kupitia vyombo mbalimbali vya mawasiliano hususan radio, televisheni, na hata mitandao ya kijamii.  Mitandao ya kijamii kama whatsapp, facebook, instragram, Youtube na Twitter ni maeneo pendwa hivi leo ambako watu hutumia muda mwingi kuperuzi habari, na hivi Habari Njema au Injili ya wokovu haiwezi kubaki nyuma. Mama Kanisa “halazi damu” kulilisha taifa la Mungu Neno la uzima kupitia uwanja huo madhubuti wa mitandao ya kijamii.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya Hamsini na Nne (54) ya Upashanaji Habari Ulimwenguni anakita mawazo yake katika dhana simulizi. Kauli mbiu ya Siku hii ni ''Nawe upate kuwasimulia wanao na wajuu wako'' (Kut. 10:2). Katika tafakari yake Baba Mtakatifu analiasa taifa la Mungu kuonja thamani ya usambazaji wa Imani na Neno la Mungu kupitia mbinu rahisi ya kusimuliana hususan katika familia ambako walio wadogo wanaweza kurithishwa hazina ya imani kupitia midomo ya wazazi na walezi wao. Baba Mtakatifu anasisitiza kwamba, mwanadamu kwa asili yake ni kiumbe kinachofumbatwa na hadithi. Maisha ya mwanadamu katika ujumla wake tayari ni hadithi iliyoandikwa na Mwenyezi Mungu kupitia maisha ya mtu huyo. Katika maisha mtu hukutana na changamoto kadha wa kadha lakini pia huimarishwa na upendo ambao humuwezesha kukabiliana nazo na mwisho kuibuka mshindi kama ilivyo katika hadithi nyingi katika filamu, sinema na vitabu. Aidha, hadithi ya mwanadamu inaweza kukumbwa na hatari ya kuharibiwa au kuchafuliwa na waovu wasiopenda wenzao kuwa na hadithi za kupendeza. Kumbe yapasa kulinda na kuheshimu hadithi ya kila mtu.

Hata hivyo Baba Mtakatifu anangalisha kwamba si kila hadithi ni nzuri. Hadithi nyingine zimejaa ndani yake chembechembe za chuki, rapsha, uzandiki na uchochezi, ambao lengo lake ni kuzua purukushani na tafrani katika maisha ya watu. Hali hii hupelekea watu kushindwa kuishi kwa amani, maelewano mazuri na utulivu katika familia zao na jamii kwa ujumla. Zipo hadithi ambazo chimbuko lake ni majungu na maudhui yake ni takilifu (hayana upendo). Hizi hulenga kuvuruga maisha ya watu na kuongeza adha, kashfa na karaha kwa watu. Mfano hai ni hadithi ile ya Kitabu cha Mwanzo 3:4, ''….Mkiwa mtafanana na Mungu''. Baba Mtakatifu anaangalisha akisema kwamba mara nyingi tunaweza kukuta katika vyombo vya habari hadithi ambazo badala ya kuzijenga jamii zetu, zinapotosha na kuleta uhasama. Hata hivyo hadithi hizi au stori za kutungwa licha ya umaarufu wake wa ghafla, hizo huishi muda mchache kabisa. Histori na hadithi za kweli ndizo huishi muda mrefu, hudumu karne kwani hizo hukuza uhai wa jamii.

Baba Mtakatifu amekazia kusema Maandiko Matakatifu ndiyo mama wa hadithi zote. Mtiririko wa utitiri wa watu, matukio na habari chungu mzima katika Biblia ni ushahidi tosha kwamba Mungu ndiye mwumbaji na vilevile msimuliaji mahiri. Kwa kutumia Neno tu aliita na kutaja vitu navyo vikawa. Baba Mtakatifu anakazia kusema kwamba katika Neno la Mungu tunaona jinsi ambavyo Mungu anaingilia kati kumwokoa mwanadamu katika madhila yake mbalimbali. Mungu ni Mungu anayesikiliza na kusikia na hivi kuwakumbuka watu wake tangu mwanzo. Katika kumbukumbu ya Mungu ipo chemichemi ya ukombozi wa mwanadamu ambao unaonekana kupitia ishara kadha wa kadha katika Biblia, hususan katika Kitabu cha Kutoka. Yesu mwenyewe alifundisha habari za Mungu na ufalme wake akitumia mifano na masimulizi kupitia mifano ya maisha ya kawaida ya watu. Kama haitoshi, Injili zenyewe ni zimeandikwa katika mfumo wa masimulizi ambayo wakati zikitusimulia habari za Yesu hutushirikisha pia wokovu wake na kutuunganisha na Kristo Mwokozi. Katika injili, Neno wa Mungu ndiye hadithi na msimuliaji mwenyewe; ''Mwana wa pekee aliye sawa na Baba, ndiye aliyetujulisha habari za Mungu'' (Yohane 1:18). Katika masimulizi anajifunua na kujiweka wazi kuweza kutambulika kwa aliye mbele yake.

Katika historia ya kila binadamu imo historia ya Mungu. Mungu anaingia katika hadithi ya kila mtu ulimwenguni kwani ukombozi wake ni kwa watu wote. Historia ya Kristo Yesu si habari iliyopitwa na wakati bali inayo mashiko kwa zama zote bila kuruka hata moja. Nayo kwa kuwa hugusa karne zote, ndiyo huzifanya historia za wanadamu kufunikwa na historia ya Mungu. Kumbe historia ya kila mwanadamu, kwa namna moja ama nyingine ni historia ya Mungu. Mt. Paulo anawaambia wakristo wa Korinto kwamba wao ni ''barua ya Kristo....Barua yenyewe imeandikwa si kwa wino, bali kwa Roho wa Mungu aliye hai, imeandikwa si juu ya kipande cha jiwe, bali juu ya mioyo ya watu''. (2Wakorinto 3:3). Roho Mtakatifu huandika mioyoni mwa watu, na anapoandika hutukumbusha wema na ukuu wa Mungu. Neno kumbuka kwa lugha ya Kiitalia ni “ri-cordare” humaanisha kupeleka jambo na kulizamisha moyoni. Kumbe, kila historia, kila hadithi ya maisha ya mtu inayo nafasi ya kukumbukwa katika Moyo wa Mungu haijalishi inatisha kiasi gani au inayo mabaya kiasi gani. Mungu ndiye aifanyayo kuwa mashuhuri kadiri ya mapenzi yake. Amefanya hivyo kwa Mtakatifu Inyasi wa Loyola, Mtakatifu Agustino na wengine wengi.

Katika kusoma Maandiko Matakatifu na hadithi za Maisha ya Watakatifu tunaweza kupyaisha historia zetu na hadithi zetu binafsi. Roho Mtakatifu huangaza nyoyo zetu katika wongofu pale tunapoguswa na maisha ya wengine kwani hayo hututia shime na kutupatia mifano ya kufuasa katika kumtafuta na kumfahamu Mungu kwa karibu. Hadithi hizo hutuasa, hutukosoa na kutusaidia kwa zamu yetu kumsimulia Mungu hadithi na historia za maisha yetu binafsi hivyo kutuingiza katika majadiliano ya Upendo na Mungu. Ni kweli Mungu anafahamu fika maisha yetu, hata yale yaliyo katika undani wa siri ya moyo wetu, lakini kumsimulia mambo yetu hakumfanyi yeye kuwa kama anasikiliza habari zisizo na tija wala mashiko. Kumsimulia Mungu maisha yetu ni msaada kwetu kubadili mtazamo na kuchukua mwelekeo unaofaa zaidi katika mahusiano yetu naye na vilevile hutusaidia kugundua tulipokosea na kupata ufumbuzi kutoka kwa Mungu. Hata tunapomsimulia mambo yetu maovu ni wasaa kwetu kutengeneza nafasi ya wokovu kwa maisha yetu.

Baba Mtakatifu anahitimisha ujumbe wake kwa Siku ya 54 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni kwa Mwaka 2020 akielekeza mawazo yake kwa Bikira Maria Mama wa Yesu na mfano kwetu. Anasema,  yeye aliyempatia Mungu ubinadamu kwa kumtunga Mwanae katika tumbo lake, atusaidie kufumbua vifundo vya maisha yetu kwa  Upendo wa Mungu. “Ee Bikira Maria, mwanamke na mama, wewe uliyemtunga Neno wa Mungu katika tumbo lako, ukasimulia kwa maisha yako matendo makuu ya Mungu, sikiliza hadithi zetu na uzitunze salama katika moyo wako, uhifadhi hata zile hadithi zetu ambazo hakuna apendaye kuzisikiliza. Tufundishe kutambua kila kinachotuelekeza njia njema ya historia. Utazame mlima wa vifundo vinavyosonga maisha yetu na kupoozesha kumbukumbu zetu. Katika mikono yako laini vyote huweza kufunguliwa. Mama wa Roho, mama mwaminifu. Utuhamasihe nasi pia, utusaidie kutengeneza hadithi za amani na za mustakabali na utuoneshe njia ya kufuata pamoja.” AMINA.

Siku ya Mawasiliano Tanzania

 

01 August 2020, 13:58