Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa na imani thabiti kama ilivyokuwa kwa Mwanamke Mkananayo aliyevuta huruma, upendo na wokovu kwa binti yake. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa na imani thabiti kama ilivyokuwa kwa Mwanamke Mkananayo aliyevuta huruma, upendo na wokovu kwa binti yake. 

Papa: Imani ya Mwanamke Mkananayo na Wokovu wa Mungu!

Imani kubwa ni ile inayosheheni historia ya mtu mzima, ikiwa na majeraha yake, inayowekwa miguuni pa Kristo Yesu, ili aweze kuiganga na kuiponya na hatimaye, kuipatia maana na mwelekeo mpya wa maisha. Mwanamke Mkananayo ana imani thabiti kwa sababu anatambua kwamba, kamwe Mwenyezi Mungu hafurahii kifo cha mja wake, kila mtu akimbilie huruma na wokovu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Injili kama ilivyoandikwa na Mathayo, Sura ya 15: 21-28 inaelezea kwa kina na mapana imani ya mwanamke Mkananayo aliyekutana na Kristo Yesu, akampazia sauti akiomba rehema kwa binti yake anayepagawa sana na pepo. Lakini, Kristo Yesu, hakumjibu neno! Hiki ni kilio cha mwanamke ambaye amejaribiwa na kutikiswa sana na matatizo, kiasi cha kuonesha udhaifu wa mama kushindwa kumhudumia na kumtibu binti yake aliyekuwa anateseka kutokana na pepo wachafu! Mama Mkananayo, hakusita kupiga kelele kuomba rehema kutoka kwa Kristo Yesu. Wanafunzi wake wakamwendea, wakamwomba wakisema, “mwache aende zake kwa maana anapiga kelele nyuma yetu”. Lakini Kristo Yesu anawajibu akisema, hakutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. Yule mwanamke Mkananayo akaendelea kumwomba Kristo Yesu, ili amsaidie. Hapa ndipo Yesu anapotumia mithali akisema, “Si vema kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa”. Mwanamke Mkananayo mara moja akamjibu akisema kwa ujasiri, “Ndiyo Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yaangukayo mezani pa bwana zao.” Hii inaonesha kwamba, wema na huruma ya Mungu iliyofunuliwa kwa njia ya Kristo Yesu ni kwa ajili ya mahitaji ya watu wote wa Mungu. Hii ni hekima ambayo ilisheheni imani thabiti, kiasi hata cha kumgusa Kristo Yesu kutoka katika undani wake. Ndipo Kristo Yesu alipomjibu akamwambia “Mama imani yako ni kubwa! Na iwe kwako kama utakavyo. Akapona binti yake tangu saa ile.

Hii ni sehemu ya ufafanuzi uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 16 Agosti 2020, Jumapili ya XX ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, imani kubwa ni ile inayosheheni historia ya mtu mzima, ikiwa na majeraha yake, inayowekwa miguuni pa Kristo Yesu, ili aweze kuiganga na kuiponya na hatimaye, kuipatia maana na mwelekeo mpya wa maisha. Mwanamke Mkananayo ana imani thabiti kwa sababu anatambua kwamba, kamwe Mwenyezi Mungu hafurahii kifo cha mja wake. Ndiyo maana Mwinjili Mathayo anahitimisha tukio hili kwa kusema, “Akapona binti yake tangu saa ile.” Haya ni mapambazuko ya matumaini yanayoendelea kujitokeza hata kwa waamini katika ulimwengu mamboleo. Ikiwa kama waamini wataweza kujitokeza mbele ya Kristo Yesu jinsi walivyo, katika hali yao ya umaskini, kwa machozi ya toba na wongofu wa ndani; kwa shida na taabu, lakini zaidi kwa imani thabiti kama aliyokuwa nayo yule mwanamke Mkananayo, kwa hakika anasema Baba Mtakatifu Francisko, Kristo Yesu atasikiliza kwa jicho na moyo wa Kibaba, sala ya waja wake!

Katika hali na mazingira kama haya, wanafunzi wa Kristo Yesu wakagundua kwamba, hata kama mwanzoni mwa maisha na utume wake, ilionekana kana kwamba, utume wake wa uinjilishaji ulijielekeza zaidi kwa watu wa nyumba ya Israeli, lakini sasa Mwenyezi Mungu anaendelea kupanua zawadi ya wokovu hata nje ya mipaka ya Israeli, ili uweze kuwafikia watu wote kwa sababu hii ni zawadi ya Mungu kwa watu wote wa Mataifa. Sharti muhimu ili kuweza kupata zawadi ya wokovu kutoka kwa Mwenyezi Mungu ni kuamini nguvu ya Mkombozi na kujiaminisha bila kujibakiza katika wema wake wenye huruma. Hata leo hii, Kristo Yesu anaendelea kuwafundisha wanafunzi wake kwamba, hakuna pingamizi kwa imani inayosimikwa katika unyenyekevu kwa kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu.  Baba Mtakatifu amewaalika waamini kuchunguza dhamiri zao na kuangalia kila mmoja historia ya maisha yake, ikiwa kama amekuwa na ujasiri wa kupiga moyo konde na kumwendea Kristo Yesu, ili aweze kuwaganga na kuwaponya kutoka katika: mateso, mahangaiko na dhambi zao. Kwa ujasiri kama huu, mwamini ataweza kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yake. Jambo la msingi ni mwamini kuhakikisha kwamba, mbele ya macho yake ya imani, yupo Kristo Yesu, Mwenye moyo mpole na mnyenyekevu. Moyo Mtakatifu unaobubujika huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake; Moyo Mtakatifu unaobeba mateso, mahangaiko, dhambi na mapungufu ya binadamu.

Moyo Mtakatifu wa Yesu, ni kielelezo cha upendo wa Mungu usiokuwa na masharti, Mungu anayewapenda waja wake jinsi walivyo, kwa kutambua wema na ubaya unaowasonga nyoyoni mwao. Ili kuweza kuonja huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka, waamini hawana budi kujenga utamaduni wa kukutana mara kwa mara na Kristo Yesu kwanza kabisa katika: Neno lake Takatifu, Sakramenti za Kanisa na zaidi katika maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu anawashauri waamini kujijengea mazoea ya kutembea na Biblia Takatifu, ili wanapopata nafasi hata kidogo, waweze kuchungulia Neno la Mungu. Wale wenye simu za kisasa, watumie pia maendeleo haya makubwa ya sayansi na teknolojia, ili kuweza kuwasiliana na Kristo Yesu katika hija ya maisha yao ya kila siku. Kwa njia hii, waamini wataweza kukutana na Kristo Yesu, anayewapenda, upeo na kuwatakia kila jema la mbinguni.

Sala kuu ambayo, Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuimwilisha katika uhalisia wa maisha yao ni kumkimbilia Kristo Yesu na kumwambia, “Bwana, ukitaka waweza kuniponya na kunitakasa". Hii ni sala ya mwanamke mpagani, lakini ambayo imekuwa kweli ni kielelezo cha imani kubwa na hali ya kujiaminisha mbele ya Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu, ambaye amekuja kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Sala ya mwanamke mpagani, ambaye hata hakuwa Mkristo, Myahudi, lakini zaidi, mpagani, lakini leo hii, Mama Kanisa anamweka mbele ya waamini kuwa ni kielelezo cha imani thabiti! Hii inatokana na ukweli kwamba, Mwenyezi Mungu hutaka watu wote waokolewe, na kupata kujua yaliyo kweli. Kanisa ni Sakramenti ya Wokovu na hiki ndicho kiini cha maisha na utume wake. Hili ni Kanisa katoliki na wala si kwa ajili ya baadhi ya watu, bali watu wote bila ya kumtenga mtu awaye yote kutokana na tamaduni, kwani wote wanakiri imani kwa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai.

Mwishoni, Baba Mtakatifu amewaambia waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria, ili kwa njia ya sala na maombi yake, furaha ya imani ya kila mbatizwa, ari na kiu ya kutaka kuiungama na kuishuhudia katika uhalisia wa maisha kamili iweze kutekelezeka. Lengo ni kuhakikisha kwamba, Mwenyezi Mungu anapendwa, anasifiwa na kutukuzwa kutokana na kazi ya matendo ya huruma na wokovu.

Papa: Imani Thabiti
16 August 2020, 13:29