Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha kumbukumbu ya miaka 75 tangu mji wa Hiroshima na Nagasaki iliposhambuliwa kwa mabomu ya nyuklia. Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha kumbukumbu ya miaka 75 tangu mji wa Hiroshima na Nagasaki iliposhambuliwa kwa mabomu ya nyuklia. 

Miaka 75 Tangu Hiroshima Iliposhambuliwa kwa Nyuklia!

Baba Mtakatifu Francisko alikazia: madhara ya vita; misingi ya amani duniani kama inavyofafanuliwa na Mtakatifu Yohane XXIII katika Waraka wake wa Kitume, “Pacem in terris” yaani: “Amani Duniani”. Baba Mtakatifu anasema, Hiroshima ni mji ambao ndoto na matumaini ya watu yalitoweka na kuwaachia watu maafa makubwa ambayo kamwe hayataweza kusahaulika kwa urahisi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumuiya ya Kimataifa tarehe 6 Agosti 2020 inaadhimisha Kumbukumbu ya Miaka 75 tangu mji wa Hiroshima uliposhambuliwa kwa mabomu ya nyuklia na kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao, hadi wakati huu. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya Kitume nchini Japan Mwezi Novemba 2019, alipata bahati ya kutembelea Uwanja wa Kumbu kumbu ya Amani mjini Hiroshima na huko akasikiliza shuhuda za wahanga wawili: Yoshiko Kajimoto pamoja na Koji Hosokawa. Walielezea jinsi walivyoshuhudia marafiki zao wakizikwa wangali hai baada ya kufunikwa na kifusi cha udongo, kufumba na kufumbua wakaona mji wote umeteketea na kutoweka kabisa, giza nene likatanda na kuufunika mji wa Hiroshima na harufu mbaya ikaanza kusikika na hapo kukawa na milipuko mbali mbali. Zaidi ya watu 140, 000 kati ya watu 350, 000 waliokuwa wanaishi hapo wakapoteza maisha.

Hiroshima ukageuka kuwa ni makaburi ya watu wake; wengi waliathirika na hatimaye kufariki dunia kutokana na mionzi ya nyuklia. Hata leo hii kuna maelfu ya watu ambao wameathirika kutokana na mashambulizi ya mabomu ya nyuklia. Shuhuda za waathirika wa mashambulizi ya nyuklia mjini Hiroshima ziwe ni fundisho kuhusu madhara makubwa yanayoweza kusababishwa na matumizi ya silaha za maangamizi kama ilivyokuwa mjini Nagasaki na Hiroshima. Ni wajibu na dhamana kwa vijana wa kizazi kipya kuwa kweli ni vyombo na wajenzi wa amani duniani. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake, alizungumzia kuhusu: madhara ya vita; misingi ya amani duniani kama inavyofafanuliwa na Mtakatifu Yohane XXIII katika Waraka wake wa Kitume, “Pacem in terris” yaani: “Amani Duniani”. Alikazia umuhimu wa kukumbuka, kutembea na kulinda kwa pamoja kama njia ya kudumisha amani duniani. Baba Mtakatifu anasema, Hiroshima ni mji ambao ndoto na matumaini ya watu yalitoweka na kuwaachia watu maafa makubwa ambayo kamwe hayataweza kusahaulika kwa urahisi.

Baba Mtakatifu alisema alikwenda Hiroshima ili kutoa heshima yake kwa waathirika wa mashambulizi ya mabomu ya atomiki na kwamba, alikuwa kati yao kama hujaji wa amani katika ukimya na sala, ili kuwakumbuka na kuwaombea wale wote wanaotaka kujizatiti katika mchakato wa kutafuta amani. Moyoni wake alibeba machozi na masikitiko ya maskini ambao ndio waathirika wakubwa wa vita, chuki na kinzani mbali mbali duniani. Baba Mtakatifu alisema, yuko kati kati yao kama sauti ya watu wasiokuwa na sauti; shuhuda wa ukosefu wa haki; mambo yanayotishia: amani na mafungamano ya kijamii; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na vita inayohatarisha mustakabali wa amani duniani. Matumizi ya silaha za nyuklia ni uhalifu dhidi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu pamoja mazingira nyumba ya wote. Hakuna amani ya kweli wakati bado kuna mashindano ya utengenezaji wa silaha duniani; kuna sera za kibaguzi, chuki na uhasama.

Ikumbukwe kwamba, amani ya kweli inasimikwa katika misingi ya: Ukweli, haki, upendo na uhuru wa kweli kama anavyofafanua Mtakatifu Yohane XXIII katika Waraka wake wa Kitume “Pacem in terris” yaani: “Amani Duniani”. Kimsingi, watu wanatofautiana kwa mambo mengi sana, lakini kanuni hizi zinaweza kutumika ili kuheshimu na kuwawajibisha wanasiasa, ili kujizatiti katika kudumisha mafao ya wengi. Hii ni changamoto kwa watu wa Mungu kudumisha upendo, kwa kukuza majadiliano, mshikamano na matumizi bora zaidi ya nguvu kazi. Amani duniani inahatarishwa sana kutokana na vitisho vya silaha za nyuklia. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, amani siyo tu kutokuwepo kwa vita, bali ni matunda ya haki, maendeleo, mshikamano, utunzaji bora wa mazingira pamoja na kusimamia mafao ya wengi. Baba Mtakatifu anasema, Hiroshima iwe ni kumbu kumbu, ili watu wajitahidi kutembea kwa pamoja, kulinda na kudumisha misingi ya amani duniani.

Watu wasimame na kuthubu kusema, hatutaki tena vita! Watu wa Mungu wathubutu kujenga matumaini kwa kuwa ni vyombo vya upatanisho na haki na kwamba, wote wanayo hatima moja katika maisha. Kumbe, watu wote wanapaswa kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya mustakabali wa maisha yao kwa siku za usoni. Huu ni wakati wa kukataa katu katu utengenezaji na majaribio ya silaha za nyuklia. Watu wana kiu ya haki na amani ya kudumu. Miji ya Hiroshima na Nagasaki ni mahali ambapo panawapatia watu fursa ya kujifunza kusimama na kutafakari; kufunga, kutubu na kusali ili kutoa nafasi ya hekima na busara ya Mungu kutenda kazi katika maisha ya waja wake. Nagasaki iliharibiwa sana na mashambulizi ya mabomu ya atomiki, lakini ukawa ni chemchemi ya ukristo na mashuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Wakristo wakadhulumiwa na kuteswa sana, lakini ushuhuda wao ukaacha chapa ya kudumu katika akili na nyoyo za watu wa Mungu. Mjini Hiroshima, watu wanaendelea bado kuonja madhara na ukatili wa silaha za atomiki dhidi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Mji wa Hiroshima ni mahali ambapo binadamu amejifunza ukatili mkubwa unaofumbatwa katika utamaduni wa kifo. Ni kutokana na muktadha huu, Baba Mtakatifu anasema bila kupepesapepesa macho kwamba, matumizi  na ulimbikizaji wa silaha za atomiki ni kinyume cha maadili na utu wema. Mafundisho haya yatafafanuliwa na hatimaye kuingizwa kwenye Katekisimu ya Kanisa Katoliki kwa sababu madhara yake ni makubwa kwa familia ya binadamu. Pengine, kama alivyosema Einstein: Vita Kuu ya Nne ya Dunia watu watapigana kwa kutumia fimbo na mawe! Kuna mataifa ambayo yanachakata na kutengeneza silaha za kinyuklia, mengine yanahifadhi, hali inayotishia usalama na amani ya Jumuiya ya Kimataifa sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Usalama wa maisha ya binadamu na mazingira yake ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza kabla ya kuanza kufikiria utengenezaji, usambazaji na ulimbikizaji wa nishati ya nyuklia. Usalama wa maisha na afya ya watu ni mambo yanayopaswa kuzingatiwa sana.

Kuhusu Injili ya amani Baba Mtakatifu Francisko anasema, Vijana wanapaswa kujenga tabia ya kujiamini na kukabiliana na changamoto za maisha kwa ujasiri na busara, watambue nguvu na uzuri uliomo ndani mwao; udhaifu na mapungufu katika maisha na kwamba, kwa wale wanaotaka “kujimwambafai kwa kutumia mitandao ya kijamii wanadhani kwamba, kwa kufanya hivi wanakuwa ni watu muhimu sana katika jamii. Baba Mtakatifu anasema hiki ni kinyume chake kabisa kwani hawa ni watu waoga lakini wanataka kujitutumua kwa kutumia mitandao ya kijamii. Jukumu la kudhibiti unyanyasaji, uonevu na ubaguzi wa kimtandao ni dhamana inayopaswa kutekelezwa na vijana wenyewe kwa kuunganisha nguvu zao huku wakisaidiwa na taasisi za elimu pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kusema “HAPANA” ili kuwaonesha kwamba, haya wanayotenda si mambo mazuri kwa jamii.

Papa: Nyuklia

 

 

06 August 2020, 13:43