Papa Francisko: Katekesi Kuhusu Uponyaji wa Ulimwengu: Muhimu Kuzingatia: Utu, Heshima na Haki Msingi za Binadamu. Papa Francisko: Katekesi Kuhusu Uponyaji wa Ulimwengu: Muhimu Kuzingatia: Utu, Heshima na Haki Msingi za Binadamu. 

Papa: Uponyaji wa Ulimwengu: Utu na Heshima ya Binadamu

Mzunguko mpya wa katekesi unaongozwa na kauli mbiu “Uponyaji wa Ulimwengu."Magonjwa yanayomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo: mwono tenge wa mwanadamu, uharibifu wa mazingira nyumba; Ubinafsi na uchoyo. Amekazia umuhimu wa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu kama changamoto pevu ya kiimani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kuanzia sasa, anapenda kuwaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kujiunga pamoja naye, ili kutafakari kuhusu janga kubwa la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, kwa kuangalia madhara yake, mintarafu magonjwa ya kijamii. Tafakari hii makini, inaongozwa na Mwanga angavu wa Injili, Fadhila za Kimungu pamoja na Kanuni za Mafundisho Jamii ya Kanisa. Hii ni nafasi muafaka ya kutumia Mafundisho Jamii ya Kanisa, ili kuweza kuisaidia familia ya binadamu kuweza kuganga na kuponya ulimwengu huu unaoteseka kutokana na magonjwa makubwa na mazito! Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwa pamoja, wataweza kushiriki tafakari hii kama wafuasi wa Kristo Yesu anayeganga na kuponya, ili kujenga ulimwengu bora zaidi unaosimikwa katika matumaini kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Baba Mtakatifu katika mzungumo mpya wa katekesi unaongozwa na kauli mbiu “Uponyaji wa Ulimwengu”, Jumatano tarehe 12 Agosti 2020 amekita tafakari yake hasa kuhusu: Magonjwa yanayomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo: mwono tenge wa mwanadamu, uharibifu wa mazingira nyumba ya wote; Ubinafsi na uchoyo. Amekazia umuhimu wa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu kama changamoto pevu ya kiimani.  Baba Mtakatifu anasema, janga la Virusi vya Corona, COVID-19 limedhihirisha udhaifu na unyonge wa mwanadamu, kiasi kwamba, ili kuweza  kuponya ulimwengu kuna haja ya kusaidiana kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa wanyonge sanjari na kusimama kidete kutunza mazingira nyumba ya wote. Katika kipindi hiki kuna watu wengi ambao wamejitoa na kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa jirani zao wagonjwa kiasi hata cha kuhatarisha maisha yao.

Virusi vya Corona si gonjwa peke yake linalomwandamana mwanadamu katika ulimwengu mamboleo, lakini limetoa mwanga mkubwa zaidi kwa magonjwa ya kijamii yanayomwandama mwanadamu kujionesha zaidi. Kati ya magonjwa haya ni mwono tenge wa mwanadamu unaodharau utu na heshima ya binadamu; uwezo wake wa kufikiri na kutenda, kiasi cha kuangaliwa kuwa kama ni kichokoo au chombo kinachoweza kutumika. Huu ndio utandawazi wa kutojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Katika mwanga wa imani, Mwenyezi Mungu anamwangalia mwanadamu katika mwono tofauti kabisa, kwa sababu ameumbwa kwa sura na mfano wake; anao uwezo wa kupenda na kupendwa. Mwanadamu amepewa utu na heshima yake, changamoto na mwaliko kwa mwanadamu kuendelea kujenga na kudumisha mafungamano na Mwenyezi Mungu, jirani pamoja na mazingira nyumba ya wote. Mambo yote haya yanamwezesha mwanadamu kushiriki kikamilifu katika kazi ya uumbaji pamoja na ulinzi wa maisha; kwa kuitumia na kuitunza ardhi.

Katika Injili kama ilivyoandikwa na Mathayo, Sura ya 20: 20-38, Mama yake wana wa Zebayo anaoneshwa kama kielelezo cha tamaa na uchu wa madaraka, kwa kumtaka Kristo Yesu kuagiza ili wanawe wawili waketi mmoja mkono wake wa kulia na mwingine mkono wake wa kushoto katika Ufalme mpya ambao ungeanzishwa na Kristo Yesu. Lakini, jibu la Yesu ni wazi na makini kwa kusema kwamba: uongozi ni huduma na ni sadaka inayomtaka mwamini kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya jirani zake na ili kuonesha msisitizo huo, Kristo Yesu akawaponya vipofu wawili wa Yeriko na kuwafanya kuwa wafuasi wake. Kumbe, kuna haja kwa mwamini kuvuka  mwono unaogubikwa na ubinafsi na hivyo kumwangalia jirani yake kama ndugu na wala si kumgeuza kuwa ni kichokoo cha kupandia ngazi ya madaraka, wala kutaka kujimwambafai mbele ya wengine kwa kuwadharau kana kwamba, wao si mali kitu! Amani na utulivu wa ndani ni nguzo msingi katika huduma.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwajalia jicho makini, ili kuweza kuwangalia jirani zao, lakini zaidi maskini na wale wote wanaoteseka kwa sababu mbali mbali. Uchoyo na ubinafsi kamwe visipate nafasi katika maisha ya waamini. Wajitahidi daima kulinda, utu, heshima na haki msingi za binadamu bila kuangalia: lugha, rangi, tabaka au anapotoka mtu, bali kipaumbele cha kwanza ni utu wake! Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, binadamu ameumbwa kwa mfano na sura ya Mwenyezi Mungu, mwenye uwezo wa kumjua na kumpenda Muumba wake. Huu ndio msingi thabiti wa maisha ya kijamii na mwongozo wa utendaji wote wa mwanadamu. Mwelekeo huu unapewa uzito wa pekee katika Tamko la Haki Msingi za Binadamu, ambalo Mtakatifu Yohane Paulo II anakaza kusema, utu wa binadamu ni njia muhimu sana kwa maisha ya mwanadamu na kielelezo cha hali ya juu kabisa cha mwanadamu kinachopatikana katika dhamiri yake nyofu. Kuna haki binafsi, haki jamii, haki za watu na haki za mataifa. Itakumbukwa kwamba, mwanadamu ni kiumbe jamii ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu Mmoja katika Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Utu, heshima na haki msingi za binadamu ni mambo muhimu sana katika sera na mikakati ya shughuli za kiuchumi, kijamii na kisiasa. Binadamu wanapaswa kuangaliana na kuchukuliana kama ndugu na kwamba, kazi nzima ya uumbaji ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na inashangaza sana. Ni katika muktadha wa tafakari hii, mwanadamu hawezi kumwona jirani yake kuwa kana kwamba ni kiumbe wa ajabu au mgeni, bali mtu anayepaswa kupendwa na kuhudumiwa bila kinyongo wala uadui. Waamini kwa kuongozwa na mwanga wa imani, wanajitahidi  kwa njia ya neema na kwa kutumia kipaji chao cha ubunifu, ari na mwamko mpya kuweza kutafuta suluhu ya changamoto za kale. Wanaweza kufahamu na kutambua kwamba uwajibikaji wao unabubujika kutoka katika misingi ya imani, kama zawadi kwa ajili ya huduma kwa binadamu na kazi ya uumbaji.

Kama sehemu ya mchakato wa uponyaji wa ulimwengu dhidi ya virusi vinavyomwanadama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo, waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, hawana budi kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Imani iwasaidie kupona na kuongoka kutoka katika ubinafsi na uchoyo kama mtu binafsi na jamii katika ujumla wake, ili binadamu wote waweze kujisikia kuwa kweli ni familia moja ya binadamu wanaopaswa kuheshimiana na kuthaminiana; kwa kulinda na kutunza mazingira bora nyumba ya wote.

Papa: Utu wa Binadamu

 

 

 

 

 

12 August 2020, 14:05