Baba Mtakatifu anawataka wadau katika mgogoro wa Belarus kujikita zaidi katika mchakato wa majadiliano kwa kusimamia sheria, haki na wajibu wa kila upande, ili kuondokana na kinzani ambazo ni hatari sana. Baba Mtakatifu anawataka wadau katika mgogoro wa Belarus kujikita zaidi katika mchakato wa majadiliano kwa kusimamia sheria, haki na wajibu wa kila upande, ili kuondokana na kinzani ambazo ni hatari sana. 

Papa Francisko: Belarus: Majadiliano, Sheria na Haki Msingi!

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika wadau wote wanaohusika na mgogoro huu, kuhakikisha kwamba, wanajikita katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi sanjari na kukataa katu katu kishawishi cha kutaka kutumia nguvu na badala yake, wasimamie sheria, haki na wajibu. Papa amewaweka watu wa Belarus chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Malkia wa amani. Amani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 16 Agosti 2020, alisikika akisema kwamba, anafuatilia kwa wasi wasi mkubwa hali tete ya kisiasa nchini Belarus baada ya matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika nchini humo tarehe 9 Agosti 2020 na kumpatia ushindi Rais Alyaksandr Ryhoravich Lukashenka, ambaye amekuwa madarakani tangu tarehe 20 Julai 1995. Amebahatika kuongoza Belarus kwa miaka zaidi ya ishirini na mitano! Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kuwaalika wadau wote wanaohusika na mgogoro huu, kuhakikisha kwamba, wanajikita katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi sanjari na kukataa katu katu kishawishi cha kutaka kutumia nguvu na badala yake, wasimamie sheria, haki na wajibu. Baba Mtakatifu amewaweka watu wote wa Mungu nchini Belarus chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Malkia wa amani.

Wakati huo huo, Baraza la Maaskofu Katoliki Belarus, limeitaka Serikali kuacha mara moja kutumia nguvu kupita kiasi, hali inayopelekea watu wengi kupoteza maisha, kupata vilema vya kudumu na wengi wao kuishia magerezani. Mashambulizi yote haya dhidi ya watu wasiokuwa na hatia hayana mvuto wala mashiko kwa ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Belarus. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, Serikali inaunda mazingira ya majadiliano katika ukweli na uwazi kwa ajili ya ustawi, maendeleo, haki, amani na maridhiano kati ya wananchi wa Belarus. Baraza la Maaskofu Katoliki Belarus linasikitika kusema kwamba, matumizi ya nguvu kubwa dhidi ya raia yamejenga kinzani kubwa kati ya wananchi na vikosi vya ulinzi na usalama.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Tadeusz Kondrusiewicz, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Belarus, anawataka viongozi wa Serikali na wanasiasa kusimamia ukweli utakaowaweka huru na kamwe watu wa Mungu nchini Belarus hawatakubali kusadaka ukweli kwa ajili ya mafao ya wanasiasa na viongozi wanaotaka kutumia fursa hii ya hali tete ya kisiasa kwa ajili ya mafao binafsi. Vikosi vya ulinzi na usalama kufanya mauaji ya kinyama, kuwakamata na kuwaweka watu kizuizini bila hatia, kwa vile tu wanataka kufahamu ukweli ni dhambi kubwa na ukosefu wa maadili ya uongozi bora. Ni hatari sana kuvuruga misingi ya haki, amani na mafungamano ya kijamii, kwani madhara yake ni makubwa hata kwa vizazi vijavyo.

Wakati huo huo, Baba Mtakatifu amekumbusha kwamba, kwa watu wengi, huu ni muda wa likizo unaowapatia nafasi ya kupumzika ili kujichotea nguvu za kiroho na kimwili katika maisha yao. Likizo, kiwe ni kipindi cha sala, tafakari, ukimya pamoja na kufurahia kazi ya uumbaji ambayo Mwenyezi Mungu amemkabidhi mwanadamu, kuitunza na kuiendeleza. Likizo, isiwafanye watu kusahau kwamba, janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 bado lipo na linaendelea kuwatesa watu sehemu mbali mbali za dunia. Kuna familia nyingi ambazo zinateseka kutokana na ukosefu wa fursa za ajira na hivyo kushindwa kutekeleza dhamana na wajibu wake wa kifamilia. Kuna maskini ambao hawana chakula wala mahitaji yao msingi. Kumbe, likizo ya kipindi cha kiangazi, iwe ni fursa ya kujenga na kudumisha Injili ya upendo, mshikamano na ukaribu kwa familia na watu wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali katika maisha!

Papa: Belarus

 

 

17 August 2020, 14:30