Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko asema, Madhabahu ya Mtakatifu Rita wa Cascia ni chemchemi ya amani na utulivu wa ndani. Baba Mtakatifu Francisko asema, Madhabahu ya Mtakatifu Rita wa Cascia ni chemchemi ya amani na utulivu wa ndani. 

Papa:Madhabahu ya Mtakatifu Rita wa Cascia ni Chemchemi ya Amani

Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru Wamonaki wa Shirika la Mt. Augustino kwa sala, sadaka na majitoleo yao. Amewahakikishia kwamba, iko siku atawatembelea kwani hapa ni kisima cha amani, kwani wale wote waliovunjika na kupondeka moyo wanaweza kujichotea nguvu na kuanza tena kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu, huku wakifuata ile njia ya ukweli inayowaweka huru!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amewaandikia ujumbe wa shukrani Wamonaki wa Shirika la Mtakatifu Augustino, Monasteri ya “Santa Rita da Cascia”, kwa maua matano ya waridi waliyomtumia kama kielelezo chao cha sala kwa ulinzi na tunza ya watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Mawaridi haya yalibarikiwa kunako tarehe 22 Mei 2020, Kumbukumbu ya Mtakatifu Rita wa Cascia. Baba Mtakatifu amewaambia Wamonaki hawa kwamba, maua yale ameyaweka chini ya Sanamu ya Bikira Maria kwa ajili ya ulinzi na tunza yake ya kimama, hasa wakati huu, watu wa Mungu wanapoendelea kupambana na janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, yote yanawezekana kwa mtu mwenye imani thabiti. Katika kipindi hiki cha maambukizi makubwa ya Virusi vya Corona, COVID-19, Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu ni matumaini ya waja wake. Jambo la msingi ni kwa waamini kuendelea kuwa waaminifu katika kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao. Huu ni wakati wa kusimama na kuendelea na safari ya ujenzi wa leo na kesho iliyobora zaidi kadiri ya mapenzi ya Mungu. Wamonaki wa Shirika la Mtakatifu Augustino, Monasteri ya “Santa Rita da Cascia” wameupokea ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa mikono miwili. Hiki ni kielelezo makini cha uwepo wa karibu wa Baba Mtakatifu kwa watawa.

Hawakuwaza hata mara moja kwamba, maua yale yaliyobarikiwa kwenye Monasteri yao, yangeweza kuwa ni sehemu kubwa ya habari na hata kufurahiwa na Baba Mtakatifu Francisko. Kwa hakika huu ni moyo wa shukrani na mapendo makubwa mbele yao! Kuna umati mkubwa wa watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia, wenye Ibada kwa Mtakatifu Rita wa Cascia. Maadhimisho ya Mwaka huu, yameathiriwa sana na maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Katika maadhimisho ya kumbukumbu ya Mtakatifu Rita wa Cascia, Wamonaki hawa wamemtumia pia maua ya waridi Rais Sergio Mattarella pamoja na viongozi mbali mbali wa Italia.

Kwa upande wake, Baba Mtakatifu amewashukuru kwa sala, sadaka na majitoleo yao. Amewahakikishia kwamba, iko siku atawatembelea kwani hapa ni kisima cha amani, kwani wale wote waliovunjika na kupondeka moyo wanaweza kujichotea nguvu na kuanza tena kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu, huku wakifuata ile njia ya ukweli inayowaweka huru! Ni matumaini ya Rais Sergio Mattarella wa Italia kwamba, Mtakatifu Rita wa Cascia, ataendelea kuwaombea na kuwasindikiza watu wa Mungu nchini Italia, ili hatimaye, kuweza kuvuka janga hili la maambukizi makubwa ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Sala na sadaka ya Wamonaki hawa ni faraja kubwa kwa watu wa Mungu ambao wameguswa na kutikiswa kutoka katika undani wa maisha yao! Ni wakati muafaka kwa Serikali kuendelea kujizatiti zaidi katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Italia!

Mtakatifu Rita

 

15 June 2020, 13:21