Mchango wa Baba Mtakatifu Francisko katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene duniani! Mchango wa Baba Mtakatifu Francisko katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene duniani! 

Mchango wa Papa Francisko katika Harakati za Kiekumene Duniani!

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video kwa mwaka 2020 anasema, athari za maambukizi makubwa ya homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-16 yamewafanya watu kuwa na hofu pamoja na taharuki kiasi cha kutengana, lakini Roho Mtakatifu Mfariji, atawawezesha wale wanaomtumainia Mungu, faraja katika mahangaiko yao. Mshikamano!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Roho Mtakatifu ni mhimili mkuu wa umoja wa wale wanaotangaza na kushuhudia Injili. Mitume walikuwa na ari na mwamko wa kuwashirikisha watu wa Mungu, kile ambacho walikuwa wamepokea! Roho Mtakatifu ni kiini cha siri ya umoja kama zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayowashirikisha wengine, ili kuweza kumfahamu Mungu anayeleta mageuzi katika sakafu ya maisha ya mwamini. Waamini wakilitambua hili, wala hakuna sababu ya kuteseka kutafuta nafasi, kutambulikana au kuwa na uchu wa madaraka. Waamini wahakikishe kwamba, maisha yao yanakuwa pia ni zawadi. Kwa njia hii, wataweza: kupenda kwa unyenyekevu, kuhudumia kwa furaha na katika uhuru kamili, kama kielelezo cha sura ya kweli ya Mwenyezi Mungu. Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni hadi Sherehe ya Pentekoste, imekuwa ni fursa kwa Makanisa sehemu mbali mbali za dunia kuendelea kusali kwa ajili ya kuombea umoja wa Wakristo.

"Thy Kingdom Come" yaani “Ufalme wako ufike” ni harakati za mchakato wa kiekumene zilizoanzishwa kunako mwaka 2016 na zinayaunganisha Makanisa na Madhehebu ya Kikristo yapatayo 172. Kwa mara ya kwanza Baba Mtakatifu Francisko, alituma ujumbe wake kwa njia ya video kwenye maadhimisho haya kunako mwaka 2019, kwa mwaliko kutoka kwa Askofu mkuu Justin Welby wa Jimbo kuu la Canterbury, Uingereza ambaye pia ni kiongozi mkuu wa Kanisa la Anglikani. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video kwa mwaka 2020 anasema, athari za maambukizi makubwa ya homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-16 yamewafanya watu kuwa na hofu pamoja na taharuki kiasi cha kutengana, lakini Roho Mtakatifu Mfariji, atawawezesha wale wanaomtumainia Mungu, faraja katika mahangaiko yao. Hii ni changamoto kwa Wakristo kushikamana kwa dhati, ili waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Roho Mtakatifu awajalie hekima na busara, ili viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa waweze kufanya maamuzi yatakayosaidia kukuza na kudumisha uhai wa mwanadamu, utu, heshima na haki zake msingi.

Kardinali Kurt Koch anasema, Mama Kanisa anaadhimisha Jubilei ya Miaka 25 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipochapisha Waraka wake wa Kitume “Ut unum sint” yaani “Ili wawe wamoja: Dhamana ya Kiekumene”. Ujumbe huu ulichapishwa hapo tarehe 25 Mei 1995. Mchakato wa majadiliano ya kiekumene ni dhamana inayoendelezwa mbele. Baba Mtakatifu Francisko anatambua fika kwamba, dhamana na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro ni kati ya vikwazo vya mchakato wa ujenzi wa umoja wa Wakristo. Lakini pia anatambua fika kwamba, Kanisa Katoliki linao mchango wa pekee katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo linasema, ushiriki wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya harakati za kiekumene miongoni mwa Makanisa na Madhehebu mbali mbali ya Kikristo ni kielelezo kwamba, majadiliano ya kiekumene ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa Katoliki.

Hii ni changamoto inayobubujika kutoka katika Sala ya Yesu “Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako, hao nao wawe ndani yetu, ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba, wewe ndiye uliyenituma” Yn. 17:21. Kumbe, umoja ni matokeo ya kushukiwa na Roho Mtakatifu na hii ndiyo nguvu inayowaunganisha kama wafuasi wa Kristo Yesu. Mitume waliweza kushuhudia kwa macho yao kwani watu wa Mungu waliweza kusema kwa lugha nyingine kama Roho Mtakatifu alivyowajalia kutamka, kwa sababu Roho Mtakatifu ni chemchemi ya umoja. Uekumene wa sala ni sehemu muhimu katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaofumbatwa katika ushuhuda na kama sehemu ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Wakristo wanapaswa kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa watu wa Mataifa!

Mchano wa Papa Francisko katika ujenzi wa Umoja wa Wakristo
08 June 2020, 13:42