Baba Mtakatifu Francisko ametoa zawadi ya Gari la Kubebea wa Wagonjwa Maskini wa mjini wa Roma. Baba Mtakatifu Francisko ametoa zawadi ya Gari la Kubebea wa Wagonjwa Maskini wa mjini wa Roma. 

Papa Francisko atoa Gari la Wagonjwa kwa Maskini wa Roma!

Baba Mtakatifu Francisko kabla ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, alibariki gari maalum la kubebea wagonjwa maskini, waliko mjini Roma. Gari hili amekabidhiwa Kardinali Konrad Krajewski, Mtunza Sadaka mkuu wa Kipapa kwa ajili ya maskini wasiokuwa na makazi maalum; watu wanaojipatia hifadhi kuzunguka viunga vya Roma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake anakaza kusema “Maskini ni amana na utajiri wa Kanisa”: Hawa ni walengwa wakuu wa Habari Njema ya Wokovu inayopaswa kutangazwa na kushuhudiwa kwa watu wa Mataifa. Mtakatifu Francisko wa Assisi akawa ni mfano wake wa kuigwa katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa kutambua wazi kwamba, si rahisi sana kuiga mfano wa maisha ya Mtakatifu Francisko wa Assisi ambaye alichezea sana ujana wake, lakini alipokutana na Uso wa huruma ya Mungu, akatubu, akaongoka na kujisadaka kwa ajili ya kulipyaisha tena Kanisa la Mungu. Maskini kadiri ya Papa Francisko ni dhana inayowakumbatia: maskini wa hali na kipato; watu waliokengeuka na kutopea katika utepetevu wa kanuni maadili na utu wema! Hawa ni wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi ugenini hata kiasi cha kuhatarisha maisha yao! Ni waathirika wa biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo unaonyanyasa na kudhalilisha utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Maskini ni watoto wanaodhalilishwa kijinsia, wanaotumikishwa kwenye kazi za suluba na hata kubebeshwa mtutu wa bunduki, kama chambo cha vita! Maskini ni wafungwa magerezani wanaotamani kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Magereza yawe ni nafasi ya kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kuandika tena kurasa mpya zinazofumbatwa kwenye Injili ya furaha na matumaini! Maskini ni wazee na wagonjwa; watu wasiokuwa na makazi maalum. Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake, anaendelea kutoa kipaumbele cha kwanza kwa watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii na mambo msingi ya maisha kutokana na hali zao mbali mbali, ili waweze kuonjeshwa tena ile furaha ya Injili inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Baba Mtakatifu, Jumapili tarehe 31 Mee 2020, Sherehe ya Pentekoste, kabla ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, alibariki gari maalum la kubebea wagonjwa maskini, waliko mjini Roma.

Gari hili amekabidhiwa Kardinali Konrad Krajewski, Mtunza Sadaka mkuu wa Kipapa kwa ajili ya maskini wasiokuwa na makazi maalum; watu wanaojipatia hifadhi kuzunguka Kanisa kuu la Mtakatifu Petro na kwenye viambaza vya mabarabara ya mji wa Roma. Hawa ni watu wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi, kiasi kwamba, hata wakati mwingine si rahisi sana kuonekana na Serikali pamoja na taasisi mbali mbali za huduma. Kutokana na maambukizi makubwa ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, maskini na watu wasiokuwa na makazi maalum wamekumbana na changamoto kubwa katika kipindi hiki. Lakini Vatican imeendelea kutoa huduma ya afya kwa watu hawa! Kardinali Konrad Krajewski, Mtunza Sadaka mkuu wa Kipapa kwa kushirikiana na kusaidiana na madaktari, wauguzi na wahudumu wa sekta ya afya wamekuwa wakijitahidi kutoa msaada wa huduma ya afya kwa ajili ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kuna kituo maalum cha huduma ya kwanza kwa maskini na wale wote wasiokuwa na bima ya afya! Lengo ni kulinda utu, heshima na haki msingi za binadamu kama ushuhuda wa Injili ya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake!

Papa: Maskini
02 June 2020, 13:24