Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Siku ya 54 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni kwa Mwaka 2020. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Siku ya 54 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni kwa Mwaka 2020. 

Ujumbe wa Papa Francisko Siku ya 54 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni

Ujumbe wa Siku ya 54 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni unaongozwa na kauli mbiu “Nawe upate kusema masikioni mwa wanao, na masikioni mwa mjukuu wako” Kitabu cha Kutoka:10:2. Maisha yanakuwa ni historia”. Kuhusu mwingiliano wa hadithi na kwamba, si kila hadithi ni hadithi njema. Kuna hadithi ya hadithi; hadithi iliyopyaishwa na hadithi inayoendelea kumpyaisha mwanadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 54 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni inayoadhimishwa na Mama Kanisa tarehe 24 Mei 2020 sanjari na Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni, unaongozwa na kauli mbiu “Nawe upate kusema masikioni mwa wanao, na masikioni mwa mjukuu wako” Sehemu ya Maandiko Matakatifu kutoka katika Kitabu cha Kutoka:10:2. Maisha yanakuwa ni historia. Katika ujumbe huu, Baba Mtakatifu anapembua kwa kina na mapana kuhusu mwingiliano wa hadithi na kwamba, si kila hadithi ni hadithi njema. Kuna hadithi ya hadithi; hadithi iliyopyaishwa na hatimaye kuna hadithi inayoendelea kumpyaisha mwanadamu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanamwilisha ndani mwao ukweli wa historia ya Habari Njema ya Wokovu

Hizi ni historia zinazowajenga watu badala ya kuwaporomosha; zinawasaidia watu kugundua asili yao na nguvu zinazohitajika ili kusonga mbele. Hata katika makelele na ujumbe mwingi, bado kunahitajika historia ya binadamu inayomzungumzia binadamu mwenyewe na uzuri unaomzunguka. Ni historia inayouangalia ulimwengu sanjari na yote yanayoendelea kutendeka kwa jicho jema. Ni simulizi inayoweza kumwonesha mwanadamu kuwa ni sehemu ya maisha na kwamba, wanategemeana. Ni simulizi ambalo linawafunulia watu mwingiliano na mafungamano yanayowaunganisha kwa pamoja. Baba Mtakatifu anasema, kimsingi binadamu ni mtamba hadithi tangu katika mifumo mbali mbali tangu kuzaliwa kwake hata kama halitambui hilo. Mwanadamu anaweza kuamua ni hadithi ipi ni nzuri au mbaya kwa kulinganisha na wahusika wakuu na ukweli ambao wameunafsisha. Hadithi huacha alama katika maisha ya mwanadamu, zinasaidia kujenga misimamo na tabia ya watu. Hadithi zinaweza kumsaidia mtu kujifahamu na kuwasiliana na wengine jinsi alivyo!

Baba Mtakatifu anasema, mwanadamu anahitaji “kushonewa mavazi” ili kuficha udhaifu wake; anahitaji hadithi ili kulinda maisha yake; kwa kudumisha mwingiliano na maandishi. Hadithi za watu wa vizazi mbali mbali yana mambo yanayowaunganisha. Hawa ni mashujaa wa kila siku wanaosimama kidete kupambana na hali ngumu na ubaya wa moyo wakiwa na ujasiri pamoja na nguvu ya upendo. Mwanadamu kwa kuzama katika hadithi anaweza kupata ari na nguvu ya kuweza kukabiliana na changamoto za maisha. Binadamu ni mtamba hadithi kwa sababu hii ni sehemu ya ukuaji wake, inayomsaidia kujitambua na kutajirishwa katika hatua mbali mbali za maisha. Lakini, tangu mwanzo wa historia ya mwanadamu, hadithi imekuwa ikitishiwa sana. Baba Mtakatifu anakaza kusema, si kila hadithi ni hadithi njema. Katika Kitabu cha Mwanzo, Nyoka alimjaribu na mwamke kwa kusema mkila matunda ya mti huo… nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya!

Kishawishi hiki kimemtumbukiza mwanadamu katika lindi la dhambi kiasi hata cha kushindwa kujinasua. Huu ni ujumbe unao onekana kumjengea matumaini. Hata leo hii kuna watu wanasimulia hadithi za kuwanyonya wengine; kwa kuwajengea mazingira ya huzuni; kwa kumilikiwa, kutawaliwa na kugeuzwa kuwa ni walaji. Watu wamekuwa wachoyo kiasi cha kuwa ni wapiga majungu na wasengenyaji wakuu; wamekuwa ni walaji wa kupindukia wa hadithi za vita, uwongo na ulaji. Njia mbali mbali za mawasiliano ya jamii zimetumika kama jukwaa la maangamizi na hadithi potofu zinazovuruga ujenzi wa umoja na mafungamano ya kijamii. Kwa kuunga uunga habari zisizokuwa na uhakika; sanjari na kurudia rudia mambo yasiyokuwa na msingi; vyombo vya mawasiliano ya jamii vimekuwa chanzo cha kusambaza ujumbe unaowagawa wanadamu na kuvuruga historia, utu na heshima ya mwanadamu.

Pale ambapo hadithi zimetumika kwa ajili ya kuwanyonya watu na kuendekeza uchu wa madaraka, hadithi za namna hii haziwezi kudumu hata kidogo. Hadithi nzuri inavuka mipaka, nafasi na nyakati. Katika ulimwengu ambamo hadithi za kughushi zinaendelea kushika kasi kubwa, kuna haja ya kuwa na busara, ili kukaribisha na kuunda hadithi njema, zenye uzuri na ukweli. Watu wawe na ujasiri wa kukataa hadithi zisizo na ukweli na zile hadithi mbaya. Watu wanahitaji uvumilivu na manga’amuzi ili kugundua hadithi ambazo zitamsaidia mwanadamu kutokupoteza mwingiliano, licha ya matatizo mbali mbali yanayoendelea kujitokeza. Binadamu anahitaji hadithi zinazojitahidi kumfunulia mwanadamu ukweli kuhusu jinsi alivyo pamoja na kusimulia hadithi za mashujaa wa kila siku! Baba Mtakatifu anasema, kuna hadithi ambazo ni hadithi kweli kweli. Maandiko Matakatifu ni hadithi yenye matukio na wahusika mbali mbali kama jamii na hata kama mtu mmoja mmoja.

Maandiko Matakatifu yanamwonesha Mwenyezi Mungu ambaye ni Muumbaji na Mtamba hadithi, ambaye kwa neno lake, aliumba vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana. Alimuumba mwanaume na mwanamke, akajenga mahusiano pamoja na kuzungumza nao. Mzaburi katika Zaburi yake ya 139:13-15 anakiri heshima kwa Mwenyezi Mungu anayefahamu yote. Kwa maana ndiye aliyemuumba, akamuunga tumboni mwa mama yake kwa siri na ustadi mkubwa. Zawadi ya maisha ni mwaliko wa kuendeleza fumbo hili la ajabu. Biblia ni hadithi kubwa ya upendo kati ya Mungu na mwanadamu na kiini cha hadithi hii ni Kristo Yesu, changamoto na mwaliko kwa vizazi vyote kujizatiti kukumbuka na kuendelea kusimulia matukio makuu ya hadithi ambayo ni hadithi kweli kweli; hadithi zinazosimulia maana yake. Israeli alipokuwa utumwani, akamlilia Mungu naye akakisikiliza kilio chake na kukumbuka Agano alilofanya na Ibrahimu, Isaka na Yakobo. Mungu akawaona wana wa Israeli na Mungu akawaangalia. Rej. Kut. 2: 24-25.

Kumbukumbu ya Mwenyezi Mungu ni chemchemi ya ukombozi inayopaswa kusimuliwa kwa vizazi vyote, ili kuonesha kwamba, hata leo hii, Mwenyezi Mungu bado yuko kati pamoja na watu wake. Mungu wa uhai anaendelea kuwasiliana na mwanadamu kwa njia ya hadithi ya maisha. Kristo Yesu alisimulia kuhusu Mwenyezi Mungu kwa njia ya mifano na hadithi fupi fupi kutoka katika uhalisia wa maisha ya watu. Ni katika muktadha huu, maisha yanakuwwa ni hadithi na kwa hadhira, hadithi inakuwa maisha na hivyo kuwa ni sehemu ya maisha ya watu wanaosikiliza na kuruhusu mabadiliko yafanyike ndani mwao. Injili ni hadithi kumhusu Kristo Yesu na ni hadithi inayowafananisha waamini na Kristo Yesu. Waamini wanahamasishwa kuwashirikisha wengine imani na maisha. Mwenyezi Mungu alipenda Mwanae wa pekee aweze “kufunuliwa” (exegèsato, Rej. Jn.1:18) na “kutangazwa” kati ya watu wa Mataifa ili awe ni sehemu ya mwingiliano wa hadithi ya mwanadamu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema hii ni hadithi iliyopyaishwa kwani inamwonesha Mwenyezi Mungu anavyojitaabisha kwa ajili ya binadamu kiasi kwamba, kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, akawa binadamu na kwamba, kila hadithi ya mwanadamu ina maana yake. Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho hata hadithi ya binadamu imekuwa ni hadithi ya Mungu, inayo hadhi na utu wake. Binadamu anahitaji kusikiliza hadithi kadiri ya kiwango kilichotolewa na Kristo Yesu. Mtakatifu Paulo anawaandikia Wakorintho akisema wao wamekuwa barua ya Kristo waliyoikatibu, iliyoandikwa si kwa wino, bali kwa Roho wa Mungu aliye hai; si katika vibao vya mawe, ila katika vibao ambavyo ni mioyo ya nyama. Kwa njia ya Roho Mtakatifu kila hadithi inapaswa kukumbukwa. Kuna waandishi ambao wameandika hadithi mbali mbali zinazoonesha jinsi ambavyo uhuru wa Mungu unakutana na ule wa mwanadamu. Watu wengi wanafahamu hadithi zenye harufu ya Injili, ambazo zimegeuka kuwa chemchemi ya upendo unaoleta mabadiliko katika maisha. Hizi ni hadithi ambazo watu wanapaswa kushirikishana, kusimuliwa tena na tena na kupyaishwa katika kila hatua ya maisha, kila lugha na katika kila njia ya mawasiliano ya jamii.

Baba Mtakatifu Francisko katika Ujumbe wake wa Siku ya Upashanaji Habari Ulimwenguni anaendelea kudadavua akisema kwamba, hii ni hadithi inayopyaisha maisha ya waamini kwa sababu hadhi zao zinakuwa ni sehemu ya hadithi hii. Maandiko Matakatifu, hadithi za watakatifu pamoja na maandiko mbali mbali yanayo toa mwanga angavu katika nyoyo na uzuri wake ni kazi ya Roho Mtakatifu. Upendo wa Mungu unajidhihirisha katika kazi ya uumbaji na ukombozi, changamoto na mwaliko kwa waamini kumwilisha Injili ya upendo na huruma katika maisha yao, ili kuweza kuandika ukurasa mpya. Waamini wawe na ujasiri wa kujifunua kwa jirani zao wakiwa na wazo pana kwamba, hata wao ni watamba hadithi waliobobea. Binadamu wanapaswa kuwa ni watamba hadithi ya Mungu inayobadilika kila wakati; hadithi inayowakirimia wengine upendo wenye huruma. Kumbe, waamini wanaweza kusimulia hadithi zao na zile za jirani zao kadiri ya mazingira wanamoishi, dhamana kubwa kwa kila mwamini.

Kila hadithi ya mwanadamu iko wazi kwa ajili ya kufanyiwa maboresho, ili kupata wokovu na kuona mema katika maisha ya watu na hivyo kuyapatia mwanya! Binadamu wanapaswa kutambua kwamba, wanayo thamani kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu. Kumbe, wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa Roho Mtakatifu. Ili kuweza kufikia hatua hii, kuna haja kwa waamini kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu, aliyehifadhi yote moyoni mwake. Kwa maombezi yake ya daima, ataweza kufungua mafundo ya maisha kwa nguvu yake ya upendo. Aweze kusikiliza na kuhifadhi hadithi katika moyo wake Mtakatifu. Awasaidie kutambua mambo mazuri yanayowaunganisha katika maisha; afungue mafundo ya maisha yanayohatarisha kumbukumbu. Bikira Maria awasaidie waamini kutunga hadithi za amani na zile zenye mtazamo mpana zaidi.

Papa: Ujumbe Siku ya 54 ya Upashanaji Habari

 

 

21 May 2020, 14:15