Ni matumaini ya Papa Francisko kwamba, Taasisi ya Utamaduni ya Chuo Kikuu cha Kipapa cha Angelicum itasaidia kufanya upembuzi yakinifu kuhusu changamoto mamboleo za utamaduni. Ni matumaini ya Papa Francisko kwamba, Taasisi ya Utamaduni ya Chuo Kikuu cha Kipapa cha Angelicum itasaidia kufanya upembuzi yakinifu kuhusu changamoto mamboleo za utamaduni. 

Ujumbe wa Papa Francisko: Taasisi ya Utamaduni, Angelicum

Lengo la Taasisi hii ni kufanya upembuzi yakinifu kuhusu tamaduni mamboleo, kwa kushirikiana na wanafalsafa, wanataalimungu pamoja na wanawake waliobobea katika medani hii. Papa Yohane Paulo II, ni kiongozi anayestahili kupewa shukrani kutokana na amana na utajiri mkubwa ambao ameliachia Kanisa; Ushuhuda, tafakari ya kina kuhusu: Mungu, binadamu na kazi ya Uumbaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kama sehemu ya Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu kuzaliwa kwa Mtakatifu Yohane Paulo II, tarehe 18 Mei 2020, Chuo Kikuu cha Kipapa cha Mtakatifu Thoma wa Akwino, Angelicum, kilichoko mjini Roma, kimezindua rasmi Taasisi ya Utamaduni, itakayokuwa chini ya Kitivo cha Falsafa. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko amemwandikia ujumbe, Padre Michal Paluch, O.P., Gambera wa Chuo Kikuu cha Kipapa cha Angelicum, akimpongeza kwa hatua hii muhimu. Anawapongeza wajumbe wa Mfuko wa “Futura Iuventa” na wa “Saint Nicholas” inayofadhili Taasisi ya Utamaduni, Chuo Kikuu cha Angelicum. Baba Mtakatifu anasema, lengo la Taasisi hii ni kufanya upembuzi yakinifu kuhusu tamaduni mamboleo, kwa kushirikiana na wanafalsafa, wanataalimungu pamoja na wanawake waliobobea katika medani hii. Mtakatifu Yohane Paulo II alikuwa ni muasisi na lengo kuu la Mradi huu. Ni kiongozi anayestahili kupewa shukrani kutokana na amana na utajiri mkubwa ambao ameliachia Kanisa; lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wa uwazi wa mawazo yake, tafakari ya kina sanjari na upendo wake kwa Mwenyezi Mungu na binadamu; kwa kazi ya uumbaji, historia na sanaa!

Mtakatifu Yohane Paulo II alikuwa na uzoefu na mang’amuzi makubwa katika historia na maisha katika ujumla wake, kiasi kwamba, mateso yake binafsi yanapaswa kutafsiriwa mintarafu mtazamo wake uliomwezesha kufanya tafakari ya kina kuhusu binadamu na mizizi yake ya kitamaduni kama njia mahususi ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Mtakatifu Yohane Paulo II katika Wosia wake wa kwanza wa Kitume “Redemptor Hominis” yaani “Mkombozi pekee wa Binadamu” katika muktadha huu alisema, Kanisa linapaswa kuziendea tamaduni, itikadi, dhana pamoja na watu wote wenye mapenzi mema. Kanisa liwaendee kwa kuwajali, kuwaheshimu na kufanya mang’amuzi ambayo tangu nyakati za Mitume, yamekuwa ni mwongozo wa shughuli za kimisionari. Ni vyema kukumbuka hotuba ya Mtume Paulo mbele ya Areopago mjini Athene. Ni tabia ya kimisionari kuthamini mambo msingi yaliyomo ndani ya mwanadamu, kwa yale yote aliyotenda katika maisha yake kwa siku za nyuma ili kushughulikia matatizo yanayomsibu.

Hili ni suala la kuheshimu kila kitu kilicholetwa na Roho Mtakatifu anayetenda kadiri anavyopenda. Baba Mtakatifu Francisko anasema hii ni dhana inayopaswa kuvaliwa njuga, ikiwa kama Kanisa linataka “kutoka kifua mbele” badala ya kuridhika kwa kutunza na kuratibu yale yaliyopo, lakini daima Kanisa likiendelea kuwa aminifu kwa utume wake! Baba Mtakatifu anakipongeza Chuo Kikuu cha Kipapa cha Angelicum kwa kupokea wazo hili na kulifanyia kazi. Angelicum ni Jumuiya ya Wasomi kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Hapa ni mahali muafaka pa kuweza kufanya upembuzi yakinifu kuhusu changamoto msingi za utamaduni katika ulimwengu mamboleo. Baba Mtakatifu analipongeza Shirika la Wadominikan ambalo limeendelea kutoa tafakari ya kina katika masuala ya imani na maudhui yake mintarafu mafundisho ya Mtakatifu Thoma wa Akwino. Yote haya ni mazingira yatakayosaidia kuendeleza Taasisi ya Utamaduni, Chuo Kikuu cha Angelicum. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Taasisi hii itajipambanua kwa kuwa na ujasiri wa ukweli, uhuru wa kiroho na ukweli wa kiakili. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amewatakia wote heri na baraka wale wote waliojisadaka bila ya kujibakiza ili kuhakikisha kwamba, Taasisi hii inaanzishwa.

Papa: Angelicum

 

18 May 2020, 13:30