Baba Mtakatifu Francisko katika mzunguko mpya wa Katekesi kuhusu Fumbo la Sala anasema, Sala na Kielelezo cha hali ya juu kabisa cha imani na matumaini kwa Mwenyezi Mungu Baba Mtakatifu Francisko katika mzunguko mpya wa Katekesi kuhusu Fumbo la Sala anasema, Sala na Kielelezo cha hali ya juu kabisa cha imani na matumaini kwa Mwenyezi Mungu 

Papa Francisko: Sala ni Kielelezo cha Hali ya Juu cha Imani!

Baba Mtakatifu asema sala ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha imani kwa Mwenyezi Mungu, chemchemi ya mapendo yenye huruma kwa waja wake. Waamini wawe na ujasiri wa kumwomba, ili waweze kuwa na moyo wa unyenyekevu na matumaini, daima waoneshe kiu ya uwepo wa Mungu katika maisha yao. Kristo Mfufuka, awe ni chemchemi ya amani na furaha ya kweli mioyoni mwao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Katekesi yake kuhusu Fumbo la Sala, Jumatano, tarehe 6 Mei 2020, ametumia fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza waamini na watu wote wenye mapenzi mema ambao walikuwa wamejiunga naye kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandoa ya kijamii. Anasema, Kipindi cha Pasaka ni muda muafaka wa kufurahi kwa kujichotea nguvu kutoka kwa Kristo Mfufuka. Ni mwaliko wa kutoka katika ubinafsi na kuanza kujenga madaraja ya mshikamano wa upendo na watu wanaoteseka sehemu mbali mbali za dunia hasa kutokana na athari za maambukizi makubwa ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, Covid-19.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuwa ni mashuhuda, vyombo na mwanga wa faraja na matumaini kwa wale wote walioathirika kwa ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Waamini waendelee kujifunza kutoka kwa “Mwana wa Timayo, Bartimayo kipofu aliyepiga kelele na kumwita Yesu kwa jina linalojulikana na Wayahudi wote: “Yesu mwana wa Daudi, unirehemu”. Bartimayo kwa imani thabiti kabisa alikuwa anaomba rehema. Waamini wasichoke kumwomba Mwenyezi Mungu kwani atawakirimia kadiri ya wema na huruma yake kwa wakati muafaka, kwa ajili ya ustawi na wokovu wa roho zao! Ikumbukwe kwamba, Sala ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha imani kwa Mwenyezi Mungu, chemchemi ya mapendo yenye huruma kwa waja wake. Waamini wawe na ujasiri wa kumwomba, ili waweze kuwa na moyo wa unyenyekevu na matumaini, daima waoneshe kiu ya uwepo wa Mungu katika maisha yao. Kristo Mfufuka, awe ni chemchemi ya amani na furaha ya kweli mioyoni mwao! Katika shida na magumu ya maisha ni muda muafaka wa kugundua fumbo la sala katika maisha ya mwanadamu kwa sababu Mwenyezi Mungu daima anawasikiliza na kuwajibu waja wake kwa muda muafaka!

Mtakatifu Stanislaus, Askofu na mfiadini (Stanisław Szczepanowski; 26 Julai 1030 – 11 Aprili 1079) alikuwa askofu wa Jimbo kuu la Kraków kuanzia mwaka 1072 akajulikana hasa kwa kuuawa na mfalme wa Polandi Bolesław II. Askofu Stanislaus alitangazwa kuwa mtakatifu na mfiadini na Papa Inocenti IV tarehe 17 Septemba 1253. Kumbu kumbu yake huadhimishwa na Kanisa Katoliki kila mwaka ifikapo tarehe 8 Mei. Baba Mtakatifu Francisko amewakumbusha watu wa Mungu kutoka nchini Poland kwamba Mtakatifu Stanislaus ameacha amana na utajiri mkubwa wa maisha ya kiroho miongoni wa wananchi wa Poland. Ni kiongozi wa Kanisa aliyesimama kidete kulinda, kutangaza na kushuhudia imani yake katika masuala ya kimaadili na kijamii; akajipambanua kwa kuwalinda na kuwatetea maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii! Ni Askofu aliyethubutu kuyamimina maisha yake kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Baba Mtakatifu anawaalika watu wa Mungu nchini Poland kusali kwa ajili ya kuliombea Kanisa na Poland katika ujumla wake, ili kwamba, hata katika Janga la homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, waendelee kupata baraka, amani, ustawi na maendeleo!

Papa: Salam kwa Mahujaji
06 May 2020, 13:47