Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuungana pamoja kumwomba Bikira Maria wa Pompei, ulinzi na tunza yake ya kimama! Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuungana pamoja kumwomba Bikira Maria wa Pompei, ulinzi na tunza yake ya kimama! 

Papa Francisko: Tarehe 8 Mei 2020: Sala kwa B. Maria wa Pompei!

Papa anawaalika waamini Ijumaa tarehe 8 Mei 2020 kushiriki kikamilifu katika Sala kwa Bikira Maria wa Rozari Takatifu. Hiki ni kielelezo cha imani na Ibada kwa Bikira Maria, ili Mama wa Mungu aweze kuliombea Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake, ili uweze kupata huruma na amani. Mwezi Mei, kadiri ya Mapokeo ya Kanisa umetengwa maalum kwa ajili ya Ibada kwa Bikira Maria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Madhabahu ni mahali muafaka pa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Ni mahali pa toba na wongofu wa ndani, unaomwezesha mwamini kuchuchumilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha, kama chachu ya utimilifu na utakatifu. Madhabahu ya Bikira Maria wa Pompei, yaliyoko kwenye Jimbo kuu la Napoli, Kusini mwa Italia ni kitovu cha Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Ibada kwa Bikira Maria imekuwa ni chemchemi na kichocheo kikuu cha waamini kuonesha mshikamano wa upendo na huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake kuhusu Fumbo la Sala, Jumatano tarehe 6 Mei 2020, amewaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, Ijumaa tarehe 8 Mei 2020 kushiriki kikamilifu katika Sala kwa Bikira Maria wa Rozari Takatifu. Hiki ni kielelezo cha imani na Ibada kwa Bikira Maria, ili Mama wa Mungu aweze kuliombea Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake, ili uweze kupata huruma na amani. Waamini wanapaswa kukumbuka kwamba, Mwezi Mei, kadiri ya Mapokeo ya Kanisa umetengwa maalum kwa ajili ya Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kukimbilia chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, kwani atawakirimia ulinzi, tunza na faraja yake ya daima.

Bikira Maria wa Rozari, Pompei, Italia
06 May 2020, 13:32