Vatican News
Jumapili ya Matawi tarehe 5 Aprili 2020 Mama Kanisa anaadhimisha Siku ya XXXV ya Vijana Kimataifa katika ngazi ya Kijimbo: Kauli mbiu: "Kijana, nakuambia: Inuka" Lk. 7:14 Jumapili ya Matawi tarehe 5 Aprili 2020 Mama Kanisa anaadhimisha Siku ya XXXV ya Vijana Kimataifa katika ngazi ya Kijimbo: Kauli mbiu: "Kijana, nakuambia: Inuka" Lk. 7:14  (Vatican Media)

Ujumbe wa Papa Francisko Siku ya XXXV ya Vijana Ulimwenguni, 2020

Ujumbe wa Baba Mtakatifu katika Maadhimisho ya Siku ya XXXV ya Vijana Ulimwenguni katika ngazi ya Kijimbo kwa Mwaka 2020 yanaongozwa na kauli mbiu “Kijana, nakuambia: Inuka.” Lk. 7:14. Siku hii inaadhimishwa Jumapili ya Matawi, tarehe 5 Aprili 2020, mwanzo wa Juma kuu, Mama Kanisa anapotafakari kuhusu: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Kumekucha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka vijana wa kizazi kipya kufanya tafakari ya kina kuhusu: uwezo wa kuona maumivu na kifo; vijana wawe na moyo wa huruma; waoneshe ujasiri wa kujongea mbele na kugusa, vijana wajitanabaishe na yule kijana ambaye alifufuliwa na Kristo Yesu, kwa kuinuka na kuanza kuishi maisha mapya kama watu waliofufuliwa! Ujumbe wa Baba Mtakatifu katika Maadhimisho ya Siku ya XXXV ya Vijana Ulimwenguni katika ngazi ya Kijimbo kwa Mwaka 2020 yanaongozwa na kauli mbiu “Kijana, nakuambia: Inuka.” Lk. 7:14. Siku hii inaadhimishwa Jumapili ya Matawi, tarehe 5 Aprili 2020, mwanzo wa Juma kuu, Mama Kanisa anapotafakari kuhusu: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Baba Mtakatifu anawakumbusha vijana kuhusu Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana iliyofanyika mwezi Oktoba 2018 mjini Vatican, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito.

Maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Ulimwenguni huko Panama kuanzia tarehe 22 - 27 Januari 2019 yaliongozwa na kauli mbiu “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; iwe kwangu kama ulivyosema”. Lk. 1:38. Matukio yote haya ni kipimo cha msingi kwamba, Kanisa linasafiri pamoja na vijana ambayo ni changamoto kutoka kwa Mungu na mwanzo wa maisha mapya Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Maadhimisho ya Siku ya XXXVII ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2022 yatafanyika Jimbo kuu la Lisbon, nchini Ureno kwa kuongozwa na kauli mbiu “Maria aliondoka akaenda kwa haraka” Lk. 1:39. Tafakari ya Mwaka 2021 ni “Inuka usimame. Nimekuweka uwe shahidi wa mambo haya uliyoyaona” (Rej. Mdo. 26:16). Tafakari zote hizi zinaongozwa na kitenzi “Inuka” yaani ufufuko na maisha mapya maneno ambayo yanajitokeza sana katika Wosia wa Kitume mara baada ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana: "Christus vivit" yaani "Kristo anaishi” pamoja na Hati ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana kwa mwaka 2018.

Huu ni mwanga na dira inayoliongoza Kanisa katika mchakato wa safari ya maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya XXXVII ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2022 huko Lisbon. Nyaraka hizi ni muhimu katika maisha na huduma za kichungaji kwa vijana wa kizazi kipya. Baba Mtakatifu anawataka vijana kuinuka ikiwa kama wamepoteza: uhai, ndoto, ari, mtazamo chanya pamoja na ukarimu. Kama ilivyokuwa kwa yule kijana wa Naini, mwana pekee wa mama yake ambaye ni mjane, hata leo hii Kristo Yesu anasimama mbele yako wewe kijana na kwa nguvu zote za ufufuko wake anasema “Kijana, nakuambia: Inuka”. Hiki ni kielelezo cha huruma na upendo wa Kristo Yesu kwa vijana wa kizazi kipya, changamoto na mwaliko kwa vijana kuchukua muda, ili kuweza kutafakari ishara hizi zilizotendwa na Kristo Yesu. Baba Mtakatifu anawataka vijana kujenga uwezo wa kuona maumivu na kifo kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu katikati ya umati mkubwa wa waombolezaji, anamwonea huruma na kumfariji yule mama aliyekuwa na maumivu makali. Uwezo wake wa kuona unazaa matunda, chemchemi ya maisha mapya.

Baba Mtakatifu anawakumbusha vijana kwamba, kunahitajika maneno machache tu, lakini wajitahidi katika maisha yao, kuwa kweli ni mashuhuda wa matukio mbali mbali kwa kuyashiriki kikamilifu katika uhalisia wake, kwa kuzama na kuguswa na mahangaiko ya wahusika badala ya kukimbilia kupiga picha ili kuzirusha kwenye mitandao ya kijamii! Baba Mtakatifu anawataka vijana waguswe ndani ya maisha yao kuhusu uhalisia wa kifo: kimwili, kiroho, kihisia na kijamii ili hatimaye, waweze kuangalia uwezekano wa kupyaisha tena hali hizi. Kuna vijana wengi ambao wamemezwa na malimwengu kiasi hata cha kuweka rehani maisha yao binafsi; wengine ni wafu kwa kukosa matumaini na ujasiri wa kuweza kusimama tena baada ya kuteleza na kuanguka! Kuna vijana wengi wanaosumbuliwa na msongo wa mawazo, kiasi hata cha kutumbukia katika ugonjwa wa sonona na hivyo, kujikatia tamaa ya maisha. Hiki ni chanjo cha vijana wengi kujinyonga. Kuna vijana ambao wametumbukia katika lindi la mateso na majuto na wala hakuna mtu anayesikiliza kilio chao!

Kuna vijana ambao wamekufa kiroho na wameporomoka katika utu na heshima yao kama binadamu, kwa kuzama katika mambo na furaha za mpito! Vijana wengi wamekuwa ni wategemezi wa vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii; kwa kuthamini fedha na vitu, badala ya utu na heshima ya watu wanaowazunguka. Matokeo yake ni vijana kukosa furaha ya kweli katika maisha na hivyo kuanza kuchoka na maisha hali inayopelekea utupu na kujikatia tamaa. Mazingira pia yamepelekea vijana wengi kutoweza kunafsisha ndoto za maisha yao na hivyo kujisikia wafu. Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha vijana kwamba, kushindwa katika jambo fulani si mwisho wa maisha. Vijana wanakumbana na mazingira ya kifo cha kimwili na kimaadili kwa kujitumbukiza katika: ulevi wa kupindukia, maovu pamoja na umaskini wa hali na kipato. Hata leo hii, bado vijana kama hawa wanayo jeuri ya kuweza kuinuka tena na kupyaisha maisha yao. Vijana wanaweza kusaidiana na kuokoana, ili kuondokana na hali na mazingira kama haya!

Baba Mtakatifu anawataka vijana kujenga moyo wa huruma, kwa kuguswa na maumivu, mateso na mahangaiko ya jirani zao, kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu, wawe tayari kushiriki majonzi na vifo vya wengine. Vijana wawe ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya ukarimu, wasimame kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Wasikilize na kujibu kilio cha Dunia Mama na Maskini wanaowazunguka, wawe tayari kusafisha machozi ya wale wanaoteseka, kama kielelezo cha: huruma, upendo na mshikamano unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu anayewapenda upeo na kuwakomboa kwa njia ya Kristo Yesu anayewatumia vijana kama vyombo vya ukombozi!  Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya Vijana Ulimwenguni kwa ngazi ya Kijimbo anawataka vijana kuwa na ujasiri wa kujongea mbele, ishara ya kinabii, kwa kuonesha ukaribu wao kwa wale wanaoteseka, ili kuweza kuwarejeshea tena maisha, Mguso wa Kkristo Yesu anayeishi ni mguso unaomimina Roho Mtakatifu kwa maiti ya kijana na kumfanya hai tena! Mguso huu una penya katika undani wa maisha ya mtu na kuponya majeraha kwa njia ya upendo, uhuru kamili na utimilifu wa maisha mapya. Uwepo wa vijana katika mahangaiko ya jirani zao inaweza kuwa ni ishara ya kuamsha nguvu za ufufuko.

Vijana waguswe kwanza na upendo wa Kristo Yesu ili waweze kuwa tayari kuwahudumia ndugu zao wanaokumbana na baa la njaa, magonjwa na kiu, walio uchi pamoja na kuwatembelea walioko kifungoni. Vijana wasaidie kupyaisha maisha yale waliokufa kutoka ndani mwao, wale wanaoteseka na kupoteza imani, matumaini na mapendo. Vijana wanapaswa kujitanabainisha na yule kijana aliyefufuliwa na Kristo Yesu. Watambue kwamba, kama Wakristo wanaanguka na wapaswa kusimama tena na kuendelea na safari, kwa kukita imani yao kwa Mwenyezi Mungu, kwa kukubali kupokea maisha mapya yanayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu. Haya ni maisha yenye maana na hadhi yake: kielelezo cha uumbaji na maisha mapya. Vijana wanapaswa kujiamini kwa kutambua nguvu zao za ndani zinazobubujika kutoka kwa Kristo Yesu anayeweza kuwafafua na kupyaisha tena maisha yao! Kwa wale walioguswa na kufufuliwa na Kristo Yesu, wanapaswa kuishi maisha kama ya watu waliofufuliwa, kwa kushuhudia matendo makuu ya Mungu katika maisha yao. Kuonesha haiba, matamanio yao halali, mahitaji na ndoto zao, ilikiwa kama hawakueleweka siku za nyuma kwani kwa sasa kuna watu wanaoweza kuwaelewa barabara.

Vijana wajitahidi kujenga uhusiano, mafungamano na umoja na vijana wengine. Leo hii njia mbali mbali za mawasiliano na mitandao ya kijamii ina uwezo wa kuwaunganisha watu sehemu mbali mbali za dunia lakini bila kuwajengea umoja na mshikamano wa dhati. Haya ni mahusiano yanayoelea katika ombwe! Watu wanaunganika lakini, hawana mawasiliano. Huu ni wakati wa kuinuka! Kutumia njia za mawasiliano na mitandao ya kijamii kama nyenzo na wala si ukomo. Inuka ni mwaliko wa kufanya maamuzi magumu katika maisha, ilikuwa ni chachu ya mageuzi, ili kupyaisha tena matumaini na matamanio ya vijana wa kizazi kipya katika ulimwengu mamboleo. Ni mwaliko kwa vijana kuondokana na uchovu ili kupyaisha nyuso zao, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya vijana wenzao ambao wako tayari kupokea zawadi hii. Vijana wanahimizwa kuinuka kutoka kwa wafu, ili waweze kuwa ni mashuhuda wa Kristo Yesu, tayari kujisadaka kwa ajili ya jirani zao.

Baba Mtakatifu Francisko mwishoni mwa ujumbe wake, katika Maadhimisho ya Siku ya XXXV ya Vijana Ulimwenguni katika ngazi ya Kijimbo kwa Mwaka 2020 yanaongozwa na kauli mbiu: “Kijana, nakuambia: Inuka” Lk. 7:14, anawataka vijana kuyapatia matamanio na ndoto zao uhuru wa kutawala ili hatimaye, kuleta mabadiliko katika ulimwengu wa roho, sanaa na jamii katika ujumla wake. Ni wakati wa vijana kupaaza sauti zao ili ziweze kusikika. Kwa njia ya Bikira Maria, vijana wawe na jeuri ya kuweza kuona taswira ya Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa, tayari kuwakabidhi na kuwaweka vijana wote ulimwenguni chini ya ulinzi na tunza yake ya kimama! Kwa njia yake, Kanisa linatambua kwamba, linataka kuwakaribisha vijana wote bila ubaguzi ili kuwaonjesha upendo. Kanisa litaendelea daima kuwa ni Mama kwa watoto wafu, likilia na kuomboleza kwa ajili yao, ili waweze kurejeshewa uhai kwa watoto wake waliokufa. Kanisa linakufa kati ya watoto wake waliokufa. Linainuka kati ya watoto wake wanaoinuka.

Papa: Ujumbe Siku ya Vijana 2020

 

 

02 April 2020, 12:55