Baba Mtakatifu Francisko amemtumia salam na matashi mema Rabbi Riccardo Di Segni kwa ajili ya Maadhimisho ya Sherehe ya Pasaka ya Wayahudi kwa mwaka 2020. Baba Mtakatifu Francisko amemtumia salam na matashi mema Rabbi Riccardo Di Segni kwa ajili ya Maadhimisho ya Sherehe ya Pasaka ya Wayahudi kwa mwaka 2020. 

Papa Francisko: Salamu za Pasaka kwa Jumuiya ya Wayahudi Roma

Papa Francisko amemtumia salam za Pasaka Rabbi Riccardo Di Segni, akimwalika kuendelea kupyaisha mahusiano ya urafiki pamoja na huduma ya upendo kwa watu wa Mungu. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, familia ya Mungu inapitia kipindi kigumu sana, kutokana na maambukizi makubwa ya Virusi vya Corona vinavyoendelea kusababisha majanga makubwa kwa watu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Pasaka ni ni Sherehe ya upendo, huruma na msamaha wa Baba wa milele ambao umening’inizwa kwenye mti wa Msalaba! Katika kipindi hiki cha Maadhimisho ya Sherehe ya Pasaka, Baba Mtakatifu Francisko amemtumia salam na matashi mema Rabbi Riccardo Di Segni, Mkuu wa Jumuiya ya Wayahudi mjini Roma, akimwalika kuendelea kupyaisha mahusiano ya urafiki pamoja na huduma ya upendo kwa watu wa Mungu, lakini zaidi kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.  Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, familia ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia inapitia kipindi kigumu sana, kutokana na maambukizi makubwa ya Virusi vya Corona, COVID-19 vinavyoendelea kupukutisha maisha ya watu pamoja na kusababisha majanga makubwa.

Wayahudi kwa upande wao, wanaadhimisha Sherehe ya Pasaka, inayojulikana kwa Kiebrania kama “Pesach”, “Passover”, yaani "kupita juu", ni Sherehe kubwa kwa Wayahudi kwani wanakumba siku ile Malaika wa Bwana alipopita juu ya nyumba za Waisraeli akawapiga wazaliwa wa kwanza wa Wamisri ili kuwakomboa Waisraeli kutoka utumwani Misri na kuwapeleka kwenye Nchi ya Ahadi! Baba Mtakatifu amemhakikishia Rabbi Riccardo Di Segni, sala na sadaka yake na kumwomba hata yeye kumkumbuka katika maisha na utume wake.

Kwa upande wake, Rabbi Riccardo Di Segni, anasema, maadhimisho ya Pasaka kwa Mwaka 2020 yanamwelekeo tofauti kabisa, kwani maisha ya kawaida yamevurigwa na maambukizi ya homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Janga hili linaendelea kusababisha watu wengi kupoteza maisha; wengi wao kuendelea kuishi kwa hofu na taharuki kubwa na kwamba, madhara yake ni makubwa katika masuala ya kiuchumi na kijamii. Jumuiya ya Wayahudi mjini Roma, kama walivyo watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia inaendelea kujifunga kibwebwe katika huduma ya upendo kwa waathirika wa Virusi vya Corona, COVID-19. Wanaendeleza mchakato wa kuwafariji waathirika, kuhimiza umuhimu wa kuchunguza dhamiri na hatimaye, kusali ili kuomba huruma na msaada kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Katika muktadha huu, waamini wa dini mbali mbali duniani, wamejikuta wakitambua na kushirikishana tunu msingi za maisha ya kiroho, kwa kuonesha umuhimu wa kushirikiana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Rabbi Riccardo Di Segni, Mkuu wa Jumuiya ya Wayahudi mjini Roma, anasema, licha ya maafa na changamoto kubwa inayotolewa kutokana na maambukizi makubwa ya homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vy Corona, lakini Sherehe ya Pasaka inapaswa kuendelea kuadhimishwa kwa amani na utulivu, ili iweze kuwa ni chachu ya upyaisho na ujio wa ulimwengu mpya!

Papa: Jumuiya ya Wayahudi Roma

 

15 April 2020, 11:33