Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kupambana na virusi vya corona kwa imani, matumaini na mapendo sanjari na uwajibikaji mkubwa! Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kupambana na virusi vya corona kwa imani, matumaini na mapendo sanjari na uwajibikaji mkubwa! 

Papa Francisko: Virusi vya Corona, COVID-19: Mshikamano wa imani, matumaini na mapendo!

. Baba Mtakatifu anawapongeza wafanyakazi wote katika sekta ya afya wanaowahudumia wagonjwa, viongozi wa serikali na wale wote wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza, ili kuhakikisha kwamba wanadhibiti kikamilifu kuenea kwa ugonjwa huu ambao unaendelea kusababisha madhara makubwa katika medani mbali mbali za maisha. Imani, matumaini na mapendo ni silaha kubwa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii anasema, anapenda kuonesha tena mshikamano wa dhati na uwepo wa karibu kwa wagonjwa na waathirika wa Virusi vya Corona, COVID-19 ambavyo kwa sasa vimekuwa ni tishio la usalama wa maisha ya watu wengi sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu anawapongeza wafanyakazi wote katika sekta ya afya wanaowahudumia wagonjwa, viongozi wa serikali na wale wote wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza, ili kuhakikisha kwamba wanadhibiti kikamilifu kuenea kwa ugonjwa huu ambao unaendelea kusababisha madhara makubwa katika medani mbali mbali za maisha. Mapambano haya yanapaswa kukita mizizi yake katika: imani, matumaini na mapendo ya dhati kwa waathirika.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Kwaresima ni kipindi kilichokubalika kwa waamini kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya wagonjwa ambao wanashindwa kupata huduma na msaada kutokana na sababu mbali mbali. Huu ni wakati uliokubalika wa kumwilisha huruma na upendo kama ushuhuda wa mshikamano, kielelezo makini cha imani tendaji! Wakati huo huo, Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha, katika ujumbe wake wa upendo na mshikamano linakazia kwamba, maisha ya binadamu yana thamani kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu. Hata pale mwanadamu anapoguswa na kutikiswa na magonjwa mbali mbali, anapaswa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu yuko pamoja naye!

Katika kipindi hiki kigumu, Baraza hili la Kipapa linapenda kuonesha mshikamano wa dhati na waathirika wote wa Virusi vya Corona, COVID-19 kwa njia ya uwepo wake wa sala na huduma. Linaendelea kuwatia moyo wadau mbali mbali kushikamana ili kwamba, tiba na kinga dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19 iweze kupatikana haraka. Wale wote waliopewa karama mbali mbali na Mwenyezi Mungu wazitumie kikamilifu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wote wa Mungu. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wakabiliane na changamoto hii: kikamilifu katika hali ya utulivu na ujasiri mkuu na pale inapotakiwa, watu watoe sadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Watu wengi wanaonekana kukata tamaa, lakini wanakumbushwa kwamba, bado Mwenyezi Mungu anawapenda, anawalinda na kuwatunza. Mama Kanisa anapenda kuwahakikishia waathirika wote uwepo wake wa karibu kama Mama mpendelevu.

Familia kama Kanisa dogo la nyumbani, zinahamasishwa kwa namna ya pekee kuwahudumia watu wake kwa moyo wa huruma na upendo; kwa kuwajibika barabara pamoja na kuwasindikiza wale wote walioathirika. Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha linaendelea kuwahimiza watu wote kuhakikisha kwamba, wanazingatia kikamilifu itifaki ya mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Watu waoneshe upendo na mshikamano na familia ambazo zinaogelea katika umaskini kwa kukosa mahitaji msingi. Uwajibikaji, moyo wa upendo na mshikamano, nguvu, busara na hekima ni muhimu sana katika kupambana na ugonjwa huu wa Homa ya Virusi vya Corona, COVID-19.

Papa: Virusi vya Corona

 

07 March 2020, 16:10