Nia za Baba Mtakatifu Francisko kwa Mwezi Machi 2020: Uaminifu kwa Injili pamoja na kukoleza mchakato wa umoja na mshikamano! Nia za Baba Mtakatifu Francisko kwa Mwezi Machi 2020: Uaminifu kwa Injili pamoja na kukoleza mchakato wa umoja na mshikamano! 

Nia za Baba Mtakatifu Mwezi Machi 2020: Umoja wa Wakristo China!

Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa Mwezi Machi 2020 zinazosambazwa kwa njia ya video na Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa, anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuliombea Kanisa nchini China, ili liweze kudumisha uaminifu wake kwa Injili pamoja na kukoleza mchakato wa umoja na mshikamano kwa ajili ya ustawi wa Kanisa la Kristo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwahamasisha Wakristo nchini China ili kweli waweze kuwa ni vyombo na wajenzi wa umoja na upatanisho; ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu! Waendeleze mchakato wa utamadunisho pamoja na kuwekeza tunu msingi za kiinjili, kiutu na kimaadili kwa vijana wa kizazi kipya kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Baba Mtakatifu katika nia zake za jumla kwa Mwezi Machi 2020 zinazosambazwa kwa njia ya video na Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa, anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuliombea Kanisa nchini China, ili liweze kudumisha uaminifu wake kwa Injili pamoja na kukoleza mchakato wa umoja na mshikamano. Ujumbe huu unaweza kupatikana hata kwa lugha ya Kiswahili katika anuani ifuatayo: www.thepopevideo.org. Jumuiya za Kikatoliki nchini China ndio walengwa wakuu wa ujumbe huu wa Baba Mtakatifu. Kila kukicha, Kanisa Katoliki nchini China linaendelea kusonga mbele kwa imani na matumaini makubwa.

Mama Kanisa anataka kuona kwamba, Wakristo nchini China, wanakuwa kweli ni Wakristo na raia wema, mfano bora wa kuigwa mintarafu mwanga wa tunu msingi za Kiinjili. Wakristo nchini China, wanapaswa kujifunga kibwebwe ili kuhakikisha kwamba wanatangaza na kushuhudia Injili, bila kulazimisha wongofu wa shuruti. Sanjari na hili, Wakristo wa Kanisa Katoliki wanapaswa kuonesha umoja na mshikamano. Itakumbukwa kwamba, Jumuiya za kwanza kabisa za Wakristo nchini China zilianza kujitokeza kunako karne ya 6, wakati Wakristo Wamonaki kutoka Siria walipopandikiza imani ya Kanisa la Mashariki (Wanestoriani). Mwishoni mwa Karne ya 16 Wamisionari kutoka Shirika la Wayesuit, wakawasili, lakini mchakato wa uinjilishaji uliendelea kusuasua hadi kunako Karne ya 20, idadi ya Wakristo ilipo ongezeka kwa kiwango kikubwa.

Takwimu zisizo rasmi zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya Wakristo milioni mia moja, sawa na asilimia 7.1% ya idadi ya wananchi wote wa China inayosaidikiwa kufikia bilioni moja na milioni mia nne. Idadi ya Wakristo nchini China inaweza kuongezeka maradufu na hivyo kuiwezesha China kuwa na idadi kubwa zaidi ya Jumuiya za Kikristo duniani. Baba Mtakatifu anasema, anaipenda sana familia ya Mungu nchini China ni hamu ya moyo wake, iko siku kwamba atakwenda kutembelea China. Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwepo na uhusiano mzuri kati ya Vatican na China. Wakatoliki waliokuwa wanaishi ufichoni na wale waliokubaliwa na Serikali, sasa wanaishi kwa umoja na upendo kama ndugu wamoja.

Baadhi ya Maaskofu kutoka China wamekwisha kutembelea Vatican. Kuna ushirikiano wa utamaduni unaoendelea kwa sasa kati ya China na Vatican. Vatican imekubali mwaliko wa Serikali ya China wa kushiriki katika “Expo Bejing 2019” yaani “Onesho la Kilimo cha Maua na Utunzaji Bora wa mazingira” na lililo ongozwa na kauli mbiu “Ishi kijani, Ishi vizuri zaidi”. Katika hali na mazingira kama haya, upinzani ni jambo la kawaida, lakini hali hii ni kwa ajili ya watu wachache sana. Wakatoliki nchini China kunako mwaka 2019 wameadhimisha kwa mara ya kwanza Fumbo la Pasaka kwa pamoja bila matatizo. Baba Mtakatifu anasema, Kanisa lina dhamana na wajibu mkubwa wa kuwasindikiza Wakristo nchini China kwa njia ya sala, udugu wa kibinadamu na urafiki katika Kristo Yesu. Wakristo nchini China wanapaswa kujisikia katika hija ya maisha yao ya imani, wakati huu malango mbali mbali ya matumaini yanapoendelea kufunguka, watambue kwamba, kuna ndugu zao katika Kristo wanaowasindika, kwani hata wao ni sehemu hai ya maisha na utume wa Kanisa.

Ni za Papa Machi 2020
10 March 2020, 10:51