Papa Francisko tarehe 26 Novemba 2019 ametembelea na kuzungumza na wanajumuiya wa Chuo Kikuu Cha Kikatoliki cha Sophia na kufafanua dhamana ya vyuo vikuu katika maisha na utume wa Kanisa. Papa Francisko tarehe 26 Novemba 2019 ametembelea na kuzungumza na wanajumuiya wa Chuo Kikuu Cha Kikatoliki cha Sophia na kufafanua dhamana ya vyuo vikuu katika maisha na utume wa Kanisa. 

Hija ya Papa Francisko Japan: Utume wa Kanisa kwa vyuo vikuu

Chuo Kikuu cha Sophia kinapaswa kuwa ni mahali pa majiundo makini ya akili na sehemu ya kuwajengea wanafunzi matumaini. Chuo hiki kiwasaidie wanafunzi kupata mawazo mapana zaidi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya mwanadamu pamoja na kuwa na matumizi sahihi ya teknolojia, kwa kuzingatia utu, heshima na haki msingi za binadamu. Utu wa kweli unajikita katika usanisi mpya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kuanzia tarehe 23 hadi 26 Novemba 2019,  Baba Mtakatifu Francisko amekuwa akifanya hija ya kitume nchini Japan ambayo imeongozwa na kauli mbiu “Linda Maisha Yote”. Pamoja na mambo mengine, Baba Mtakatifu ametangaza kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini, haki na amani. Baba Mtakatifu amepata nafasi ya kutembelea Hiroshima na Nagasaki kama alivyofanya Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1981. Amekutana na kuzungumza na waathirika wa tetemeko la ardhi na Tsunami iliyoleta madhara makubwa katika mtambo wa Nyuklia wa Fukushima na vitongoji vyake kunako mwaka 2011. Ujumbe wa Baba Mtakatifu mjini Nagasaki umekuwa wazi kabisa, yaani matumizi ya nishati ya atomiki kwa ajili ya vita ni vitendo ambavyo vinakwenda kinyume kabisa cha kanuni maadili na utu wema. Baraza la Maaskofu Katoliki Japan linasema, maisha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, yanayopaswa kulindwa, kutunzwa na kuendelezwa.

Maandiko Matakatifu yanabainisha kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye aliyeumba dunia na kuifanya, ndiye aliyeifanya imara, hakuimba ukiwa, aliiumba ili ikaliwe na watu. Ili kulinda utu, heshima na haki msingi za binadamu kuna haja wanasema Maaskofu kusimama kidete kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira nyumba ya wote. Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne, tarehe 26 Novemba 2019 amekutana na kuzungumza na Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Sophia kilichoko jijini Tokyo, nchini Japan. Lakini kabla ya mazungumzo yake, amepata nafasi kwanza kabisa kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu na Wayesuit wanaoishi nchini Japan, akapata nao kifungua kinywa na baadaye, akawatembelea na kuwasaliami mapadre wazee na wagonjwa ambao wamesadaka maisha yao ili kuwarithisha vijana wa kizazi kipya stadi za maisha, ujuzi na maarifa ya kuweza kupambana na mazingira yao, ili hatimaye, ulimwengu uweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Baba Mtakatifu katika hotuba yake amegusia kuhusu: Mchango wa Kanisa Katoliki nchini Japan; umuhimu wa kutumia hekima katika utunzaji bora wa mazingira, Utambulisho wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Sophia pamoja na Mpango mkakati  wa Wayesuit katika maisha na utume wa vijana kuanzia mwaka 2019-2029. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, hija yake ya kitume nchini Japan hata kama imekuwa ni kwa muda mfupi, anapenda kumshukuru Mungu aliyemwezesha kutembelea Japan, nchi ambayo Mtakatifu Francisko Xavier alitamani sana kuitembelea na imekuwa kweli ni chemchemi ya mashuhuda wa imani ya Kikristo. Kanisa Katoliki linaheshimiwa na kuthaminiwa sana nchini Japan na ni matumaini yake kwamba, ushirikiano huu utadumishwa hata kwa siku za mbeleni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Japan. Hii ni Jamii inayotaka kujenga na kujielekeza zaidi katika ukuaji wa kiuchumi, kwa kuunda mazingira bora zaidi; jamii inayosimikwa katika upendo na huruma.

Masomo na tafakari ni sehemu ya utambulisho wa watu wa Mungu nchini Japan, mambo ambayo ni sehemu ya utambulisho wake wa kitamaduni. Chuo kikuu kinapaswa pia kuwa ni mahali pa kuwafunda viongozi wa siku za usoni, ili waweze kujizatiti katika kulinda na kudumisha maisha, kwa kuwa na mawazo shirikishi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya jamii. Katika ulimwengu wa utandawazi na mashindano makubwa, Chuo Kikuu cha Sophia kinapaswa kuwa ni mahali pa majiundo makini ya akili na sehemu ambayo itawawezesha wanafunzi kuwa na matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Chuo hiki kiwasaidie wanafunzi kupata mawazo mapana zaidi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya mwanadamu pamoja na kuwa na matumizi sahihi ya teknolojia, kwa kuzingatia utu, heshima na haki msingi za binadamu. Utu wa kweli unajikita katika usanisi mpya. Chuo Kikuu cha Sophia kimekuwa kikijitambulisha na kujipambanua kuwa ni mahali pa ujenzi wa tunu msingi za kiutu, kikristo na kimataifa kwa kuwa na majaalimu kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Wamo hata wale wanaotoka katika nchi zile ambazo wakati fulani zilikuwa zinapambana na Japan kivita, lakini kwa sasa zimejiunga kwa pamoja ili kutoa mambo mazuri zaidi kwa ajili ya malezi na majiundo ya vijana wa Japan, ari na moyo unaopaswa kudumishwa ndani na nje ya Japan. Maendeleo ya sayansi na teknolojia yasaidie kutoa huduma makini kwa binadamu, ili kujenga jamii inayosimikwa katika haki na ellimu ya ekolojia inayowajibika barabara. Ushirikiano na mafungamano kati ya majaalimu na wanafunzi, uchochee tafakari na mang’amuzi ya dhati ili kuwawezesha wanafunzi wanaohitumu masomo yao chuoni hapo kuweza kuchagua, kuwajibika na kufuata dhamiri zao nyofu, tayari kuwajibika katika matendo yao. Wanafunzi wanaohitimu chuoni hapo watambulikane kwa uadilifu wao unaofumbatwa katika maneno adili.

Baba Mtakatifu amegusia kuhusu Mpango Mkakati wa Wayesuit katika Kipindi cha Miaka kumi yaani kuanzia mwaka 2019-2029, unaotoa kipaumbele cha pekee kwa vijana wa kizazi kipya, mambo yaliyopembuliwa na Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana kwa mwaka 2018 pamoja na nyaraka zake mbali mbali. Kanisa linapenda kutoa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wake miongoni mwa vijana wa kizazi kipya. Taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu viwe ni mahali pa kuwapatia vijana elimu pamoja na kuwajengea mwono mpana na matumaini kwa siku za mbeleni. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, taasisi za elimu ya juu pamoja na vyuo vikuu vya Kikatoliki vitaendelea kujipambanua kwa kuwa ni mtindo unaowashirikisha  na kuwatajirisha vijana katika medani mbali mbali za maisha.

Chuo Kikuu cha Sophia kinapaswa kuwa ni chombo cha ushuhuda na mashikamano wa pekee na maskini, kwa kusaidia kujenga na kudumisha mazingira yatakayounganisha kweli mbali mbali za maisha; kwa kuwaunganisha watu na kupunguza wigo mkubwa unaoweza kuwatenganisha. Hata maskini wanayo haki ya kupata elimu bora na wala isiwe ni upendeleo kwa watu wachache katika jamii. Elimu iwe ni huduma kwa ajili ya kudumisha haki, ustawi na mafao ya wengi, huduma ambayo inapaswa kutekelezwa na kila mmoja wao kadiri ya wito na nafasi yake. Haya ndiyo mambo makuu ambayo Baba Mtakatifu amependa kuwaachia wanajumuiya wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Sophia kilichoko Jijini Tokyo, nchini Japan kama ushauri wake, ili hekima hii iweze kuwa ni chemchemi ya furaha na matumaini kwa jamii mamboleo. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwashukuru watu wote wa Mungu nchini Japan kwa ukarimu wao!

Papa: Elimu Makini
26 November 2019, 15:49