Wito wa Baba Mtakatifu Francisko: Lebanon sikilizeni na kujibu kilio cha vijana wa kizazi kipya wanaotaka kuona leo na kesho iliyo bora zaidi katika maisha yao! Wito wa Baba Mtakatifu Francisko: Lebanon sikilizeni na kujibu kilio cha vijana wa kizazi kipya wanaotaka kuona leo na kesho iliyo bora zaidi katika maisha yao! 

Papa Francisko: Lebanon sikilizeni na kujibu kilio cha vijana!

Papa anamwomba Bikira Maria aweze kuiombea nchi hii, ili kwa njia ya mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa, Lebanon iweze kuendelea kuwa ni mahali pazuri pa watu wa Mungu kuishi kwa amani na utulivu; kwa kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi na uhuru wa kila raia; kwa ajili ya ustawi na maendeleo huko Mashariki ya Kati, eneo ambalo watu wake wanateseka sana!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya tafakari ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 27 Oktoba 2019, aliyaelekeza mawazo na sala zake nchini Lebanon, lakini kwa namna ya pekee kwa vijana. Katika siku za hivi karibuni, vijana wa kizazi kipya nchini Lebanon wamefanya maandamano makubwa nchini humo, wakitaka kilio na sauti yao iweze kusikilizwa na kupatiwa majibu muafaka kama sehemu ya mustakabali wa maisha yao kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Vijana wanakumbana na changamoto pamoja na matatizo ya kijamii, kimaadili na kiuchumi nchini Lebanon. Baba Mtakatifu anawaalika wadau wote, kuhakikisha kwamba, wanatafuta suluhu ya haki kwa njia ya majadiliano yanayofumbatwa katika ukweli na uwazi; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Anamwomba Bikira Maria, Malkia wa Lebanon, aweze kuiombea nchi hii, ili kwa njia ya mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa, Lebanon iweze kuendelea kuwa ni mahali pazuri zaidi pa watu wa Mungu kuishi kwa amani na utulivu; kwa kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi na uhuru wa kila raia; kwa ajili ya ustawi na maendeleo huko Mashariki ya Kati, eneo ambalo watu wake wanateseka sana!

Baba Mtakatifu Francisko amekumbusha kwamba, Mwezi Oktoba 2019, umetengwa maalum na Mama Kanisa kwa ajili ya kuhamasisha ari na mwamko wa kimisionari duniani, kwa mwaka huu 2019, Kanisa linaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu Papa Benedikto XV alipochapisha Waraka wa Kitume "Maximum Illud" yaani “Kuhusu Shughuli za Kimisionari.” Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019 unaongozwa na kauli mbiu “Mmebatizwa na kutumwa: Kanisa la Kristo katika utume”. Kanisa linataka kuendeleza utume wake wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, agizo kutoka kwa Kristo Yesu mwenyewe kwa wafuasi wake. Maadhimisho haya ambayo kwa sasa yanafikia kilele chake umekuwa ni muda wa: sala, katekesi, tafakari na matendo ya huruma! Itakumbukwa kwamba, Mwezi Oktoba, ni mwezi wa Rozari Takatifu: muhtasari wa huruma ya Mungu katika hija ya maisha ya mwanadamu hapa ulimwenguni.

Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwaombea wamisionari sehemu mbali mbali za dunia, wanaokumbana na matatizo pamoja na changamoto katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Waamini wanahimizwa kuendelea kusali Rozari Takatifu. Ikumbukwe kwamba, Injili na Amani ni sawa na chanda na pete, vinatembea kwa pamoja!

Papa: Lebanon
27 October 2019, 11:56