Vatican News
Papa Francisko: Uinjilishaji unafumbatwa katika: Kutangaza Neno la Mungu; Huduma kwa maskini pamoja na ushuhuda amini kwa Kristo na Kanisa lake kama walivyofanya mashuhuda wa imani. Papa Francisko: Uinjilishaji unafumbatwa katika: Kutangaza Neno la Mungu; Huduma kwa maskini pamoja na ushuhuda amini kwa Kristo na Kanisa lake kama walivyofanya mashuhuda wa imani.  (Vatican Media)

Papa Francisko: Uinjilishaji: Huduma kwa maskini na ushuhuda

Tangu mwanzo wa maisha na utume wake, Mama Kanisa ameendelea kujikita katika mchakato wa uinjilishaji kwa njia ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii sanjari na ushuhuda wa uaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Huu ni mwaliko wa kumwilisha tunu hizi msingi katika uhalisia wa maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kupembua kwa kina na mapana kuhusu utangazaji wa Injili, huduma ya upendo na ushuhuda kwa Kristo Yesu na Kanisa wakati wa Katekesi yake, Jumatano, tarehe 25 Septemba 2019, alitambua uwepo wa mahujaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia, baadhi yao ni wale waliotoka nchini Kenya. Kwa namna ya pekee, ametambua uwepo wa wajumbe wa Familia ya Kikarmeli wanaoshiriki katika semina ya kimataifa kwa mwaka 2019 hapa mjini Roma. Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu anasema, tarehe 27 Septemba 2019, Mama Kanisa ataadhimisha Kumbu kumbu ya Mtakatifu Vincent wa Paulo, Baba wa maskini; mlezi na msimamizi wa Mashirika na vyama vya kitume vinavyojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo kati ya watu maskini. Mfano wa maisha na utume wake, uwe ni kikolezo cha kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini; tayari kuwasaidia kukuza ndani mwao moyo wa ukarimu, tayari kupokea na kuendeleza zawadi ya maisha.

Tangu mwanzo wa maisha na utume wake, Mama Kanisa ameendelea kujikita katika mchakato wa uinjilishaji kwa njia ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii sanjari na ushuhuda wa uaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kumwilisha tunu hizi msingi katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku. Baba Mtakatifu amechukua fursa hii kuwakaribisha Majandokasisi wapya waliowasili hivi karibuni mjini Roma kwa ajili ya kuanza masomo na majiundo yao ya Kikasisi. Huduma ya upendo kwa Mungu na jirani ni jambo la kupewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Kanisa, kielelezo cha unyenyekevu. Kwa njia hii, inawezekana kwa watu kuondokana na tabia ya kutaka kutumia nguvu kwa kila jambo na kuanza kujielekeza katika uvumilivu na amani. Mtakatifu Stefano, Shahidi awe ni mfano bora wa kuigwa katika: imani, upendo na ushuhuda amini wa Sura ya Kristo Yesu.

Papa: Mashuhuda wa Imani

 

25 September 2019, 17:08