Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko amewatumia watu wa Mungu nchini Mauritius ujumbe wa shukrani na matashi mema na anatarajia kukutana nao ili kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo! Baba Mtakatifu Francisko amewatumia watu wa Mungu nchini Mauritius ujumbe wa shukrani na matashi mema na anatarajia kukutana nao ili kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo! 

Hija ya Papa Francisko Mauritius: Ujumbe wa shukrani! Hadi raha!

Lugha ya Injili ni upendo. Papa Francisko anamwomba Mwenyezi Mungu aweze kumkirimia nguvu za Roho Mtakatifu ili kuwatangazia na kuwashuhudia Injili, ili wote waweze kuifahamu na kuipokea kwa moyo mkunjufu! Anawaomba watu wa Mungu kuongeza bidii ya sala, kwani yeye tayari amekwisha wameba na mbereko ya sala katika sakafu ya moyo wake na anaendelea kusali kwa ajili yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anawaomba waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumsindikiza kwa sala na sadaka zao, ili hija yake Barani Afrika iweze kuzaa matunda yanayokusudiwa yaani: amani na upatanisho wa kidugu; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote,  sanjari na ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Barani Afrika. Kauli mbiu inayoongoza hija ya Baba Mtakatifu nchini Msumbiji ni: matumaini, amani na upatanisho. Kwa upande wa Madagascar, ni “Mpanzi wa amani na matumaini na kauli mbiu ya familia ya Mungu nchini Mauritius ni “Hujaji wa amani”.

Baba Mtakatifu Francisko kuanzia Jumatatu tarehe 9 hadi Jumanne, tarehe 10 Septemba, 2019 anatarajiwa kuwa nchini Mauritius. Anasema, hija hii ya kitume, itamwezesha kutembelea Kisiwa cha Mauritius! Akiwa mjini Roma, anapenda kuwapatia salam na shukrani kubwa kwani anatambua kwamba, kwa kipindi kirefu wamekuwa wakijisadaka kwa ajili ya maandalizi ya hija hii ya kitume. Baba Mtakatifu anasema, itakuwa kwake furaha kubwa isiyokuwa na kifani kutangaza na kushuhudia Injili kati ya watu wa Mungu nchini humo. Hawa ni watu kutoka katika makabila mbali mbali, amana na utajiri mkubwa unaofumbatwa katika mapokeo, tamaduni na imani mbali mbali.

Tangu mwanzo na kwa asili yake, Kanisa Katoliki limetumwa kwa watu wote na linazungumza lugha zote za ulimwengu huu. Lakini, ikumbukwe kwamba, luga ya Injili ni upendo. Kwa njia ya maombezi ya Bikira Maria, anamwomba Mwenyezi Mungu aweze kumkirimia nguvu za Roho Mtakatifu ili kuwatangazia na kuwashuhudia Injili, wote waweze kuifahamu na kuipokea kwa moyo mkunjufu! Mwishoni mwa ujumbe wake kwa njia ya video, anawaomba watu wa Mungu nchini Mauritius kuongeza bidii ya sala, kwani yeye tayari amekwisha wameba na mbereko ya sala katika sakafu ya moyo wake na anaendelea kusali kwa ajili yao!

Papa: Mauritius

 

03 September 2019, 15:48