Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko awataka waamini kuzingatia masharti yaliyotolewa na Kristo Yesu katika mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko awataka waamini kuzingatia masharti yaliyotolewa na Kristo Yesu katika mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu.  (Vatican Media)

Hija ya Papa Francisko nchini Madagascar: Masharti ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani

Papa Francisko amekazia umuhimu wa kuangalia mahusiano na mafungamano ya kifamilia; Ujenzi wa ufalme wa Mungu kadiri ya mapenzi ya Mungu na mwishoni ni jinsi ya kushirikishana maisha mapya yanayobubujika kutoka kwa Kristo, ili kweli Mwenyezi Mungu aweze kuwa ni kiini na mwongozo wa maisha ya waja wake. Umuhimu wa kufuata masharti ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Madagascar, Jumapili tarehe 8 Septemba 2019 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kadiri ya Kalenda ya Liturujia ya Kanisa, yaani, Jumapili ya XXIII ya Mwaka C wa Kanisa. Ibada hii imehudhuriwa na umati mkubwa wa watu wa Mungu kutoka Madagascar, waliopamba ibada kwa rangi mbali mbali, nyimbo na utamadunisho wa amana na utajiri wa watu wa Mungu kutoka Madagascar. Vijana wengi waliohudhuria mkesha na Baba Mtakatifu, wamelala na kuamkia kwenye uwanja wa michezo wa Soamandrakizay unaomilikiwa na Jimbo kuu la Antananarivo. Baba Mtakatifu amewapongeza kwa uwajibikaji wao, ambao unakaziwa sana na Mwinjili Luka.

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake, amesisitizia: umuhimu wa kuangalia mahusiano na mafungamano ya kifamilia; Ujenzi wa ufalme wa Mungu kadiri ya mapenzi ya Mungu na mwishoni ni jinsi ya kushirikishana maisha mapya yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake, ili kweli Mwenyezi Mungu aweze kuwa ni kiini na mwongozo wa maisha ya waja wake. Baba Mtakatifu anasema, wajibu unaotolewa katika Liturujia ya Neno la Mungu hususan Injili ni wakati ule Kristo Yesu alipokuwa anapanda kwenda Yerusalemu ili kukabiliana na Fumbo la Msalaba. Alikuwa anapanda kwenda kuwaandalia karamu ya maisha na uzima wa milele, mwaliko kwa watu wote kushiriki, lakini wenye upendeleo wa pekee ni maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Hiki ndicho kiini cha mifano ya Injili ya huruma ya Mungu, pale ambapo kile kilichopotea kinapatikana; yule aliyedhaniwa kwamba amefariki, anapokelewa tena na kwamba, kila sadaka ya maisha ya Mkristo inapata maana kamili katika mwanga wa furaha na sherehe ya kukutana na Kristo Yesu. Baba Mtakatifu anasema, wajibu wa kwanza unaopaswa kuangaliwa ni mahusiano na mafungamano ya kifamilia. Ufalme wa Mungu hauwezi kukita mizizi yake kwa mahusiano ya damu; upendeleo wa kikabila au mahali anapotoka mtu, hali ambayo inaweza kuwasababisha watu kutumbukia katika masuala ya rushwa na ufisadi, kashfa katika maisha na utume wa Kanisa. Mwaliko wa Kristo ni kila mmoja kumwangalia jirani yake kama ndugu, tayari kushirikishana furaha ya Injili bila kujali makando kando yake, mahali anapotoka na nafasi yake katika jamii. Ndiyo maana Kristo Yesu anakazia umuhimu wa kuacha yote na kumfuasa kikamilifu.

Baba Mtakatifu anasema, ni vigumu sana mwamini kumfuasa Kristo Yesu kwa kutaka kujenga Ufalme wa Mungu kadiri ya mafao na vionjo vyake binafsi, kiasi hata cha kukashfu jina la Mwenyezi Mungu, ili kuhalalisha: matumizi ya nguvu, ubaguzi, mauaji ya kimbari, vitendo vya kigaidi; utumwa pamoja na kuwakandamiza watu. Kristo Yesu anawataka wafuasi wake kujenga historia inayosimikwa katika udugu wa kibinadamu na mshikamano; kwa kuheshimu kazi ya uumbaji, kwa kujikita katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi pamoja na ushirikiano; kwa kujitahidi kufahamiana zaidi kuwa na mfumo na vigezo vinavyoweza kutumika kama sehemu ya mchakato wa maridhiano kati ya watu, hadi siku ile Bwana wa mavuno atakapokuja kuvuna shamba lake.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, maisha mapya yanayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu hayataki kuhalalisha matendo ya watu binafsi, kwa kujidai kwamba, wanaweza kutekeleza yote kwa nguvu zao binafsi, matokeo yake ni ubinafsi na kukengeuka kwa watu. Jambo la msingi ni kumtegemea Mwenyezi Mungu katika maisha na wakati wa kufanya maamuzi mazito. Mafanikio katika maisha ni zawadi ya kutoka kwa Mwenyezi Mungu na mchango wa umati mkubwa wa watu, watakaoweza kufahamika tu, wakati wa ufunuo wa Ufalme wa Mungu. Masharti yote yanayotolewa na Kristo Yesu yanapania kuwaandaa Mitume wake, kushiriki kikamilifu katika Karamu ya Ufalme wa Mungu, kwa kuondokana na vikwazo vinavyo wadidimiza katika utumwa, uchoyo na ubinafsi na hata wakati mwingine kumweka Mungu pembezoni mwa vipaumbele vya maisha, kwa kudhani kwamba, wako salama lakini ukweli wa mambo si hivyo, kwani furaha ya kweli inabubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Kristo Yesu Mfufuka.

Kristo Yesu alipokuwa anapanda kwenda mjini Yerusalemu, aliwataka wafuasi wake, kutoa kipambele cha kwanza kwa uwepo wa Mungu, nguzo ya maisha. Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, leo hii kuna umati mkubwa wa watu ambao wako nje kabisa na mpango wa Mungu, changamoto na mwaliko wa kufisha ubinafsi, uchoyo na kiburi, tayari kutangaza na kushuhudia udugu wa kibinadamu; kwa kuthamini utu, heshima na haki msingi za binadamu. Huu ni wakati wa kuthubutu kuanza hija inayo pania kuboresha hali ya maisha ya watu, kwa kujikita katika msingi wa haki, kwa kutokubali kumwabudu mungu fedha kwa kujikita katika uchu wa mali na madaraka, taaluma pamoja na kujitafutia umaarufu usiokuwa na mvuto wala mashiko! Furaha ya kweli kwa waamini ni kutambua kwamba, Kristo Yesu anajitaabisha kuwatafuta, huu ni mwaliko wa kusimama kidete kupambana na changamoto mamboleo sanjari na kutoa nafasi ili Injili iweze kumwilishwa katika maisha, kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu.

Papa: Misa Madagascar
08 September 2019, 17:56