Sinodi ya Kanisa Katoliki la Kigiriki nchini Ukraine: Baba Mtakatifu anawataka wajumbe kuhakikisha kwamba wanamsikiliza Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa. Sinodi ya Kanisa Katoliki la Kigiriki nchini Ukraine: Baba Mtakatifu anawataka wajumbe kuhakikisha kwamba wanamsikiliza Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa. 

Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa: Msikilizeni Roho Mtakatifu

Sinodi ya Kanisa si kama vikao vya Bunge, bali ni sehemu ya maisha na utume wa Kanisa wa kutaka kutembea kwa pamoja chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu kama sehemu ya mchakato wa utambulisho wa Kanisa na uinjilishaji unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Huu ndio ufafanuzi wa kina uliotolewa na Mtakatifu Paulo VI, Muasisi wa Sinodi kwa Kanisa Katoliki.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kulihamasisha Kanisa kuhusu umuhimu wa kumwilisha matunda ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, kwa kukazia umuhimu wa watu wa Mungu kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Hiki ni kiini cha “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa”. Baba Mtakatifu anakazia ukuhani wa waamini wote; umuhimu wa waamini kushiriki kikamilifu Sakramenti za Kanisa; umuhimu wa majadiliano ya kidini na kiekumene; ari na mwamko wa kimisionari pamoja na umuhimu wa waamini walei kuwa ni chachu ya uinjilishaji mpya na utakatifu kwa njia ya ushuhuda wa maisha, kama kielelezo makini cha imani tendaji!

Umoja, upendo na mshikamano wa dhati ni mambo msingi katika utangazaji na ushuhuda wa Injili ya upendo kwa watu wa Mataifa. Mambo yanayopaswa kuzingatiwa ni: Ufahamu wa Neno la Mungu; umuhimu wa toba na wongofu wa ndani; ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Haya ni mambo msingi katika mchakato mzima wa uinjilishaji mpya katika ulimwengu mamboleo. Dhana ya Sinodi ni wazo lililotolewa na Mtakatifu Paulo VI, linaloihusisha Familia ya Mungu katika ujumla wake. Baba Mtakatifu analitaka Kanisa kuanza kumwilisha dhana hii katika maisha ya Makanisa mahalia; Mabaraza ya Maaskofu; Mashirikisho ya Kanda hadi kufikia Kanisa la Kiulimwengu.

Hivi karibuni, Baba Mtakatifu alilipongeza Kanisa Katoliki la Kigiriki nchini Ukraine kutokana na: amana na utaji wake wa maisha ya kiroho; maadhimisho ya Liturujia Takatifu, bila kusahau utajiri unaobubujika kutoka katika Taalimungu, Sheria, Kanuni na Taratibu za Kanisa. Amewapongeza watu wa Mungu nchini Ukraine kwa udumifu na uaminifu wao kwa Kristo, Kanisa na kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 2 Septemba 2019 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Sinodi ya Maaskofu wa Kanisa Katoliki la Kigiriki nchini Ukraine. Katika hotuba yake, amekazia umuhimu wa wajumbe kumpatia nafasi Roho Mtakatifu katika mchakato mzima wa maadhimisho ya Sinodi.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Sinodi ya Kanisa si kama vikao vya Bunge, bali ni sehemu ya maisha na utume wa Kanisa wa kutaka kutembea kwa pamoja chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu kama sehemu ya mchakato wa utambulisho wa Kanisa na uinjilishaji unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Huu ndio ufafanuzi wa kina uliotolewa na Mtakatifu Paulo VI, Muasisi wa maadhimisho ya Sinodi mara baada ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Sinodi ni chombo cha uinjilishaji unaolisaidia Kanisa baada ya kutembea pamoja katika sala, tafakari na mang’amuzi mbali mbali wanaweza kufikia maamuzi kama ilivyokuwa kwa Mababa wa Mtaguso wa Efeso, walipofikia uamuzi kwamba, Bikira Maria ni Mama wa Mungu, “Theotokos”. Mwelekeo wa Kanisa kwa sasa ni dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Sviatoslav Shevchuk, Mkuu wa Kanisa Katoliki la Kigiriki nchini Ukraine amekazia umuhimu wa Sinodi kama jukwaa la kufafanua taalimungu na tasaufi ya maisha na utume wa Kanisa, ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Sinodi ni chombo kinacholiwezesha Kanisa kupanga sera na mikakati ya shughuli za kichungaji; kwa njia ya majadiliano, ushuhuda na tafakari ya Neno la Mungu chini ya nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu. Sinodi hii inawahusisha Maaskofu 47 kutoka sehemu mbali mbali za dunia pamoja na Kardinali Angelo De Donatis, Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma.

Huu ni wakati wa Kanisa kukita maisha na utume wake katika Sinodi, ili kushirikishana: furaha, matumaini, matatizo na changamoto katika maisha na utume wa Kanisa nchini Ukraine. Hii ni hija ya familia ya Mungu yenye utajiri mkubwa unaobubujika kutoka katika nchi mbali mbali, tamaduni na lugha. Wanataka kutembea kwa pamoja wakiongozwa na kauli mbiu “Ushirikiano na umoja katika ushuhuda wa Kanisa la Ukraine wakati huu”. Hii ni changamoto kwa Kanisa kuendelea kujikita katika wongofu wa kichungaji, ili kumwilisha amana na utajiri wa Mapokeo ya Kanisa Katoliki la Kigiriki nchini Ukraine sanjari na kuendeleza umoja na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Familia ya Mungu nchini Ukraine, ina kiu kubwa ya kuona inatembelewa siku moja na Baba Mtakatifu Francisko ambaye katika maisha na utume wake, ameendelea kuonja furaha, magumu na changamoto za maisha ya watu wa Mungu kutoka nchini Ukraine.

Papa: Ukraine

 

 

 

03 September 2019, 15:18