Papa Francisko amewataka Maaskofu Katoliki Makanisa ya Mashariki kudumisha moyo wa sala, unyenyekevu na upendo unaoshuhudiwa katika matendo! Papa Francisko amewataka Maaskofu Katoliki Makanisa ya Mashariki kudumisha moyo wa sala, unyenyekevu na upendo unaoshuhudiwa katika matendo! 

Papa Francisko: Ujumbe kwa Maaskofu: Unyenyekevu, Sala & Upendo katika matendo

Maaskofu wawe ni wajenzi wa haki na amani inayofumbatwa katika majadiliano na upatanisho wa kitaifa. Wawe ni vyombo na wajenzi wa utamaduni wa watu kukutana, ili kuondokana na wimbi la vita, machafuko na kinzani mbali mbali ili hatimaye, kupandikiza Injili ya upendo. Maaskofu wasaidie kuganga na kuponya madonda ya kihistoria, kwa kuvuka tabia ya maamuzi mbele na mipasuko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, katika maadhimisho ya Siku kuu ya Kutukuka kwa Msalaba, Jumamosi tarehe 14 Septemba 2019 amekutana na kuzungumza na Maaskofu Katoliki kutoka katika Makanisa ya Mashariki mwa Bara la Ulaya, ambao wamekuwepo mjini Roma kuanzia tarehe 12- 14 Septemba 2019, ili kushiriki katika mkutano wa kawaida wa mwaka. Baba Mtakatifu katika hotuba yake, amewapongeza kwa utajiri mkubwa wa Mapokeo ya Kanisa unaofumbatwa katika Makanisa ya Mashariki; Ushuhuda wa uaminifu na umoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro; Mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani na upatanisho; Tasaufi, Liturujia na Taalimungu ya Makanisa ya Mashariki pamoja na utambulisho wa Makanisa mahalia unaopaswa kuendelezwa na kudumishwa. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanasema Kanisa takatifu na Katoliki ni sehemu ya Fumbo ya Mwili wa Kristo unaoundwa na waamini wanaounganishwa kiimani na Roho Mtakatifu, Sakramenti na uongozi, wakifungamanishwa na hierakia, wanaunda Makanisa maalum yenye madhehebu.

Katika Makanisa haya wanaendelea kusema Mababa wa Mtaguso kuna ushirika wa ajabu, kiasi kwamba, tofauti hizi haziwezi kudhuru umoja wa Kanisa, bali unaendelea kuuimarisha. Baba Mtakatifu amesema, hija yake ya kitume nchini Romania, alibahatika kuwatangaza maaskofu saba kuwa ni wenyeheri, kwani katika maisha na utume wao, walijikita katika ushuhuda na uaminifu wao kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, kiasi hata cha kuyamimina maisha yao. Uaminifu huu ni kito cha thamani kubwa katika maisha ya kiimani na kamwe hakiwezi kufutika. Hii inatokana na ukweli kwamba, kwao imani ilimwilishwa katika maisha ya kila siku. Imani isaidie mchakato wa umoja na mshikamano wa watu wa Mungu ili kuondokana na utaifa, umajimbo na ukabila usiokuwa na mvuto. Watakatifu na mashuhuda wa imani wanaendeleza umoja na ushirika huu huko mbinguni, changamoto na mwaliko kwa Kanisa kusafisha na kupyaisha kumbu kumbu zake ili kujenga na kudumisha umoja wa wafuasi wa Kristo, ili wote wawe wamoja! Makanisa Katoliki Mashariki mwa Bara la Ulaya yanayo utume wa kuendeleza majadiliano ya kiekumene.

Maaskofu  wanahamasishwa na Baba Mtakatifu kuwa ni wajenzi wa haki na amani inayofumbatwa katika majadiliano na upatanisho wa kitaifa. Wawe ni vyombo na wajenzi wa utamaduni wa watu kukutana, ili kuondokana na wimbi la vita, machafuko na kinzani mbali mbali ili hatimaye, kupandikiza Injili ya upendo. Maaskofu wasaidie kuganga na kuponya madonda ya kihistoria, kwa kuvuka tabia ya maamuzi mbele na mipasuko. Baba Mtakatifu anasema, amepata uzoefu mkubwa kwa kukutana, kusali na kutafakari kwa pamoja katika nyakati mbali mbali za maisha na utume wake kama Khalifa Mtakatifu Petro. Kwa pamoja wamewezeshwa kusali kwa ajili ya kuombea amani nchi Takatifu, wakaweza kushuhudia wimbi kubwa ya wakimbizi na wahamiaji kule Lesvos, Ugiriki, Sala kwa ajili ya Kuombea Amani Mashariki ya Kati. Haya ni mambo yanayosimikwa katika: sala, unyenyekevu na upendo wa dhati unaowawajibisha kutembea bega kwa bega. Askofu wa Roma ni mtumishi wa watumishi wa Mungu “Servus servorum Dei”.

Baba Mtakatifu anasema, Makanisa ya Mashariki yana utajiri na amana kubwa katika: Tasaufi, Liturujia na Taalimungu. Kuna haja ya kuwafunda Mapadre wapya kutoka Makanisa ya Magharibi, ili kujichotea utajiri huu, unaoweza kuwasaidia kufungua upendo wao, ili kuishi na watu wote kwa upendo unaomwilishwa katika huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na upweke hasi, umaskini wa hali na kipato; watoto wanaotolewa mimba wangali tumboni mwa mama zao. Hawa ni wale vijana wasiokuwa na matumaini ya leo na kesho iliyo bora kwa kukosa matumaini; familia zilizovunjika na kusambaratika; wagonjwa na wazee. Kwa hakika upendo unagangana na kuponya mipasuko ya kijamii. Baba Mtakatifu amehitimisha hotuba yake kwa kuwakumbusha Maaskofu kwamba, utambulisho wao ni upendo kwa Mungu na jirani zao; dhamana na wajibu wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kwa wale wote wanaokutana nao katika hija ya maisha yao. Wawe ni vyombo na mashuhuda wa: furaha, upendo na matumaini kwa wale wote waliokata tamaa. Yote yatapita, lakini upendo kwa Mungu na jirani wadumu milele.

Papa: Maaskofu

 

15 September 2019, 12:58