Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 4 Agosti 2019 ametafakari kuhusu tajiri mpumbavu na mali ya ulimwengu huu! Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 4 Agosti 2019 ametafakari kuhusu tajiri mpumbavu na mali ya ulimwengu huu!  (ANSA)

Baba Mtakatifu Francisko: Tajiri mpumbavu na mali ya dunia!

Tajiri mpumbaji ni mtu aliyejitafuta, kiasi cha kumezwa na ubinafsi, huku akijikweza kupita kiasi. Mambo muhimu ya kuangalia ni haya yafuatayo anasema Baba Mtakatifu Francisko: wingi wa mazao yaliyopatikana shambani mwake; mafanikio haya yalimhakikishia usalama wa maisha kiasi kwamba, angeweza kupumzika, akala, akanywa na kufurahi, kielelezo cha amani na utulivu wa maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 4 Agosti 2019 amegusia kwa namna ya pekee kabisa jinsi ambavyo mtu  mmoja katika mkutano alivyomwomba Yesu kuwa ni msuluhishi wa urithi ndani ya familia, kwani hali ya hewa ilikuwa inaanza kuchafuka! Kristo Yesu katika jibu lake la msingi, akatoa angalisho ya kujilinda na choyo, kwa maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo. Huo ukawa ni mwanzo wa mfano wa tajiri mpumbafu, aliyedhani kwamba, angeweza kuwa na furaha tele kwa kufanikiwa kuvuna sana katika kipindi cha mwaka huo wa mavuno, kiasi cha kujisikia kuwa na usalama kwa mavuno aliyofanikiwa kupata! Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujitaabisha kusoma Injili ya Luka, Sura ya 12: 13-21.

Huu ni mfano muhimu sana unaobeba mafundisho muhimu katika maisha ya watu. Simulizi hili linachukua mwelekeo mpya unaoonesha ukinzani kati ya matarajio ya tajiri pumbavu na mpango wa Mungu katika maisha yake. Tajiri mpumbaji ni mtu aliyejitafuta, kiasi cha kumezwa na ubinafsi, huku akijikweza kupita kiasi. Mambo muhimu ya kuangalia ni haya yafuatayo anasema Baba Mtakatifu Francisko: wingi wa mazao yaliyopatikana shambani mwake; mafanikio haya yalimhakikishia usalama wa maisha kiasi kwamba, angeweza kupumzika, akala, akanywa na kufurahi, kielelezo cha amani na utulivu wa maisha. Lakini kwa bahati mbaya, maneno ya Mungu “yanafyekelea mbali ndoto ya tajiri mpumbavu”. Mwenyezi Mungu anamwambia “Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako” badala ya kufurahia maisha kwa “kula kuku kwa mrija” akashindwa kujitajirisha mbele ya Mwenyezi Mungu.

Matokeo yake tajiri mpumbavu anaulizwa swali kwa kejeri “Na vitu alivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani?” Baba Mtakatifu anakiri kwamba, kumekuwepo na mapambano pamoja na kinzaji nyingi ndani ya familia kuhusu mali ya urithi. Inasikitisha kuona kwamba, wakati mtu anakaribia kukutana na mauti, utaona makundi ya watu wakimwijia, kila mtu akitaka apewe kile kinachomwangukia katika urithi wake! Na hata wakati mwingine, wanagawana mali, wakati mwenye mali bado yuko hai kabisa! Tajiri huyu ni mpumbavu kwa sababu katika sera, mikakati na mipango yake yote, alimweka Mwenyezi Mungu pembezoni mwa vipaumbele vyake, “akaonekana kama tai inayoning’nia mtini”.

Baba Mtakatifu anasema, Mwinjili Luka anahitimisha mfano huu wa tajiri mpumbavu kwa kutoa angalisho kwamba, “ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu”. Utajiri, mali ya dunia na karama ni mambo muhimu sana katika maisha ya mwanadamu. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, utajiri, mali na karama hizi ambazo ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu zinamwilishwa katika uaminifu pamoja na kuwashirikisha maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Utajiri, mali na karama mbali mbali zisiwe ni kizingiti cha kwenda mbinguni. Mtakatifu Paulo, Mtume anawakumbusha waamini kufikiri yaliyo ya juu, siyo yaliyo katika nchi. Baba Mtakatifu anawaangalisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wasiukimbie ukweli, bali wapambane na hali pamoja na mazingira yao, kwa kutoa kipaumbele cha pekee katika tunu msingi za maisha yaani: Haki, mshikamano, ukarimu, udugu na amani.

Hii ni changamoto ya kuhakikisha kwamba, waamini wanajitahidi kuishi mintarafu mtindo wa tunu msingi za Kiinjili, ili kamwe wasimezwe na malimwengu. Kwa muhtasari huu ni upendo kwa Mungu na kwa jirani; na kuwahudumia maskini na wahajitaji kwa moyo wa upendo na ukarimu; pamoja na kujisadaka bila ya kujibakiza hata kidogo. Baba Mtakatifu anakaza kusema, tamaa na uchu wa mali na utajiri wa dunia hii ni kiu ambayo kamwe haiwezi kuzimishwa, kila wakati kuna kishawishi cha kutaka kupata zaidi. Upendo wa kweli ni chemchemi ya furaha, amani na utulivu wa ndani. Lakini, uchu wa fedha na mali za ulimwengu huu, mara nyingi ni chanzo cha vita, kinzani, mahangaiko ya ndani, uhalifu, uasi na upotofu. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumwomba Bikira Maria ili aweze kuwasaidia, ili kamwe wasitumbukie kwenye usalama wa mambo mpito, bali kila siku wawe ni mashuhuda wa tunu msingi za Kiinjili hapa duniani!

Papa: Tajiri Mpumbavu
04 August 2019, 10:59