Baba Mtakatifu Francisko: Tarehe 4 Agosti 2019, Kanisa limekumbuka Miaka 160 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Yohane Maria Vianney, Msimamizi wa Maparoko Duniani. Baba Mtakatifu Francisko: Tarehe 4 Agosti 2019, Kanisa limekumbuka Miaka 160 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Yohane Maria Vianney, Msimamizi wa Maparoko Duniani. 

Papa Francisko: Mtakatifu Yohane Maria Vianney, Miaka 160 kifo chake!

Mtakatifu Yohane Maria Vianney alizaliwa mwaka 1786. Akapewa Daraja takatifu ya Upadre tarehe 12 Agosti 1815. Akafariki dunia mwaka 1859 akiwa na umri wa miaka 73. Tarehe 8 Januari 1905 akatangazwa kuwa Mwenyeheri na Papa Pio X. Tarehe 31 Mei 1925 Papa Pio wa XI akamtangaza kuwa Mtakatifu na kunako mwaka 1929 akamtangaza kuwa ni Msimamizi wa Maparoko duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara tu baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 4 Agosti 2019, amesema kwamba, Mama Kanisa, tarehe 4 Agosti 2019 ameadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 160 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Yohane Maria Vianney. mfano bora wa kuigwa na mapadre wote duniani katika wema, upendo na ukarimu wake. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko amewaandika mapadre wote duniani, barua maalum ambamo anakazia mambo makuu yafuatayo. Mosi anawataka mapadre wanaendelee kuandika kurasa za maisha na utume wa Kipadre sehemu mbali mbali za dunia. Anapenda kuwashukuru na kuwatia moyo Mapadre wote wakitambua kwamba, wao kwa hakika ni marafiki wa Kristo Yesu katika maisha na utume wao.

Baba Mtakatifu anasema, kama ilivyokuwa kwenye Agano la Kale, ameyaona mateso na mahangaiko ya watu wake, anasema haachi kutoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya Mapadre, akiwakumbuka katika sala zake; anataka kuwafariji wote katika nyoyo zao, ili hatimaye, waweze kuimba ukuu na utukufu wa Mungu katika maisha yao. Ushuhuda wa maisha na utume wa Mtakatifu Yohane Maria Vianney uwe ni mfano bora wa sadaka na majitoleo ya maisha na utume wa Kipadre katika ulimwengu mamboleo. Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Yohane Maria Vianney alizaliwa kunako tarehe 8 Mei 1786. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi kwa shida kubwa, alipewa Daraja takatifu ya Upadre tarehe 12 Agosti 1815. Akafariki dunia tarehe 4 agosti 1859 akiwa na umri wa miaka 73.

Tarehe 8 Januari 1905 akatangazwa kuwa Mwenyeheri na Papa Pio X. Ilikuwa ni tarehe 31 Mei 1925 Papa Pio wa XI akamtangaza kuwa Mtakatifu na kunako mwaka 1929 akamtangaza kuwa ni Msimamizi wa Maparoko duniani. Ni Padre ambaye kwa muda wa miaka 40 alijisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwahudumia watu wake kwa Neno na Sakramenti za Kanisa; akajitakatifuza kwa sala, toba na wongofu wa ndani, uliofumbatwa katika maisha adili na unyenyekevu mkuu. Akajitahidi kuwaongoza watu wa Mungu katika hija ya maisha, kuelekea kwenye utakatifu na furaha ya maisha na uzima wa milele.

Papa: Miaka 160 Vianney
04 August 2019, 10:18