Papa Francisko asema, Mwongozo wa Utume na maisha ya Kanisa unasimikwa katika: Sala, Hija, Ufukara pamoja na ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Papa Francisko asema, Mwongozo wa Utume na maisha ya Kanisa unasimikwa katika: Sala, Hija, Ufukara pamoja na ushuhuda wenye mvuto na mashiko! 

Mwongozo wa utume wa Kanisa: Sala, Kwenda, Ufukara & Ushuhuda katika matendo!

Mwongozo wa Utume wa Kanisa unafumbatwa: Mosi katika Sala; Pili ni kwenda na Tatu; wasichukue mfuko, wala mkoba na nyumba yoyote watakayoingia waseme kwanza Amani iwemo nyumbani humu na wakae katika nyumba iyo hiyo, wala wasihame hame kutoka nyumba hii kwenda nyumba hii, wawapoze wagonjwa waliomo na kuwaambia kwamba Ufalme wa Mungu umewakaribia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya XIV ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa inamwonesha Kristo Yesu akiwatuma wafuasi wengine 70 kuungana na Mitume kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Namba 72 kadiri ya Maandiko Matakatifu inaonesha Mataifa yote duniani. Tukio hili ni utangulizi wa utume wa Kanisa wa kutangaza na kushuhudia Injili kwa watu wote. Wafuasi hawa wanakumbushwa kwamba, mavuno ni mengi lakini watenda kazi katika shamba la Bwana ni wachache, hivyo wanapaswa kumwomba Bwana wa mavuno ili apeleke watenda kazi katika mavuno yake. Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 7 Julai 2019.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Mwongozo wa Yesu kuhusu utume wa Kanisa ni endelevu na dumifu kwani waamini wanahimizwa kusali daima ili kumwomba Mwenyezi Mungu aweze kupeleka watenda kazi katika mavuno yake, yaani ulimwengu. Hii ni changamoto na mwaliko kwa waamini kuwa wazi mbele ya Mwenyezi Mungu ili kudumisha ari na mwamko wa kimisionari, kwa kusali, huku wakiwa na mwelekeo mpana zaidi kwa ajili ya Kanisa zima na wala si kwa ajili ya mahitaji yao binafsi. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Mwongozo wa Utume wa Kanisa unafumbatwa: Mosi katika Sala; Pili ni kwenda na Tatu; wasichukue mfuko, wala mkoba na nyumba yoyote watakayoingia waseme kwanza Amani iwemo nyumbani humu na wakae katika nyumba iyo hiyo, wala wasihame hame kutoka nyumba hii kwenda nyumba hii, wawapoze wagonjwa waliomo na kuwaambia kwamba Ufalme wa Mungu umewakaribia na wasipowakaribisha watoke humo na kuwakung’utia mavumbi ya mji wao!

Kumbe, utume wa Kanisa unafumbatwa kwa namna ya pekee katika sala; unalionesha Kanisa ambalo daima liko katika hija, linasafiri na hivyo linatakiwa kuambata ufukara; ili hatimaye, liweze kuwapelekea watu amani na uponyaji, alama makini za uwepo wa Ufalme wa Mungu ambao kimsingi si wongofu wa shuruti, bali ushuhuda wa utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu. Utume huu unaitaka Mihimili ya uinjilishaji kukita maisha yake katika ukweli, uwazi na uhuru wa Kiinjili, huku wakisukumwa na Habari Njema ya Wokovu kubariki na wala si kuwalaani watu! Baba Mtakatifu anasema, kama kweli utume wa Kanisa utaweza kutekelezwa kwa kuzingatia Mwongozo uliotolewa na Kristo Yesu, kwa hakika, Kanisa litakuwa ni chemchemi ya furaha, kama walivyorudi wale wafuasi 70 wakiwa na furaha si kwa sababu pepo waliwatii au Shetani alianguka kutoka mbinguni kama umeme, bali kwa sababu majina yao yameandikwa mbinguni; kwenye “sakafu” ya Moyo wa Mwenyezi Mungu.

Waamini wanakumbushwa kwamba, Mwenyezi Mungu ni chemchemi ya furaha ambayo ni zawadi inayotolewa kwa mfuasi mmisionari, anayetembea huku akiwa ameambatana na Kristo Yesu, huku akijifunza kutoka kwake, ili aweze kujisadaka bila hata kujibakiza hata chembe kidogo; huyu ni mtu ambaye yuko huru kabisa, tayari kutumia karama na utajiri wake kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya jirani zake. Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu Francisko amewaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria, ili aweze kuwashika mkono wafuasi wa Kristo Yesu, kwa kuendeleza utume wao wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Waamini watambue kwa hakika kwamba, Mwenyezi Mungu anawapenda, anataka kuwakomboa na anawaita ili wawe ni sehemu ya Ufalme wake wa mbinguni!

Papa: Mwongozo
08 July 2019, 11:53