Vatican News
Papa Francisko atoa kibali kwa mapadre wa maisha ya kiroho utume wa bahari kuwaungamisha mabaharia na wavuvi na kuwaondolea dhambi zote, kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu! Papa Francisko atoa kibali kwa mapadre wa maisha ya kiroho utume wa bahari kuwaungamisha mabaharia na wavuvi na kuwaondolea dhambi zote, kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu!  (Vatican Media)

Utume wa Bahari wapewa mamlaka ya kuwaondolea watu dhambi zote!

Kwa kutambua magumu yanayowakabili mabaharia na wavuvi, Baba Mtakatifu Francisko kama ilivyokuwa kwa Wamisionari wa Huruma ya Mungu, amewapatia madaraka Mapadre wote washauri wa maisha ya kiroho kwa mabaharia na wavuvi ili kuwaondolea dhambi zote hata zile ambazo zilikuwa zimehifadhiwa kwa ajili ya kiti kitakatifu tu! Lengo ni kuwapatia amani na utulivu wa ndani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka Mapadri washauri wa kiroho pamoja na watu wa kujitolea kuendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa mabaharia pamoja na wavuvi sehemu mbali mbali za dunia, wakijaribu kuiga na kufuata mifano ya watangulizi wao. Mama Kanisa anajiandaa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu Papa Pio XI alipoanzisha Utume wa Bahari, Stella Maris sanjari na Kongamano la 25 ya Utume wa Bahari litakaloadhimishwa huko Glasgow, nchini Scotland. Huu ni utume ulioasisiwa na waamini walei ndani ya Kanisa kama sehemu ya mchango wao wa kuyatakatifuza malimwengu kwa ushuhuda wenye mvuto na mashiko.

Baba Mtakatifu anasema, Mama Kanisa anapenda kutafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini! Papa Pio XI alitamani sana kuona kwamba, Utume wa Bahari unaendelezwa kwenye Bahari na fukwe mbali mbali za dunia. Roho Mtakatifu, kwa maombezi ya Bikira Maria aendelee kupyaisha utume na huduma hii mintarafu mahitaji ya ulimwengu mamboleo! Kuna mabaharia ambao dhamiri zao zinahangaika sana na mara nyingi Mapadre wa maisha ya kiroho kwa mabaharia na wavuvi wamekuwa ni msaada mkubwa. Mabaharia ni watu wanaofanya kazi zao mara nyingi nje ya nchi, makazi na familia zao!

Mapadre washauri wa kiroho katika muktadha kama huu, wanakuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya matumaini kwa mabaharia na wavuvi waliopondeka na kuvunjika moyo! Mapadre wanapaswa kuwa ni watu wenye huruma, wapole na wanyenyekevu! Kwa kutambua magumu yanayowakabili mabaharia na wavuvi, Baba Mtakatifu Francisko kama ilivyokuwa kwa Wamisionari wa Huruma ya Mungu, amewapatia madaraka Mapadre wote washauri wa maisha ya kiroho kwa mabaharia na wavuvi ili kuwaondolea watu dhambi zote hata zile ambazo zilikuwa zimehifadhiwa kwa ajili ya kiti kitakatifu tu! Baba Mtakatifu anasema, lengo ni kuweza kuwapatia watu amani na utulivu wa maisha ya kiroho huko baharini!

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 27 Juni 2019 alipokutana na kuzungumza na Mapadre washauri wa maisha ya kiroho na watu wa kujitolea katika Utume wa Bahari ambao hadi wakati huu wanatekeleza dhamana hii kwenye bandari zaidi ya 300 sehemu mbali mbali za dunia. Huduma hii ni ya maisha ya kiroho na kimwili kwa ajili ya mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao. Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, zaidi ya asilimia 90% ya biashara yote duniani inategemea bahari. Bila mabaharia, uchumi wa dunia ungeyumba sana; bila wavuvi, watu wengi wangeteseka kwa baa la njaa!

Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza kwa utume wanaoutekeleza sehemu mbali mbali za dunia. Mabaharia na wavuvi ni watu wanakumbana na changamoto mbali mbali za maisha, ikiwa ni pamoja na kusumbuliwa na upweke hasi, nyanyaso mbali mbali pamoja na kutendewa kinyume cha haki msingi za binadamu. Ni watu ambao mara nyingi wanatumbukizwa kwenye biashara haramu ya binadamu na viungo vyake, utumwa mamboleo bila kusahau kazi za suluba. Ni watu ambao wakati mwingine wanapokea “mshahara kiduchu”, hata kiasi cha kutelekezwa bandarini na wamiliki wa Meli. Ni watu ambao joto na baridi, dhoruba na tufani zimekuwa ni sehemu ya maisha yao ya kila siku na hata wakati mwingine, wanapambana uso kwa uso na magaidi pamoja na maharamia baharini!

Mabaharia wakati mwingine, hawapokelewi kwa moyo wa ukarimu hata pale wanapoonesha shida na magumu yanayowasibu safarini! Hawa ndio mabaharia na wavuvi ambao, Mama Kanisa anawaangalia kwa jicho la pekee kwa njia ya Utume wa Bahari, Stella Maris. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Mapadre washauri wa kiroho pamoja na watu wa kujitolea wamekabidhiwa dhamana ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu katika ulimwengu wa mabaharia na wavuvi, kwa kukutana na kuzungumza na watu hawa ambao wanakabiliana na changamoto mbali mbali za maisha!

Hapa wanaalikwa kutekeleza sanaa ya kusikiliza kwa makini na kuwa na uwazi wa moyo unaowawezesha kuwa karibu zaidi na mabaharia pamoja na wavuvi, kwa kuwa na subira. Kusikiliza anasema Baba Mtakatifu kutawawezesha kupata ishara na neno sahihi, jambo linaloonesha kwamba, wao si watazamaji tu, bali wanaguswa na changamoto za maisha ya watu! Mapadre washauri wa maisha ya kiroho na watu wa kujitolea wanahimizwa na Baba Mtakatifu kutekeleza wajibu huu ambao wakati mwingine ni matokeo ya chuki na uhasama! Biashara haramu ya binadamu, kazi za suluba, uvunjifu wa haki msingi za binadamu ni changamoto kubwa kwa Utume wa Bahari. Ni kwa njia ya Utume wa Bahari kwamba, watu wengi wameonja Injili ya matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi.

Hawa ni watu ambao wameguswa na huruma na faraja ya Mungu katika maisha yao kwa kutambua kwamba, wao pia wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kumbe, utu, heshima  na haki msingi za binadamu ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wao! Wawe ni wajumbe na mashuhuda wa amani, wajenzi wa udugu wa kibinadamu na haki, mahali ambapo watu bado wanadhulumiwa na kunyanyasika. Upendo wa dhati ni dawa pekee, inayoweza kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya kibinadamu anasema Baba Mtakatifu Francisko!

Papa: Utume wa Bahari
27 June 2019, 16:41