Vatican News
Papa Francisko asema, kazi ni utimilifu wa maisha ya mtu binafsi, kijamii na kiekolojia. Utu, heshima na haki msingi za binadamu zinapaswa kuwa kiini cha sera na mikakati ya uchumi na kazi. Papa Francisko asema, kazi ni utimilifu wa maisha ya mtu binafsi, kijamii na kiekolojia. Utu, heshima na haki msingi za binadamu zinapaswa kuwa kiini cha sera na mikakati ya uchumi na kazi.  (ANSA)

Ujumbe wa Papa Francisko: Shirika la Kazi Duniani, ILO, Miaka 100

Umuhimu wa kazi kama utimilifu wa mtu binafsi, kijamii na kiekolojia; leo hii kuna haja ya kutengeneza na kulinda fursa za ajira duniani kwa kuzingatia matumizi bora ya ardhi mintarafu mapokeo, rasilimali muda na teknolojia. Huu ni muhtasari wa ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa washiriki wa mkutano wa 108 wa Shirika la Kazi Duniani, ulioanza hapo tarehe 10-21 Juni 2019.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Kazi Duniani, ILO, mambo makuu yafuatayo yanapaswa kupewa kipaumbele: Umuhimu wa kazi kama utimilifu wa mtu binafsi, kijamii na kiekolojia; leo hii kuna haja ya kutengeneza na kulinda fursa za ajira duniani kwa kuzingatia matumizi bora ya ardhi mintarafu mapokeo, rasilimali muda na teknolojia. Huu ni muhtasari wa ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa washiriki wa mkutano wa 108 wa Shirika la Kazi Duniani, ulioanza hapo tarehe 10-21 Juni 2019. Ujumbe huu, umesomwa kwa niaba ya Baba Mtakatifu na Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu.

Baba Mtakatifu amemhakikishia Bwana Guy Ryder, Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani kwamba, atakapopata nafasi katika shughuli zake za kitume, siku moja ataweza kutembelea Makao Makuu ya Shirika la Kazi Duniani,  huko Geneva kwani anatambua na kuthamini umuhimu wa kazi kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa amani duniani, haki jamii pamoja na kuendeleza maboresho ya kazi. Licha ya juhudi zote hizi, bado kuna ukosefu mkubwa wa fursa za ajira duniani; kuna watu wanaonyonywa na kudhalilishwa utu na heshima yao katika biashara ya binadamu na utumwa mamboleo bila kusahau kazi za shuruti na ujira “kiduchu”. Kuna watu wanafanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi bila kusahau uchafuzi mkubwa wa mazingira, hali ambayo pengine inachangiwa na mbinu za kiteknolojia na matumizi yake!

Baba Mtakatifu anafafanua kuhusu dhana ya kazi kama utimilifu wa mtu binafsi, kijamii na kiekolojia, kwa kusema kwamba, kazi ni sehemu muhimu sana ya maisha ya mwanadamu ambaye ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kwamba, kazi ni wito wa mwanadamu. Hapa ni mahali pa kubadilishana mawazo, mang’amuzi na uzoefu wa maisha; ni mahali pa kujenga mahusiano kwa kukutana na watu wengine, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi sanjari na ujenzi wa utamaduni wa upendo. Wito wa kazi una uhusiano wa pekee na mazingira nyumba ya wote, ambayo mwanadamu amekabidhiwa na Mwenyezi Mungu kuyalinda, kuyatunza na kuyaendeleza kama sehemu ya ekolojia ya maisha ya mtu binafsi, jamii na dunia katika ujumla wake.

Kazi kamwe haiwezi kuhesababiwa kuwa ni sehemu ya mnyororo wa uzalishaji wa bidhaa na utoaji wa huduma kwa ajili ya kutengeneza mtaji. Kanuni maadili ni muhimu sana katika kulinda na kuzalisha fursa za ajira kama sehemu ya utimilifu wa maisha ya mwanadamu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kutengeneza na kulinda fursa za ajira ajira duniani na kwamba, fursa za ajira zinapaswa kuangaliwa kwa mwanga wa masuala ya kijamii-kisiasa na kiuchumi, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kanisa linapenda pia kuchangia katika mchakato huu kupitia Shirika la Kazi Duniani. Mfumo wa uchumi unapaswa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu, kwa kulinda na kudumisha mazingira nyumba ya wote, kwa ajili ya maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu.

Binadamu anapaswa kuwa ni kiini na hatima ya sera na mikakati ya maendeleo fungamani kwa kukazia: umuhimu wa ardhi, makazi na ajira. Ardhi ni amana na utajiri wa binadamu wote na matunda yake ni kwa ajili ya wote. Kila mtu anayo haki ya kutumia ardhi kwa ajili ya mafao yake. Hii ni kanuni maadili inayolinda utaratibu wa maisha. Kuna uhusiano na mwingiliano mkubwa kati ya kazi na mazingira na kwamba, kuna baadhi ya shughuli za binadamu zinazosababisha uchafuzi mkubwa wa mazingira, kwa kuzalisha hewa ya ukaa. Jumuiya ya Kimataifa inapoweka sera na mikakati ya kulinda fursa za ajira, haina budi kuhakikisha kwamba inazingatia mwingiliano kati ya ardhi, makazi na ajira.

Baba Mtakatifu anasema, mapokeo “tradion” kutoka katika mzizi neno wa lugha ya Kilatini “tradere” yaani kurithisha, si tu teknolojia, bali pia uzoefu, dira na matumaini, kwa ajili ya ustawi wa binadamu na utunzaji wa mazingira nyumba ya wote! Rasilimali muda imekuwa ni changamoto kubwa kwani muda umekuwa ni kikwazo cha maendeleo na maboresho ya maisha ya watu kutokana na kasi kubwa na hivyo watu kushindwa kutambua kwamba, rasimali muda ni zawadi kutoka kwa Mungu inayopaswa kupokelewa, kudukishwa na kuthaminiwa kama sehemu ya mchakato wa maendeleo ya mwanadamu. Watu wanahitaji rasilimali muda kwa ajili ya kazi, kupumzika na kutafakari uzuri wa kazi ya uumbaji.

Rasilimali muda ni muhimu katika kupanga na kutekeleza majukumu mbali mbali ya maisha. Jamii inahitaji kusimama na kutulia, ili kugundua thamani ya muda badala ya kukimbizana na wakati! Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, teknolojia nimuhimu sana na kamwe isiwajengee watu kiburi cha kuwa na nguvu, kutaka kuwatala na kuwamiliki wengine au kuwachezea kama wanavyopenda. Kumekuwepo na maendeleo makubwa ya sayansi katika mfumo wa kidigitali, matumizi ya roboti pamoja na matumizi ya“Artificial Intelligence” yaani “akili bandia” yote haya yanaendelea kuleta mageuzi makubwa katika ulimwengu wa kazi na mahali wanapoishi watu! Mabadiliko haya ni makubwa, kumbe, yanapaswa kuongozwa na kusimamiwa na sheria mpya, kanuni maadili na utu wema ili kudhibiti kazi za suluba kwa watoto wadogo au ukosefu wa fursa za ajira kwa vijana wa kizazi kipya!

Baba Mtakatifu amelipongeza Shirika la Kazi Duniani kwa kuendelea kuapmbana na kazi za suluba kwa watoto wadogo, kiasi cha kuathuru ndoto na matumaini yao ya kuweza kuchangia ustawi na maendeleo ya jamii kwa siku za usoni. Ukosefu wa fursa za ajira na usalama kazini ni matokeo ya mfumo wa uchumi kandamizi unaotaka kunyonya nguvu kazi na mazingira, kwa kumweka mwanadamu pembezoni mwa vipaumbele vya kiuchumi. Hizi ni dalili za ukosefu wa sera na mikakati makini inayopaswa kutumika kwa ajili ya kurekebisha mwelekeo huu, ili haki iweze kutendeka. Shirika la Kazi Duniani, ILO kwa kushirikiana na Kanisa linaweza kusaidia kuwaundia watu hisia za utunzaji bora wa mazingira, sera na mikakati ya maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu, kwa kuunganisha mapokeo, rasilimali muda na teknolojia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafo ya wengi. Mwishoni, Baba Mtakatifu analitaka Shirika la Kazi Duniani, kuendelea kushughulikia changamoto changamani za kazi kwa ari na moyo mkuu!

Papa: Shirika la Kazi Duniani
26 June 2019, 15:29