Papa Francisko anawahamasisha waamini walei kushiriki kikamilifu katika masuala ya kisiasa mintarafu mwanga wa Injili na Mafundisho Jamii ya Kanisa Papa Francisko anawahamasisha waamini walei kushiriki kikamilifu katika masuala ya kisiasa mintarafu mwanga wa Injili na Mafundisho Jamii ya Kanisa 

Papa Francisko: Walei katika siasa kadiri ya mwanga wa Injili!

Baba Mtakatifu Francisko anakazia: Umoja na mshikamano katika utekelezaji wa mpango mkakati katika masuala ya kisiasa kadiri ya mwanga wa tunu msingi za Kikristo. Anahimiza umuhimu wa kukuza na kudumisha majadiliano katika ukweli na uwazi; Maisha ya kijamii yarutubishwe na sheria ya upendo kwa Mungu na jirani; Kanuni maadili pamoja na ushuhuda wa imani katika matendo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hivi karibuni, Wakatoliki nchini Italia wameadhimisha kongamano la kimataifa kuhusu uhuru wa wote, lililoongozwa na kauli mbiu “Hali halisi na uwajibikaji mpya” kama sehemu ya utekelezaji wa mbinu mkakati wa mambo 12 yaliyobainishwa na Mtumishi wa Mungu Padre Luigi Sturzo, miaka 100 iliyopita. Huo ukawa ni mwanzo wa Wakatoliki nchini Italia kujishughulisha na masuala ya kisiasa! Mambo haya ni: utu, heshima na haki msingi za binadamu; dhana ya uhuru mintarafu tunu msingi za Kiinjili; uhuru wa kuabudu unaofumbatwa pia katika uhuru wa kiraia.

Kanisa linapaswa kuwa huru kwa kujikita katika umoja wa watoto wake, ili liweze kutekeleza dhamana na utume wake wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Padre Luigi Sturzo mwanzo mwa maisha na utume wake wa Kikasisi alisimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha uhuru wa Kanisa unaofumbatwa katika ufukara na mshikamano na watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kanisa linapaswa kuandamana na kushikamana na watu katika uhalisia wa maisha yao. Haya ni kati ya mambo msingi yaliyobanishwa katika kongamano hili la kimataifa lililofanyika huko Caltagirone, Kisiwani Sicilia, Kusini mwa Italia!

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa washiriki wa kongamano hili amakazia kwa namna ya pekee: Umoja na mshikamano katika utekelezaji wa mpango mkakati katika masuala ya kisiasa kadiri ya mwanga wa tunu msingi za Kikristo. Anahimiza umuhimu wa kukuza na kudumisha majadiliano katika ukweli na uwazi; Maisha ya kijamii yanayorutubishwa na sheria ya upendo kwa Mungu na jirani; Kanuni maadili pamoja na ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo! Baba Mtakatifu anasema, kongamano hili ni muhimu sana katika historia ya Italia na Bara la Ulaya katika ujumla wake, changamoto na mwaliko kwa familia ya Mungu kuhakikisha kwamba, inamwilisha mpango mkakati wa Mtumishi wa Mungu Padre Luigi Sturzo, ili kujenga na kudumisha majadiliano ya kitamaduni na kijamii mintarafu mwanga wa tunu msingi za maisha na utume wa Kikristo.

Padre Lugi Sturzo alikazia umuhimu wa majadiliano unaomwilishwa katika medani mbali mbali za maisha ya watu, kwa kuzingatia ukweli na uwazi. Majadiliano yakuze moyo wa watu kukutana, kujadiliana pamoja na kushirikiana na watu wote wenye mapenzi mema. Lengo ni kujenga utamaduni wa watu kukutana na kusaidiana katika maisha! Baba Mtakatifu anasema, imegota miaka 100 tangu Wakatoliki walipozama katika maisha ya kisiasa nchini Italia. Hii ni fursa ya kutafakari dhana ya uelewa wa maisha ya kijamii yanayorutubishwa kwa Sheria ya upendo kwa Mungu na jirani. Hii ni fursa kwa waamini walei kutekeleza dhamana na wajibu wao wa kiraia kadiri ya mwanga wa Mafundisho Jamii ya Kanisa kama njia ya kuyatakatifuza malimwengu na kielelezo cha upendo wa Mungu unaomwilishwa katika maisha ya watu!

Sheria ya upendo wa Kikristo ni dira na mwongozo katika maisha na utume wa Kanisa, katika familia na katika kukuza na kudumisha uhusiano na mafungamano ya kijamii. Katika muktadha huu, siasa inaonekana kuwa ni huduma ya upendo kwa watu wa Mungu na wala si kichaka cha rushwa na ufisadi wa mali ya umma; siasa kama jukwaa linalowashirikisha watu kupanga, kuamua na kutekeleza hatima ya maisha yao, ili kuleta: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Upendo kwa jirani uwe ni dira na mwongozo muhimu kwa wanasiasa unaomwilishwa katika matendo na kweli! Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, maisha ya kisiasa hayana budi kuongozwa na kanuni maadili na mshikamano, ili kuweza kuunganisha fadhila ya kimungu, maisha ya kiroho na yale ya kijamii!

Katika maisha na utume wake, Mtumishi wa Mungu Padre Lugi Sturzo amekuwa kweli ni chombo na shuhuda wa kuragibisha tunu msingi za Kikristo katika maisha ya kijamii na mtetezi mahiri wa uhuru wa kiraia. Ni mfano bora wa kuigwa katika maisha, mafundisho na wito wake wa Kipadre, kwani alikuwa mwaminifu katika kufundisha na kushuhudia misingi ya haki na wajibu wa waamini walei kushiriki katika masuala ya kisiasa na kijamii mintarafu mwanga wa Mafundisho Jamii ya Kanisa. Hii ni sehemu ya mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji mtu mzima: kiroho na kimwili! Huu ni msimamo ambao ameutetea kwa hali na mali, kwa kukazia uhuru, demokrasia na kama kielelezo cha huduma ya ukweli, utume ambao ameutekeleza kwa muda wa miaka 60 ya uhai wake!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Mtumishi wa Mungu Padre Lugi Sturzo alikuwa ni shuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo. Kipaumbele cha kwanza ni utu, heshima na haki msingi za binadamu; tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; umiliki wa mali na kazi kama sehemu ya haki msingi za binadamu pamoja na umuhimu wa ujenzi wa amani kwa jumuiya ya Kimataifa. Hizi ni tunu msingi za maisha ya Kikristo ambazo zinapaswa kumwilishwa katika historia, ili kuwasaidia watu kufiriki na kutenda mintarafu kanuni maadili katika maisha. Baba Mtakatifu anawataka waamini walei kushiriki na kuwajibika kikamilifu katika maisha ya kisiasa; daima wakiendelea kusoma alama za nyakati kadiri ya mwanga wa Injili, ili kutekeleza sera na mikakati ya kisiasa inayochota uzoefu wake kutoka katika imani na amri ya upendo kwa Mungu na jirani. Vijana wanapaswa kushirikishwa katika masuala ya kisiasa na kijamii. Mwishoni, amewatakia wajumbe wote tafakari ya kina itakayoweza kuzaa matunda mengi na yanayodumu.

Papa. Don Sturzo
19 June 2019, 10:51