Askofu mkuu Lèon Kalenga Badikebele, Balozi wa Vatican nchini Argentina amefariki dunia tarehe 12 Juni 2019 Askofu mkuu Lèon Kalenga Badikebele, Balozi wa Vatican nchini Argentina amefariki dunia tarehe 12 Juni 2019 

TANZIA: Askofu mkuu Lèon k. Badikebele amefariki dunia!

Askofu mkuu Kalenga Badikebele alizaliwa kunako tarehe 17 Julai 1956 nchini DRC. Akapewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 5 Septemba 1982. Alianza utume wake wa kidiplomasia mjini Vatican tarehe 27 Februari 1990. Akateuliwa kuwa Askofu mkuu na kuwekwa wakfu mwaka 2008 na mwaka 2013 akateuliwa kuwa Balozi wa Vatican nchini Argentina. Tarehe 12 Juni 2019 amefariki dunia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi, 13 Juni 2019, amekutana na kuzungumza na Mabalozi wa Vatican kutoka katika nchi 103; kati yao kuna Mabalozi 98 na wengine 5 ni Wawakilishi wa Kudumu wa Vatican kwenye Mashirika ya Umoja wa Mataifa. Mkutano huu ni sehemu ya mchakato wa utekelezaji wa malengo ya Baba Mtakatifu anayetaka kuimarisha ari, umoja na mafungamano miongoni mwa wawakilishi wa Vatican sehemu mbali mbali za dunia!

Baba Mtakatifu ameuanza mkutano huu kwa kumkumbuka na kumwombea Askofu mkuu Léon Kalenga Badikebele, aliyekuwa Balozi wa Vatican nchini Argentina ambaye amefariki dunia, tarehe 12 Juni 2019 huko Argentina. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Kalenga Badikebele alizaliwa kunako tarehe 17 Julai 1956 huko Kamina, nchini DRC. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 5 Septemba 1982 na kuingizwa Jimboni Luebo, DRC. Alianza utume wake wa kidiplomasia mjini Vatican tarehe 27 Februari 1990. Tangu wakati huo, akatumwa kutekeleza dhamana na utume huu huko nchini Haiti, Guatemala, Zambia, Misri, Zimbabwe na Japan kwa nyakati mbali mbali.

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, tarehe 1 Machi 2008 akamteuwa kuwa Askofu mkuu na hatimaye, kuwekwa wakfu Mei Mosi, 2008 na Kardinali Tarcisio Bertone, aliyekuwa Katibu mkuu wa Vatican kwa wakati ule na kutumwa kwenda nchini Ghana kama Balozi wa Vatican. Tarehe 22 Februari 2013, akateuliwa kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini El Salvador, Belize na Antilles. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 17 Machi 2018 akatemteua kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Argentina. Apumzike katika usingizi wa amani na astahilishwe kupokea tuzo ya maisha na uzima wa milele kwa mafumbo aliyokuwa anaadhimisha!

Papa: Askofu mkuu Leon
13 June 2019, 16:11