Papa Francisko: Pyaisheni mshikamano wa kimataifa kwa kukazia kanuni auni ili kulinda: Utu, heshima, ustawi, mafao ya wengi; utunzaji wa mazingira pamoja na kudumisha amani duniani. Papa Francisko: Pyaisheni mshikamano wa kimataifa kwa kukazia kanuni auni ili kulinda: Utu, heshima, ustawi, mafao ya wengi; utunzaji wa mazingira pamoja na kudumisha amani duniani. 

Papa Francisko: Pyaisheni: Kanuni auni & Mshikamano wa kimataifa!

Mafundisho Jamii ya Kanisa kama njia ya kukabiliana na changamoto mamboleo. Baba Mtakatifu Francisko anawasihi wajumbe wa Taasisi ya Kipapa ya Sayansi Jamii kushirikiana naye, ili kuweza kupyaisha tena mshikamano wa kimataifa, unaoheshimu utu wa binadamu, ustawi na mafao ya wengi; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na amani duniani!

Na Padre richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Professa Stefano Zamagni, Rais wa Taasisi za Kipapa za Sayansi Jamii anasema, kuanzia Mei Mosi, hadi tarehe 3 Mei 2019 Taasisylake inafanya mkutano wa mwaka, kwa kuangalia changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza sehemu mbali mbali za dunia, ili kulinda na kudumisha haki jamii, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kama sehemu ya mkutano huu, Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 2 Mei 2019 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Taasisi hii ya Kipapa ya Sayansi jamii kuhusu changamoto zinazokwamisha ushirikiano katika Jumuiya ya Kimataifa, kiasi hata cha nchi husika kujikuta zinashindwa kulinda ustawi na maendeleo ya wengi.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Laudato si”  yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” anabainisha changamoto zinazoendelea kuikabili Jumuiya ya Kimataifa kwa wakati huu: Maendeleo fungamani, amani, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, athari za mabadiliko ya tabianchi, umaskini, vita, wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi, biashara ya binadamu na viungo vyake; umuhimu wa kusimammia ustawi na mafao ya wengi pamoja na changamoto ya mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo!

Utambulisho wa taifa lolote lile haufumbatwi katika eneo, sheria au maisha ya wananchi wake. Mama Kanisa katika maisha na utume wake anasema Baba Mtakatifu anawahimiza watoto wake kukazia upendo kwa ndugu zao, nchi zao, tamaduni, mila na desturi njema zinazokita mizizi yake katika maisha yao. Kanisa linakataza tabia zote za kibaguzi, chuki na uhasama; utaifa usiokuwa na mashiko na ukatili dhidi ya Wayahudi. Kwa bahati mbaya, haya ni mambo ambayo yameanza kufumuka na kuibuka upya sehemu mbali mbali za dunia. Kuna wimbi kubwa la chuki na ubaguzi dhidi ya wakimbizi na wahamiaji; utaifa wa kupindukia unaokinzana na mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa.

Chuki hizi zinaanza pia kujipenyeza katika Mashirika ya Kimataifa ambayo yanapaswa kuwa ni mahali pa majadiliano na watu kukutana, kwa kuheshimiana na kuthaminiana ili kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu na fungamani ya binadamu. Huduma kwa binadamu, ustawi na maendeleo ya wengi, haki na amani ni mambo msingi yanayopaswa kutolewa na Serikali. Mambo haya yanaposhindwa kutekelezwa kutokana masilahi ya watu wachache, faida kubwa ya kiuchumi, ukabila, dhuluma na nyanyaso, matokeo yake ni wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani. Sera na mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji kwa wakimbizi na wahamiaji unaotekelezwa na Kanisa Katoliki unajikita katika: kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwashirikisha katika maisha ya nchi inayowapokea.

Wahamiaji wanapaswa kutambuliwa, ili kupewa fursa ya kuchangia katika ustawi na maendeleo ya Jumuiya inayowakarimu. Mataifa mengi ni matunda ya mwingiliano wa wahamiaji na wakimbizi kutoka sehemu mbali mbali za dunia, changamoto ya kuendelea kujenga umoja hata katika tofauti msingi; kwa kukazia tamaduni, mila na desturi njema. Tabia ya baadhi ya serikali kuwahamasisha wananchi wake kuwachukia watu wengine ni mwelekeo potofu na ni hatari sana kwa mustakabali wa Jumuiya ya Kimataifa.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia kuna haja kwa nchi mbali mbali kushirikiana katika masuala ya kiuchumi, kiteknolojia na kitamaduni kwa kuhakikisha kwamba, utajiri na rasilimali ya dunia, vinatumika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya binadamu wote. Kwa njia hii, Jumuiya ya Kimataifa itaweza kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi, mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo sanjari na ukosefu wa amani duniani!

Kanuni auni isaidie kukoleza ushirikiano na mshikamano katika Jumuiya ya Kimataifa, kwa kuendelea kuimarisha sera, mikataba na itifaki mbali mbali zilizowekwa na Jumuiya ya Kimataifa, kama ilivyo kwa Jumuiya ya Ulaya na Ushirikiano wa Nchi za Amerika ya Kusini. Kwa njia ya mshikamano huu, Jumuiya ya Kimataifa itaweza kufyekelea mbali: vita, ukoloni wa kiitikadi, kiuchumi na baadhi ya mataifa kujisikia kuwa na nguvu kiasi cha kutishia usalama wa nchi nyingine duniani. Katika mwelekeo kama huu, utandawazi unaweza kuonekana kuwa ni dhana hatari kabisa na matokeo yake ni baadhi ya mataifa kuanza kujihami, pamoja na hatari ya amani na maridhiano kati ya watu kuanza kuporomoka!

Baba Mtakatifu anasema, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika kujenga matumaini badala ya kueneza chuki na uhasama; majadiliano na maridhiano, kwani wote ni binadamu wanaoishi katika nyumba ya wote. Haki na wajibu vidumishwe; utu, heshima na haki msingi za binadamu viendelezwe badala kueneza ukononi wa kiitikadi. Jumuiya ya Kimataifa iwaangalie wanyonge na maskini zaidi. Huu ni wajibu wa kuendelea kuimarisha utafiti kwa mambo yanayo waunganisha watu; ushirikiano na mshikamano, ili kupambana na changamoto mamboleo za biashara ya binadamu na viungo vyake, mifumo ya utumwa mamboleo, na hatimaye kudumisha ustawi wa jamii na amani.

Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kuendeleza mchakato wa kupiga rufuku utengenezaji, usambazaji na matumizi ya silaha za kinyuklia, kwani hali kama ilivyo kwa sasa inaonesha kwamba, maamuzi yaliyokuwa yamefikiwa miaka kadhaa sasa yamekwama, kiasi cha kuanza kuhisi tishio la kuibuka kwa vita; matumizi mabaya ya teknolojia. Kuna mataifa yanayotaka kujihami kwa kuweka silaha za kinyuklia si tu ardhini, bali hata angani, tishio kwa usalama wa kimataifa! Mataifa yanapaswa kuwajibika, kwa kujikita katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kimataifa, licha ya kila taifa kuendelea kuwa na utambulisho wake.

Mwishoni mwa hotuba yake ambayo imegusia mambo msingi katika Mafundisho Jamii ya Kanisa, Baba Mtakatifu Francisko amewataka wajumbe wa Taasisi ya Kipapa ya Sayansi Jamii kushirikiana naye, ili kuweza kupyaisha tena mshikamano wa kimataifa, unaoheshimu utu wa binadamu, ustawi na mafao ya wengi; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na amani duniani!

Papa: Sayansi Jamii
02 May 2019, 16:28