Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 6 Aprili 2019 amekutana na kuzungumza na wanafunzi pamoja na waalimu wa Taasisi ya San Carlo, Milano, Italia. Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 6 Aprili 2019 amekutana na kuzungumza na wanafunzi pamoja na waalimu wa Taasisi ya San Carlo, Milano, Italia. 

Papa Francisko. dhamana na wajibu wa walezi na waalimu!

Baba Mtakatifu Francisko amegusia kuhusu fumbo la mateso na mahangaiko ya watu wasiokuwa na hatia; huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka kwa waja wake; dhamana na wajibu wa waalimu na walezi katika majiundo ya vijana wa kizazi kipya! Upendo na mshikamano kati ya watu wa Mataifa; Utamaduni wa kukutana na kusaidiana; Uwepo na ukaribu wa wazazi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 6 Aprili 2019 amekutana na kuzungumza na waalimu pamoja na wanafunzi wa Taasisi ya San Carlo, iliyoko Milano, Kaskazini mwa Italia. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kujibu maswali makuu manne kutoka kwa wanafunzi na waalimu wao kwa kukazia: huruma na upendo wa Mungu ni kwa watu wote pasi na ubaguzi; Umuhimu wa kukuza na kudumisha utamaduni wa watu kukutana na kujadiliana katika ukweli na uwazi; Dhamana na utume wa walezi na waalimu katika sekta ya elimu kwa ajili ya kukuza na kudumisha: ustawi, maendeleo na mafao ya wanafunzi wao na mwishoni, amewataka waalimu na wanafunzi kuwa ni Mitume; vyombo vya ujenzi wa amani na utulivu kuanzia kwenye familia.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwa kusema kwamba, huruma na upendo wa Mungu unawaambata na kuwafumbata wote pasi na ubaguzi, ndivyo inavyopaswa kuwa hata katika Kanisa na Jamii katika ujumla wake, bila ya baadhi ya watu kutaka kujikuza na kuwatweza wengine. Huruma na upendo huu, umefunuliwa kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, ili kumwokoa binadamu kutoka katika utumwa wa dhambi na mauti! Kifo cha Msalaba ni ukatili wa hali ya juu kabisa, changamoto na mwaliko wa kuona na kuguswa na mahangaiko ya wengine wanaoteseka kutokana na vita na ukosefu wa haki msingi za binadamu! Yote haya yawakumbushe waamini kuhusu fumbo la mateso na mahangaiko ya binadamu, ambalo wakati mwingine halina majibu muafaka.

Mama Kanisa anawakirimia watoto wake Kipindi cha Kwaresima, ili kutafakari kuhusu mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu, uletao uzima na maisha ya milele! Ukosefu wa haki, uwepo wa dhambi na ubaya wa moyo, vitaendelea kumwandama mwanadamu, lakini ikumbukwe kwamba, yote haya Kristo Yesu ameyashinda kwa mateso, kifo na ufufuko wake! Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa kukuza na kudumisha utamaduni wa watu kukutana na kujadiliana katika ukweli na uwazi; kwa kujenga na kudumisha dhamiri safi na nyofu. Huu ni mwaliko wa kuondokana na tabia ya ukatili na unyama, hali ya kutojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine, uchoyo na ubinafsi wa kutupwa! Watu wakumbuke kwamba, wanategemeana na kukamilishana. Mfuasi amini wa Kristo Yesu ni yule anayekita maisha yake katika: ukarimu, majadiliano na ushuhuda unaomwilishwa katika huruma, haki na upendo.

Vijana wajifunze kukuza na kudumisha kanuni maadili na utu wema, kwa kumpatia Kaisari yale yaliyo ya Kaisari na ya Mungu apewe Mungu. Watu watambue tofauti zao msingi na waheshimiane na kuthaminiana kwani wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu! Imani kwa Kristo Yesu ni sehemu ya ushuhuda unaopaswa kutolewa na waamini kwa kuambata na kukumbatia tunu msingi za maisha ya Kikristo bila kutafuta wongofu wa shuruti ambao hauna mashiko wala mvuto katika maisha na utume wa Kanisa! Utamaduni wa majadiliano katika ukweli ni mchakato wa kuwatambua na kuwaheshimu wengine; kwa kusikilizana na kusaidiana katika safari ya maisha, ili kuondokana na tabia ya kutaka kuwaveza na kuwatweza watu wengine katika jamii, hasa zaidi wakimbizi na wahamiaji. Jamii ijenge Jumuiya inayosimikwa katika kumbu kumbu endelevu, ili kudumisha haki, upendo na mshikamano wa kweli!

Baba Mtakatifu amegusia pia kuhusu dhamana na utume wa walezi na waalimu katika sekta ya elimu kwa ajili ya kukuza na kudumisha: ustawi, maendeleo na mafao ya wanafunzi wao. Hii ni huduma inayofumbatwa katika sadaka na majitoleo binafsi; kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa majadiliano; kwa kushiriki na kushikamana na wanafunzi katika uhalisia wa maisha yao, ili kung’amua matatizo, changamoto na fursa walizo nazo katika maisha, ili kuwajengea leo na kesho iliyo bora zaidi. Pale panazokuka matatizo, waalimu wawe wepesi kuyabaini na kutoa vigezo msingi vya kufuata na kwamba, uwepo wao kati pamoja na wanafunzi, iwe ni sehemu ya mchakato wa malezi na makuzi, kielelezo cha Baba, Mama na Kaka mkubwa!

Mwishoni mwa majibu yake, Baba Mtakatifu Francisko, amewataka waalimu na wanafunzi kuwa ni Mitume, Mashuhuda na vyombo vya ujenzi wa amani na utulivu kuanzia kwenye familia, daima wakiwa wameungana na Kristo Yesu, kwani katika imani, yote yanawezekana! Wajenge utamaduni wa sala na ushiriki mkamilifu katika Sakramenti za Kanisa, hasa Ekaristi Takatifu na Upatanisho, ili kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao! Wazazi na walezi wakuze Injili ya huruma na upendo kwa watoto wao! Wawe mstari wa mbele kuwarithisha tunu msingi za Kiinjili, kanuni maadili na utu wema! Wawe Makatekista wa kwanza katika imani, matumaini na mapendo kwa njia ya ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo! Wazazi na walezi, wawe ni washauri bora wa watoto wao, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali bora zaidi pa kuishi; mahali ambapo udugu wa kibinadamu, haki, amani, ukweli na uwazi, vinapata maskani katika maisha ya binadamu!

Papa: San Carlo
06 April 2019, 15:56