Nia za Papa Francisko kwa Mwezi Machi 2019: Ni kwa ajili ya Wakristo wanaoteswa na kunyanyaswa kutokana na imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake! Nia za Papa Francisko kwa Mwezi Machi 2019: Ni kwa ajili ya Wakristo wanaoteswa na kunyanyaswa kutokana na imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake! 

Nia za Papa Francisko Mwezi Machi 2019: Wakristo wanaoteswa!

Baba Mtakatifu katika nia zake za jumla kwa mwezi Machi, anasisitiza kwamba, watu hawa wana nyanyaswa na kudhulumiwa kwa sababu wanasema ukweli; wanamtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu katika jamii ile. Hata katika Makanisa yaliyobomolewa bado kuna watu wanaendelea kusali Rozari takatifu muhtasari wa huruma na upendo wa Mungu katika maisha ya mwanadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Wakati mwingine si rahisi sana watu kuamini kwamba, kwa sasa kuna idadi kubwa ya wafiadini na waungama imani, pengine hata ilivyokuwa kwenye Karne ya kwanza ya Ukristo. Hawa ni watu wanaohisi uwepo wa Kristo karibu yao na kwamba, kuna haja ya kutambua na kuheshimu haki zao msingi. Hivi ndivyo anavyosema Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake wa Video kwenye Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa unaoweza kupatikana kwa kufuata anuani ifuatayo: www.thepopevideo.org.

Baba Mtakatifu katika nia zake za jumla kwa mwezi Machi, 2019 anasisitiza kwamba, watu hawa wana nyanyaswa na kudhulumiwa kwa sababu wanasema ukweli; wanamtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu katika jamii yao. Hata katika Makanisa yaliyobomolewa kwa mtutu wa bunduki, bado kuna watu wanaendelea kusali Rozari takatifu muhtasari wa huruma na upendo wa Mungu katika maisha ya mwanadamu! Dhuluma na nyanyaso zinatendeka mahali ambapo hakuna uhuru wa kidini wala uhuru wa kuabudu. Matokeo yake ni “mkongo’oto mkali unaotolewa na askari na watu kulazimika kuzikimbia nchi na makazi yao.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, nyanyaso na dhuluma za kidini zinatendeka hata katika nchi zile ambazo kinadharia zinalinda na kuheshimu uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini. Katika hali na mazingira kama haya kuna haja ya kuendelea kusali, ili uhuru wa kidini uweze kupatikana na watu wapate fursa ya kufuata dhamiri zao nyofu!

Papa: Nia ya Sala
14 March 2019, 11:33