Vatican News
Kituo cha Utalii wa Vijana Nchini Italia kinaadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwake! Kituo cha Utalii wa Vijana Nchini Italia kinaadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwake! 

Papa Francisko: Utalii uwe ni daraja la kuwakutanisha watu!

Watu wajifunze utamaduni wa kulinda na kutunza mazingira; wafurahie uzuri wa kazi ya uumbaji na kujizatiti kuifahamu, kuitunza na kuiendeleza. Hii ndiyo njia muafaka ya kufanya “Utalii wa mwendo pole” ili kuendeleza uzuri, uzoefu na mshikamano. Kituo hiki kimechagua Kobe kama alama ya utambulisho wao. Kobe analeta mvuto ni mwaminifu na anayapenda sana mazingira.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kituo cha Utalii wa Vijana nchini Italia kinaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwake, mchango mkubwa uliotolewa na Padre Carlo Carretto, muasisi wa Chama cha Vijana Nchini Italia. Katika uhai wake, Chama hiki kimekuwa ni chemchemi ya utajiri wa kitamaduni na kijamii; na ambacho kimewashirikisha watu na kuwapatia mwono halisi wa binadamu: kiroho na kimwili, chachu makini ya mageuzi ya kijamii. Mtu mzima ni dhana inayomwangalia binadamu katika mahitaji yake halisi, yanayomchangamotisha kufanya upembuzi yakinifu, ili kutambua mambo mapya yanayomzunguka; mawasiliano na jirani zake, tamaduni pamoja na matatizo yanayojitokeza katika ulimwengu mamboleo! Haya ndiyo mambo msingi yanayoendelezwa na kukuzwa na Kituo cha Utalii wa Vijana Nchini Italia katika sekta ya utalii. Lengo ni kuwakutanisha watu, ili waweze kufahamiana na kuheshimiana.

Huu ni mwaliko wa kuthamini mambokale, historia na watu wanaoishi katika miji hii pamoja na changamoto zao katika maisha. Watu wajifunze utamaduni wa kulinda na kutunza mazingira; wafurahie uzuri wa kazi ya uumbaji na kujizatiti kuifahamu, kuitunza na kuiendeleza. Hii ndiyo njia muafaka ya kufanya “Utalii wa mwendo pole” ili kuendeleza uzuri, uzoefu, mshikamano na mafungamano. Ndiyo maana Kituo hiki kimechagua Kobe kama alama ya utambulisho wao kwa Mwaka 2019. Kobe analeta mvuto ni mwaminifu na anayapenda sana mazingira. Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 22 Machi 2019 alipokutana na kuzungumza na Kituo cha Utalii wa Vijana nchini Italia, kinapoadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwake.

Utalii wa mwendo pole unajikita katika elimu ya utamaduni na mazingira; unasaidia watu kuishi kwa umakini zaidi kwa kufanya kazi kwa bidii, juhudi na maarifa. Dhamana ambayo inapaswa kutekelezwa kwa dhati, ili kutumia vyema muda binafsi kwa furaha na kujisadaka zaidi! Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, kuna vijana ambao wamekata tamaa katika maisha ya leo na kesho iliyo bora zaidi pengine kutokana na mazingira waliomo, kiasi kwamba, wanashindwa kutubutu kupambana na hali pamoja na mazingira yao. Kituo cha Utalii wa Vijana nchini Italia, kiwe ni msaada kwa vijana kama hawa, kwa kuwaonesha mifano bora ya kuigwa, ili waweze kuwa na matumizi bora ya muda binafsi, kwa kukutana na vijana wengine; ili kujenga urafiki na kukuza tunu msingi za maisha ya kiutu na imani.

Kituo hiki kinatambulikana na kuthaminiwa na Serikali pamoja na watu maarufu kutokana na mchango wake katika ujenzi wa ukarimu katika jamii. Kanisa linakiangalia Kituo hiki kwa matumaini na kuendelea kutoa mwaliko kwa vijana kushuhudia ukatoliki wao, ili kujisadaka kwa ajili ya jirani, ustawi na mafao ya wengi. Kumbu kumbu ya Miaka 70 si haba kama kiatu cha raba wanasema Waswahili! Ni muda muafaka wa kutambua utume wake ndani ya Kanisa na familia ya binadamu katika ujumla wake. Ni mwaliko wa kulinda na kuhifadhi amana na utajiri wake maisha ya kiroho pamoja na mfano wa Muasisi wa Chama chao. Wajitahidi kuishi yote katika sala na shukrani kwa Mungu.

Kituo cha Utalii Italia
22 March 2019, 16:54