Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 30-31 Machi 2019 anafanya hija ya kitume nchini Morocco kama hujaji wa amani na udugu! Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 30-31 Machi 2019 anafanya hija ya kitume nchini Morocco kama hujaji wa amani na udugu! 

Hija ya Papa Francisko Morocco 2019: Amani na udugu

Papa Francisko kuanzia tarehe 30-31 Machi 2019 anafanya hija ya kitume nchini Morocco ili kujenga na kudumisha amani na udugu, tema ambazo zinapewa msukumo wa pekee na Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi cha mwaka 2019. Hiki ni kielelezo cha huduma ya mshikamano wa upendo kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kuanzia Jumamosi tarehe 30 hadi Jumapili tarehe 31 Machi 2019 anafanya hija ya 28 ya kimataifa nchini Morocco kwa kuongozwa na kauli mbiu “Papa Francisko mhudumu wa matumaini Morocco 2019”. Hii ni hija inayojikita katika mchakato wa kujenga na kudumisha amani na udugu, tema ambazo zinapewa msukumo wa pekee na Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi cha mwaka 2019. Hiki ni kielelezo cha huduma ya mshikamano wa upendo kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi.

Morocco inakuwa ni nchi 48 kutembelewa na Baba Mtakatifu Francisko katika hija zake za kimataifa hadi wakati huu. Hii ni mara ya tatu kwa Baba Mtakatifu, kuitembelea familia ya Mungu Barani Afrika, akiwa na matumaini kwamba, Mwezi Septemba 2019 atapata pia nafasi ya kutembelea Msumbiji, Madagascar pamoja na Mauritius. Majadiliano ya kidini kati ya waamini wa dini mbali mbali ni nyenzo msingi ya kupambana na tabia ya ubinafsi, misimamo mikali ya kidini na kiimani, ili kujenga na kudumisha umoja, upendo, mshikamano na maridhiano kati ya watu, kila mtu akipewa nafasi ya kushuhudia imani yake! Hii ni changamoto inayowataka waamini kujikita katika mchakato wa kulinda na kudumisha misingi ya amani, kwa kuheshimiana na kuthaminiana.

Waamini watambue kwamba, wana wajibu wa kulinda uhai, kukuza na kudumisha uhuru wa kuabudu pamoja na kujikita katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Kumbe, katika mchakato wa majadiliano ya kidini, Wakristo wanapaswa kumuungama Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, chanzo cha imani, furaha na matumaini kwa waja wake. Baba Mtakatifu anasema, Mwenyezi Mungu ni kiini cha majadiliano na watu wake na kamwe hajaacha kuzungumza na wanawadamu katika safari ya maisha yao hapa duniani, kama ilivyokuwa kwenye Agano la Kale hata leo hii, Mwenyezi Mungu anazungumza na binadamu kwa njia ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Kristo ni ufunuo wa huruma na upendo wa Baba wa milele, aliyetumwa kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, ili kumshirikisha maisha ya uzima wa milele!

Baba Mtakatifu katika majadiliano ya kidini anakazia: Umuhimu wa kuzima kiu ya amani duniani, kwa kuitafuta, kuidumisha na kuhakikisha kwamba, waamini wanakuwa ni vyombo vya amani duniani vinavyofumbatwa katika udugu wa kibinadamu: Familia ya binadamu na ujasiri wa kuwathamini wengine; Majadiliano ya kidini na sala; elimu na haki; pamoja na udugu kama Sanduku la Agano na maendeleo fungamani. Morocco ni nchi ambayo imeendeleza mchakato wa maridhiano kati ya waamini wa dini mbali mbali kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa vijana nchini humo! Morocco ni kati ya nchi ambazo zinadumisha tunu msingi za maisha ya kifamilia zinazobainishwa Kikatiba. Imeendelea kupambana na umaskini wa hali na kipato vijijini na kwamba, wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji ni kati ya changamoto kubwa nchini Morocco.

Morocco pia ni nchi ambayo iko mstari wa mbele katika masuala ya kimataifa! Itakumbukwa kwamba, Mkutano wa kimataifa kuhusu mazingira nchini Morocco, COP22 ulifanyika mwaka 2016, kama sehemu ya kuanza utekelezaji wa Itifaki ya utunzaji bora wa mazingira iliyopitishwa mjini Paris, Ufaransa kunako mwaka 2015. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwenye mkutano huu alisema, athari za mabadiliko ya tabianchi zinahitaji uwajibikaji wa pamoja, ili kushiriki kikamilifu katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Huu ni wajibu wa kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inatumia kikamilifu maendeleo ya sayansi na teknolojia ili kudhibiti kikamilifu athari za mabadiliko ya tabianchi sanjari na kutumia nguvu kwa ajili ya mchakato mbadala wa maendeleo endelevu na bora zaidi, unaojikita katika tunu za kiutu na kijamii. Lengo ni kuhakikisha kwamba, uchumi wa dunia unakuwa ni kwa ajili ya huduma kwa binadamu, ili hatimaye, kujenga msingi wa haki na amani, ili kulinda na kutunza mazingira, nyumba ya wote.

Kunako Desemba 2018, Jumuiya ya Kimataifa ilifanya mkutano wake huko Marrakesh, Morocco, kuhusu Mkataba wa “Global Compact 2018” yaani “Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji 2018” ili kuhakikisha kwamba, mchakato wa uhamiaji unakuwa salama, wenye kuratibiwa na kuzingatia sheria na kanuni za Umoja wa Mataifa. Kumbe, changamoto ya wakimbizi na wahamiaji ni kati ya vipaumbele vya kwanza katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko. Hija hii ni mwendelezo wa hija ya kitume iliyofanywa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1985 wakati wa Maadhimisho ya Mwaka wa Vijana Duniani alipowakutanisha vijana wa dini mbali mbali  huko Casablanca, nchini Morocco. Mtakatifu Yohane Paulo II aliwataka vijana kukuza na kudumisha mambo msingi yanayowaunganisha kama waamini wanaosadiki katika imani kwa Mungu mmoja na kwamba, wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Mtakatifu Yohane Paulo II alikaza kusema, Kanisa linataka kuendelea kushuhudia imani, kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kidugu na kwamba, linawataka vijana kuwa kweli ni mashuhuda wa furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa. Vijana wanapaswa kuwa kweli ni vyombo vya haki na amani; uhuru, kanuni maadili na utu wema, huku wakiendeleza majadiliano ya kidini, ili kujenga umoja na udugu wa watu wa Mungu. Majadiliano ya kidini yakite mizizi yake katika huduma kwa watu wa Mungu nchini Morocco, ili kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa! Majadiliano ya kidini yawasaidie waamini wa dini mbali mbali kutambua amana na utajiri unaofumbatwa katika maisha yao, pamoja na kushirikiana na wazee, kwani wanategemeana na kukamilishana. Waamini wawe ni mashuhuda na vyombo vya tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu; kwa kukazia: maisha ya sala, toba na kufunga; sadaka na matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Yote haya yanawezekana, ikiwa kama waamini wateheshimiana na kuthaminiana kama ndugu wamoja!

Papa: Morocco 2019
29 March 2019, 09:13