Papa Francisko tarehe 19 Machi 2019 anaadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 6 tangu alipoanza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro: Vipaumbele: Maskini, Amani na Mazingira. Papa Francisko tarehe 19 Machi 2019 anaadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 6 tangu alipoanza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro: Vipaumbele: Maskini, Amani na Mazingira. 

Papa Francisko Miaka 6 ya Utume: Maskini, Amani na Mazingira

Tarehe 19 Machi 2019, Baba Mtakatifu Francisko anaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 6 tangu alipoanza rasmi utume wake kwa kama Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa kujikita katika mambo makuu matatu: Maskini, Amani na Mazingira. Hizi ni amana na urithi mkubwa kutoka kwa Mtakatifu Francisko wa Assisi. Baba Mtakatifu anasema, maskini ni amana na utajiri wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 19 Machi 2019 anaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 6 tangu alipoanza rasmi utume wake kwa kama Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa kujikita katika mambo makuu matatu: Maskini, Amani na Mazingira. Hizi ni amana na urithi mkubwa kutoka kwa Mtakatifu Francisko wa Assisi. Baba Mtakatifu anasema, maskini ni amana na utajiri wa Kanisa. Ili kuwaenzi maskini duniani, ameanzisha Siku ya Maskini Duniani inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo Jumapili ya 33 ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa.

Baba Mtakatifu ameanzisha Idara ya Wakimbizi na Wahamiaji chini ya Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu. Kuhusu huduma kwa wakimbizi na wahamiaji, Kanisa linakazia mambo makuu manne: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowakirimia. Huduma kwa wakimbizi na wahamiaji ni changamoto changamani katika maisha na utume wa Kanisa kwa nyakati hizi!

Upendeleo kwa Maskini: Siku ya Maskini Duniani ni matunda ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu na kwa mara ya kwanza imeadhimishwa kunako mwaka 2017. Siku ya Maskini Duniani ni fursa ya kushikamana kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana na kusaidiana, kama alama ya: urafiki, umoja na udugu unaovunjilia mbali kuta za utengano kwa sababu mbali mbali. Baba Mtakatifu anasema, Kanisa daima limekuwa likisikiliza na kujibu kilio cha maskini na wahitaji kama inavyoshuhudiwa kwenye Kitabu cha Matendo ya Mitume, kwa kuwachagua Mashemasi saba walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho na hekima, ili waweze kutoa huduma kwa maskini, hii ni alama ya kwanza ya huduma kwa maskini kutokana na utambuzi kwamba, maisha ya Kikristo yanafumbatwa katika udugu na mshikamano. Yesu mwenyewe aliwapatia maskini kipaumbele cha kwanza katika Heri za Mlimani kwa kusema, “Heri maskini, maana hao watairithi nchi”. Jumuiya ya kwanza ya Wakristo iliuza mali na vitu vyake na kuwagawia watu kadiri ya mahitaji yao!

Mtakatifu Francisko wa Assisi ni kati ya mifano bora ya kuigwa katika huduma ya ukarimu na upendo kwa maskini, hakuridhika kuukumbatia umaskini na kutoa sadaka kwa wakoma, bali aliamua kwenda kuishi pamoja nao kule Gubbio na huko akamwongokea Mungu na kuonja huruma yake iliyomletea mageuzi makubwa katika maisha yake; mageuzi yaliyojikita katika upendo, mtindo wa maisha ya Wakristo! Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujenga utamaduni wa kukutana na kushirikishana na maskini huruma na upendo wao, hali ambayo inapaswa kuwa ni mtindo wa maisha ya Kikristo. Hija ya maisha ya mwamini katika sala, toba na wongofu wa ndani inafumbatwa katika huduma makini kwa maskini kama njia ya kukutana uso kwa uso na Fumbo la Mwili wa Kristo, unaonyanyasika kutokana na umaskini, kama wakati ule wa kupokea Fumbo la Ekaristi Takatifu.

Sababu za umaskini duniani: Kuna mambo mengi yanayochangia kuenea kwa umaskini duniani unaoendelea kujionesha katika nyuso za watu mbali mbali wanaoteseka na kunyanyaswa kutokana na vita, ghasia na machafuko ya kijamii; wanafungwa bila kuhukumiwa! Ni watu wanaonyimwa uhuru na utu wao; wanateseka kwa ujinga, magonjwa, ukosefu wa fursa za ajira, mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo; wanalazimika kukimbia na kuishi uhamishoni; ni watu wanaoteseka na umaskini wa hali na mali; wanalazimika kukimbia nchi zao.

Umaskini unajionesha katika sura ya watu wanaoteseka na kunyanyaswa utu na heshima yao kutokana na utawala dhalimu na uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka. Umaskini ni matokeo ya ukosefu wa haki jamii; mmong’onyoko wa tunu msingi za kimaadili; chuki na uhasama pamoja na hali ya kutowajali wengine. Baba Mtakatifu anakaza kusema, maskini si tatizo bali ni rasilimali na amana inayowasaidia waamini kupokea na kuishi misingi ya Injili!

Utunzaji Bora wa Mazingira nyumba ya Wote! Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni sehemu ya Injili ya kazi ya Uumbaji, kielelezo makini cha umoja na mafungamano ya kijamii kati ya binadamu. Haya ni mafungamano yanayojikita katika:Uhusiano na Mwenyezi Mungu, Jirani na Dunia yenyewe. Haya ni mambo yanayofafanuliwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume, “Laudato si” yaani yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Mwanadamu amejeruhiwa kwa dhambi ya asili na matokeo yake yanayojionesha ardhini, majini, hewani na katika aina mbali mbali za mifumo ya maisha sanjari na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Baba Mtakatifu katika Wosia wake wa “Laudato si” anakazia: umuhimu wa kulinda, kutunza na kudumisha mazingira bora; Injili ya Kazi ya Uumbaji; Vyanzo vya mgogoro wa Ekolojia na mahusiano na watu; Ekolojia msingi; Njia za kupanga na kutenda; Elimu ya Ekolojia na maisha ya kiroho!

Injili ya Amani Duniani: Baba Mtakatifu anaendelea kutangaza na kushuhudia Injili ya amani duniani kwa kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene; kwa kukazia utu, heshima na haki msingi za binadamu. Haya ni mambo ambayo anayashuhudia katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro! Injili ya amani ni muhtasari wa upendeleo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Kwani uchafuzi wa mazingira pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi ni chanzo kikuu kinachowatumbukiza watu wengi katika dimbwi la umaskini wa hali na kipato, hali inayotishia amani na mafungamano ya kijamii duniani!

Baba Mtakatifu ana ibada ya pekee kabisa kwa Mtakatifu Yosefu, Baba mlishi wa Yesu pamoja na Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Kila mwaka ifikapo tarehe, 19 Machi, Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Mtakatifu Yosefu, Mume wa Bikira Maria na Msimamizi wa Kanisa la Kiulimwengu. Ni nafasi muafaka ya kumtafakari kwa kina na mapana Mtakatifu Yosefu aliyeonesha na kushuhudia unyenyekevu na hekima ya hali ya juu katika mchakato mzima wa ulinzi na tunza kwa Familia Takatifu. Sherehe ya Mtakatifu Yosefu, inapata chimbuko lake kutoka katika Maandiko Matakatifu.

Mtakatifu Yosefu ni mtu wa mwisho kuzungumza na Mwenyezi Mungu kwa njia ya maono na ndoto katika Agano Jipya. Yosefu ni mtu mwaminifu na mwenye haki ambaye ameteuliwa na Mwenyezi Mungu kuwa ni mlinzi na msimamizi wa nyumba yake. Yosefu ni kiungo muhimu sana kati ya Kristo Yesu, Masiha na Mkombozi wa dunia, kwani amezaliwa kutoka katika ukoo wa Yakobo na Daudi mtumishi wa Mungu. Yosefu, mtu mwaminifu na mwenye haki, ndiye Mume wake Bikira Maria na Baba Mlishi wa Yesu. Mwenyezi Mungu alimpatia dhamana na wajibu wa kuitunza na kuilinda Familia Takatifu; akamwokoa Mtoto Yesu dhidi ya upanga wa Mfalme Herode kwa kumkimbiza na kumpatia hifadhi nchini Misri na hatimaye, akamrejesha tena kutoka uhamishoni Misri na kutua nanga mjini Nazareti.

Papa Pio IX akamtangaza kuwa msimamizi wa Kanisa la Kiulimwengu. Mtakatifu Yohane XXIII akaingiza jina la Mtakatifu Yosefu katika Kanuni ya Kirumi. Huyu anaitwa mtumishi mwaminifu wa Mungu. Ni uaminifu wake huo ambao unamshirikisha kwa namna iliyositirika katika historia nzima ya wokovu wetu. Matendo yake ya imani, mapendo na matumaini hayadhiiriki kwa wazi sana katika Maandiko Matakatifu lakini ni ya kupewa mkazo wa kipekee, mathalani kwa kuwa mtii katika hali ya ukimya wakati wa kuitikia sauti ya Mungu. Huyu ndiye wakili mwaminifu na mwenye busara. Kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, “ndiyo” ya Mtakatifu Yosefu katika mpango wa ukombozi wa mwanadamu  ndiyo inayompatia ukuu. Huu ni mwanzo wa safari ya utii wa Mtakatifu wa Yosefu katika mpango mzima wa ukombozi wa mwanadamu. Yeye kama Baba mlishi ndani ya Familia Takatifu, anayachukua kikamilifu majukumu yake ya kuwa mlinzi na mtegemezaji wa familia.

Baba Mtakatifu Yohane Paulo II katika Waraka wake wa Kitume,  Redemptoris Custos anaongeza kusema: “Kama vile Mtakatifu Yosefu alivyochukua jukumu la kumtunza kwa upendo Bikira Maria na kwa furaha akajitoa katika kumtunza Yesu Kristo, vivyo hivyo ndiyo anavyolitunza na kuliangalia Fumbo la Mwili wa Kristo, Kanisa ambalo Bikira Maria ni mfano na kielelezo”. Nafasi hii ya Mtakatifu Yosefu inatekelezwa katika hali ya unyenyekevu na ukimya kabisa. Mtakatifu Yosefu anaonesha mfano bora kabisa kwa maisha ya Kikristo.

Daima hakusita kutimiza wajibu wake kama Baba wa familia na kuutekeleza kwa uaminifu mkubwa kabisa hata katika mazingira ambayo yalikuwa ni magumu na tete. Pia alijitoa mhanga kusafiri usiku kucha wakati wakimtorosha Mtoto Yesu ili kuilinda familia hii takatifu ya Mungu na mkono dhalimu wa mfalme Herode. Katika maisha ya familia kule Nazareti aliangaika kama Baba kuitafutia familia mahitaji yake ya kila siku na hii inathibitishwa na jinsi Kristo alivyojulikana kuwa ni “Mwana wa Seremala”. Huu ni mwaliko pia kwa waamini na watu wenye mapenzi mema, kujinyenyekesha mbele ya Mwenyezi Mungu. Ikumbukwe kwamba, fadhila ya unyenyekevu na heshima inayofumbatwa katika maisha ya Mtakatifu Yosefu, Baba Mlishi wa Yesu inaonesha umuhimu wa kujenga na kudumisha majadiliano yanayofumbata: ukweli, ustawi na maendeleo ya wote.  Mtakatifu Yosefu alikuwa daima kwa Yesu mfano na mwalimu wa hekima hii , ambayo ni hurutubishwa kwa Neno la Mungu.

Papa Francisko 6Yrs
19 March 2019, 08:40