Papa Francisko: Udugu ni sanduku la agano na maendeleo fungamani ya binadamu! Papa Francisko: Udugu ni sanduku la agano na maendeleo fungamani ya binadamu! 

Papa Francisko: Udugu ni sanduku la agano na maendeleo fungamani

Papa Francisko amekazia: Umuhimu wa kuzima kiu ya amani duniani, kwa kuitafuta, kuidumisha na kuhakikisha kwamba, waamini wanakuwa ni vyombo vya amani duniani vinavyofumbatwa katika udugu wa kibinadamu: Familia ya binadamu na ujasiri wa kuwathamini wengine; Majadiliano ya kidini na sala; elimu na haki; pamoja na udugu kama Sanduku la Agano na maendeleo fungamani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 4 Februari 2019 ameadhimisha binafsi Ibada ya Misa Takatifu na baadaye, akaenda Ikulu kumtembelea Mfalme Mrithi  Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan huku msafara wake ukisindikizwa na farasi. Baba Mtakatifu amepata mapokezi ya heshima kitaifa. Baadaye jioni, Baba Mtakatifu amekutana kwa faragha na Baraza la Wazee wa Dini ya Kiislam. Hili ni Baraza linaloundwa na wasomi, wazee wenye hekima na busara pamoja na wataalam waliobobea katika medani mbali mbali za maisha, ambao kimsingi, wamejipambanua katika masuala ya haki, uhuru na nidhamu. Hili ni Baraza ambalo lilianzishwa kwa makusudi ya kulinda na kudumisha tunu msingi za kiutu, maadili na imani ya dini ya Kiislam.

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa wajumbe wanaohudhuria Mkutano wa Kimataifa wa majadiliano ya kidini, unaoongozwa na kauli mbiu "Udugu wa kibinadamu” amekazia mambo yafuatayo: Umuhimu wa kuzima kiu ya amani duniani, kwa kuitafuta, kuidumisha na kuhakikisha kwamba, waamini wanakuwa ni vyombo vya amani duniani vinavyofumbatwa katika udugu wa kibinadamu: Familia ya binadamu na ujasiri wa kuwathamini wengine; Majadiliano ya kidini na sala; elimu na haki; pamoja na udugu kama Sanduku la Agano na maendeleo fungamani.

Baba Mtakatifu katika hotuba yake, amewashukuru na kuwapongeza wale wote waliojisadaka bila ya kujibakiza ili kuhakikisha kwamba, mkutano wa majadiliano ya kidini kimataifa unafanikiwa. Imegota miaka 800 tangu Mtakatifu Francisko wa Assisi alipokutana na Sultan Al- Malik ak Kamil, kielelezo cha waamini waliokuwa na kiu ya amani, waliokuwa wanatafuta fadhila ya amani na kwamba, wajumbe wa mkutano huu wana kiu ya amani, wanataka kudumisha amani na kuwa ni vyombo vya amani. Kama familia moja ya binadamu, wote wanapaswa kuingia katika Sanduku la Agano, ili kujikinga na mawimbi mazito ya bahari yanayoendelea kuuandama ulimwengu.

Jambo la msingi kwa waamini ni kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye asili ya familia ya binadamu, kumbe, ni wajibu wao kuishi kama ndugu wamoja, sanjari na kutunza mazingira nyumba ya wote. Udugu ni sehemu muhimu sana ya ubinadamu unaofumbatwa katika mpango wa kazi ya uumbaji. Kumbe, watu wote wameumbwa kwa utu sawa na hakuna anayeweza kuwa mtawala na mwingine mtumwa! Changomoto kubwa ni kulinda na kudumisha utakatifu wa maisha, kama njia ya kumtukuza Mwenyezi Mungu. Vita, kinzani na mipasuko mbali mbali inapaswa kushutumiwa na wapenda amani duniani na kwamba, ni kinyume kabisa baadhi ya watu kutumia dini au jina la Mungu kwa ajili ya kusababisha vita, kinzani na mipasuko.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, adui mkubwa wa udugu ni ubinafsi unaohatarisha hata ibada na uchaji wa Mungu. Ibada ya kweli inasimikwa katika upendo kwa Mungu na jirani, kiasi cha watu kujisikia kuwa ni ndugu wamoja na hivyo kuondokana na dhana ya kuwafikiria wengine kuwa ni adui au marafiki. Waamini wa dini mbali mbali hawana budi kuvunjilia mbali kuta za utengano, ili waweze kuipata mbingu. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuipongeza nchi ya Umoja wa Falme za Kiarabu kwa kukuza na kudumisha: maridhiano, uhuru wa kidini na uhuru wa kuabudu; mambo msingi yanayomwezesha mtu kufikia utimilifu wake. Kamwe dini zisitumiwe na wajanja wachache kama chombo cha vita na vitendo vya kigaidi.

Udugu unafumbata tofauti msingi zinazojitokeza kati ya watu, lakini kwa kutambua kwamba, wote wana asili na utu sawa; watu wa dini na imani zao mbali mbali zinazobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, aliyewaumba kwa sura na mfano wake. Changamoto kubwa kwa waamini katika ulimwengu mamboleo ni kusaidiana na kuendelea kuboresha udugu kwa njia ya upendo na mshikamano. Waamini watambue kwamba, wao ni sehemu ya familia ya Mungu na wanapaswa kuwa na ujasiri wa kuthamini na kuendeleza tofauti zao; uhuru na haki msingi za binadamu. Uhuru unawafanya kuwa ni watoto wa familia ya binadamu. Kumbe uhuru wa kidini unapaswa kupewa uzito wa pekee.

Baba Mtakatifu amegusia majadiliano ya kidini na maisha ya sala! Majadiliano yanapaswa kujikita katika ukweli, nia njema pamoja na mtu mwenyewe kujiheshimu na kuwaheshimu wengine. Sala ni mazungumzo na Mwenyezi Mungu, yanayomwezesha mwamini kutakasa moyo wake, kujenga na kudumisha udugu ili kuombeana kama ndugu wamoja. Lengo ni kudumisha amani, umoja na utulivu wa familia moja ya binadamu sanjari na kuheshimu tofauti zao msingi. Dini ziwe ni madaraja ya kuwakutanisha watu na tamaduni zao; vyombo vya upatanisho, matumaini na amani.

Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa elimu na haki mambo msingi katika kukuza na kudumisha amani duniani. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuwekeza katika elimu kwa vijana wa kizazi kipya, ili kukuza na kudumisha mahusiano na mafungamano ya watu katika medani mbali mbali za maisha. Elimu iwasaidie watu kufahamu: historia, tamaduni na imani zao badala ya kujifungia katika ubinafsi wao. Kuwekeza katika sekta ya elimu kutasaidia sana kupunguza chuki na uhasama na matokeo yake ni kudumisha ustaarabu, ustawi na maendeleo ya wengi. Shule ni mahali pa watu kujipatia: ujuzi na maarifa; ni mahali pa kujenga na kudumisha amani pamoja na hali ya kufahamiana ili kudhibiti mipasuko.

Elimu bora iwasaidie vijana kuwa na uhakika wa habari na kuondokana na tabia ya kumezwa na habari za kughushi ambazo mara nyingi zinawatumbukiza katika kishawishi cha ulaji wa kupindukia, chuki na maamuzi mbele. Vijana wajifunze kulinda na kutetea haki msingi za binadamu; kwa kukutana na kusaidiana kistaarabu. Vijana wataweza kutoa hukumu ya haki, ikiwa kama watarithishwa tunu msingi zinazoweza kuwakutanisha katika ustaarabu. Haki ni sehemu muhimu sana ya amani duniani inayopaswa kuongozwa na Kanuni ya Dhahabu “Basi yoyote myatakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo; maana hiyo ndiyo torati na manabii”.

Haki na amani ni sawa na chanda na pete, kwani ni mambo yanayotegemeana na kukamilishana. Hii ni changamoto kwa viongozi wa dini mbali mbali kuhakikisha kwamba, wanawaelimisha waamini wao kuwa makini na kamwe wasikubali kutumbukia katika uchoyo kwa kumezwa na mahitaji ya soko la dunia. Matokeo yake, ni kukosekana kwa mchakato wa watu kukutana, majadiliano pamoja na kuharibika kwa misingi bora ya kifamilia; mambo yanayohitaji muda na uvumilivu. Dini inapaswa kuwa ni sauti ya maskini na wanyonge duniani pamoja na kuwa ni chombo muhimu cha udugu, tayari kukemea ukosefu wa haki na mambo yote yanayowatumbukiza binadamu katika majanga ya maisha!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, udugu ni Sanduku la Agano na kwamba, kuna haja ya kubadili majangwa yanayowazunguka binadamu kuwa ni mahali pa maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu kama ambavyo nchi ya Umoja wa Falme za Kiarabu imekuwa ni daraja la maendeleo linalotoa fursa za ajira kwa watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia! Adui mkubwa wa udugu na maendeleo fungamani ni ubinafsi. Novemba 2018 mjini Abu Dhabi kulifanyika mkutano wa majadiliano ya kidini kimataifa kuhusu mshikamano kwa ajili ya ulinzi wa jumuiya, ili kulinda na kudumisha utu na heshima ya watoto wadogo katika ulimwengu wa kidigitali. Baba Mtakatifu amechukua fursa hii kuunga mkono viongozi wote wa kidini wanaoendelea kusimama kidete kulinda na kudumisha haki msingi za watoto sehemu mbali mbali za dunia.

Baba Mtakatifu anasema, “Jangwa la Umoja wa Falme za Kiarabu” limegeuka kuwa ni kitovu cha maendeleo na fursa za ajira kwa watu kutoka katika mataifa, tamaduni la lugha mbali mbali na kati yao wamo Wakristo ambao pia wanaendelea kuchangia katika ustawi, maendeneo na mafao ya wananchi wa Umoja wa Falme za Kiarabu. Wamekuwa pia ni mashuhuda wa imani yao, hali ambayo inakuza na kudumisha utamaduni wa watu kukutana pamoja na ujenzi wa maridhiano kati ya watu; mambo ambayo yamewawezesha kupata nyumba za ibada pamoja na ukomavu wa maisha ya kiroho; mambo yanayopaswa kuendelezwa zaidi!

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, tunu hizi msingi zitaweza pia kumwilisha huko Mashariki ya Kati. Lengo ni kuhakikisha kwamba, hata watu wenye imani tofauti wanakuwa na haki sawa za kiraia ili kulinda na kudumisha amani na utulivu. Udugu unaowawezesha watu kuishi kwa pamoja katika misingi ya elimu na haki; maendeleo fungamani ya binadamu pamoja na kudumisha haki sawa kwa wote ni muhimu sana katika kukuza na kudumisha dini sehemu mbali mbali za dunia. Hii ni dhamana inayopaswa kuendelezwa. Mashindano ya silaha, uchu wa makoloni mapya na sera kandamizi pamoja na vita ni kati ya mambo yanayosababisha maafa na majanga makubwa katika maisha ya watu. Udugu wa kibinadamu uwasaidie viongozi wa kimataifa kuondokana na vita ambavyo vimekuwa na athari kubwa katika maisha ya watu huko nchini Yemen, Syria, Iraq na Libya.

Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu anawaalika viongozi wa kidini kushikamana kupinga falsafa ya mtumizi ya nguvu na fedha; ujenzi wa kuta zinazowatenganisha watu pamoja na vitisho vya wanajeshi wenye silaha wanaolinda mipaka pamoja na umaskini unaowaandama wengi. Viongozi wa dini, wasimame kidete katika nguvu ya sala na majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kuheshimiana na kuthaminiana, ili kuzuia mafuriko ya vita pamoja kuwasukumizia jirani katika majangwa ya maisha. Mwenyezi Mungu daima yuko pamoja na wale wote wanaotafuta amani!

Papa: Mkutano wa Kimataifa

 

04 February 2019, 16:48